Mgombea urais wa Zanzibar Balozi Ali Karume akisalimia baadhi ya wanachama wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni. Picha ya maktaba.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye ni miongoni mwa mawaziri 13 waliochukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana alirejesha fomu hiyo kimya kimya huku akikwepa kuzungumzia safari yake ya kusaka wadhamini katika mikoa 23 aliyopita.
Magufuli aliyechukua fomu hiyo Juni 5, mwaka huu, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma, zikiwa ni siku mbili tangu chama hicho kifungue milango kwa wagombea urais kuchukua fomu.
Hata hivyo, Dk. Magufuli, hakuwahi kutangaza nia wala kuzungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari kama walivyofanya makada wenzake waliojitosa kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Tangu alipotangaza nia, Dk. Magufuli hajawahi kueleza vipaumbele vyake iwapo atateuliwa na chama chake kugombea kiti hicho, wala kujinasibu kama wagombea wenzake wanavyofanya kila mkoa waliopita kusaka wadhamini na kisha kupewa fursa ya kuzungumza na wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla.
Akiwa Makao Makuu ya CCM mjini hapa, Waziri Magufuli alikabidhi fomu yake kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab Luhwavi, saa 4:10 asubuhi ikiwa na wadhamini 450 pekee.
Magufuli (kulia) akikabidhi fomu za wadhamini wake katika kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM kwa naibu katibu mkuu wa chama hicho (Bara), Rajab Luhwavi, mjini Dodoma jana.
Mkitaka niwakabidhi pia kuonyesha ninavyokubalika nitawapa,” alisema na kuongeza: “Mheshimiwa huko kote nilikokwenda nilikuwa natumia ramani ambayo inaonyesha nimepita wapi na wapi? Nimekuja nayo naomba nikukabidhi Mheshimiwa Naibu Katibu Mkuu Bara.” Alipomaliza aligoma kuzungumza na vyombo vya habari na kuondoka.
BALOZI KARUME
Balozi Ali Karume, jana alirejesha fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais huku akieleza kuwa kutokana na changamoto alizokutana nazo katika safari ya kusaka wadhamini; akichaguliwa kupeperusha bendera ya chama chake na baadaye Watanzania wakampa ridhaa ya kwenda Ikulu, atachukua uamuzi mgumu wa kupunguza kodi zinazowanyonga wananchi wa kawaida.
“Nikiwa Rais, nitapunguza kodi zinazowanyonga wananchi wa chini; lengo langu ni kulipeleka taifa kwenye uchumi wa kati na kuiacha nchi kwenye amani na utulivu. Ni lazima katika utawala wangu niutetee kwa nguvu zote Muungano,” alisema Balozi Karume.
Karume ambaye ni mwanadiplomasia, alimkabidhi fomu hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab Luhwavi, saa 10:28 jioni, Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma baada ya kuzunguka mikoa yote ya Zanzibar na mikoa kadhaa ya Tanzania Bara.
Baada ya kukabidhi fomu hiyo; Karume alisita kuitaja idadi ya mikoa aliyopita kusaka wadhamini wake, akisema: “Nimezunguka mikoa yote ya Bara lakini hampaswi kujua, isipokuwa nimepita mikoa ya kutosha.
Itoshe kusema tu kwamba nimekuwa mgombea wa sita kurejesha fomu na mgombea wa nane kuchukua fomu Juni 4, mwaka huu…Nimepata wadhamin 450 tu na wengine waliojitokeza kunidhamini niliwaacha na kuwaomba radhi,” alisema Balozi Karume.
Mbio za kugombea urais hazikuanza leo kwa Balozi Karume, kwa kuwa mwaka 2000 alitangaza nia na kuingia katika kinyang’anyiro cha uteuzi ndani ya CCM kwa upande wa Rais wa Zanzibar, lakini alijitoa katika hatua za awali na kumuachia nduguye, Amani Abeid Karume.
Mwaka 2005 na mwaka 2010, alijitosa katika kugombea uteuzi wa chama chake ili apeperushe bendera ya CCM kwa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia bahati haikuwa yake.
WASIRA
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, ambaye naye alirejesha fomu hiyo saa 7:47 mchana, akiwa amesindikizwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine alisema:
“Kama mnavyotuona na wenzangu hapa, afya yangu ni nzuri na haina taabu, nimefanya majaribio ya kutembea nchi nzima kuona kama afya yangu iko safi.
Nasubiri nikiteuliwa na kuingia kwenye mshike mshike wa siku 90 za kampeni za uchaguzi mkuu, nitawachezesha ‘kwata’ hao wanaojiita Ukawa (Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi) hadi tutakapoachana njia ya kwenda Ikulu.”
Wasira alipoulizwa iwapo anaweza kuwapiku wagombea wenzake ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuteuliwa, alisema amewaomba Watanzania huko alikopita wafunge kwa sala na kumuombea atinge katika hatua ya tano bora, tatu bora na kisha awe mteule wa CCM atakayepeperusha bendera katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
KIGWANGALLA: KIZAZI CHA VIJANA, WAZEE WASHAURI
Mgombea mwingine wa urais kupitia (CCM), Dk. Khamis Kigwangalla, amewaeleza wanachama wa chama hicho kuwa Taifa linahitaji viongozi vijana katika kuongoza nchi, huku nafasi ya wazee ikibaki kwenye kushaurina na kutoa maelekezo pale watakapobaini kuna tatizo.
Dk. Kigwangalla alitoa kauli hiyo jana mjini Lindi alipokuwa akizungumza na wanachama waliokuwa wamejitokeza kumdhamini katika kinyang’anyiro hicho kinachotarajia kukamilika Julai 12, mwaka huu kupitia CCM.
Akizungumza na wanachama wa CCM Makao Makuu ya chama hicho mkoani Lindi, Dk. Kigwangalla alisema ameamua kuomba nafasi hiyo akisema anajiamini na anayo maarifa ya kutosha katika kuliongoza Taifa iwapo atapewa ridhaa hiyo.
Dk. Kigwangalla ambaye pia ni Mbunge wa Nzega, alisema anazifahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania zikiwamo masuala mazima ya dunia ya leo pamoja na ya kupata ukombozi.
Aidha, alipinga madai yanayotolewa na baadhi ya watu kwamba vijana hawastahili kushika madaraka hayo ya juu yakiwamo ya urais, hayana msingi kwani wazee tayari wamefanya kazi kubwa ikiwamo kuwasomesha na kupigania uhuru wa nchi yao.
“Hivi sasa kumekuwa na maeneo mengi yanasemwa kuhusiana na uzoefu na uongozi…watu wengine wanasema vijana wadogo sana wana haraka ya kutaka madaraka makubwa tofauti na umri walionao,” alisema Dk. Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla alisema wakati umefika kwa wazee wakapumzika kutokana na kazi kubwa waliyoifanya na kuiachia fursa hiyo kwa vijana ambao wana nguvu za kutosha na chachu ya kuliletea Taifa maendeleo.
Alisema iwapo Chama kitampa tiketi na Watanzania wakampatia ridhaa, atahakikisha serikali atakayoiunda ndani yake mnakuwa na wazee kwa ajili ya kusaidia ushauri pamoja na kuwapa kumbukumbu ya mambo yaliyokuwa yanafanyika siku za nyuma.
Kwa mujibu wa Dk. Kigwangalla, zama za wazee kuongoza Taifa zilianza wakati wanapigania Uhuru wa Taifa nao hawakuwa ni wazee bali vijana.
“Mawaziri wote wa serikali ya awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, miaka ile ya 60 tulipokuwa tunapata Uhuru wetu, walikuwa vijana kati ya umri wa miaka 25 na kuendelea na ndiyo hao hao mpaka leo wanaendelea kuwapo,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alifafanua kuwa matamshi yanayotolewa na baadhi ya watangaza nia kuwa wao ndiyo wenye uwezo na sifa ya kuliongoza Taifa, hayana msingi kwani wote wanaoiomba nafasi hiyo hakuna aliyekwisha ifanya.
“Nafasi hii tunayoiomba kwenu hivi sasa kama ningekuwa nagombea na wazee kama vile mzee Mwinyi, Mkapa na sasa Kikwete anayemaliza muda wake, nisingekuwa na ubishi kwani ndiyo wenye uzoefu kwani wamepitia kazi hiyo ya urais,” alisema Dk. Kigwangalla. Dk. Kigwangalla alipata wadamini 35 mkoani Lindi.
MWINGINE ACHUKUA FOMU
Katika hatua nyingine, Ofisa Maendeleo ya Jamii, Ritha Peter Ngowi (50), mkazi wa Kilimanjaro na Dar es Salaam, amekuwa mwanamke wa tano kutangaza nia ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais akieleza iwapo chama chake kitamteua na kisha Watanzania kumpa ridhaa; atahakikisha anatenga kambi maalum itakayowaweka pamoja watu wenye ulemavu na wengine wenye hali inayofanana na hiyo ili kuwapa ujuzi utakaowahakikishia uhakika wa kuwa na kipato kwa maisha yao yote.
Wanawake wengine waliojitosa kugombea kiti hicho ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Naibu Waziri wa zamani wa Fedha na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Monica Mbega; Balozi Amina Salum Ali na Dk. Mwele Malecela.
"...nikiwa Rais, sitaki awapo Mtanzania yeyote ambaye hana kipato cha kumwezesha kuishi na kwa kuanzia nataka kila Mtanzania apate elimu stahiki,” alisema Ritha.
Mgombea huyo alisema iwapo CCM itampa ridhaa na Watanzania kumuamini na kumchagua kuwa Rais wao, atahakikisha kwamba wafanyakazi wa serikali na taasisi za umma wanakuwa na mishahara minono ambayo itawawezesha kuishi bila ya kutegemea hisani wala mikopo ambayo hukwangua miamala yao ya kibenki katika taasisi za fedha. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment