MGOMBEA URAIS NDANI YA CCM, BENARD MEMBE AMKANA RAIS JAKAYA KIKWETE MCHANA KWEUPE.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, amekana kuwa na undugu wa damu na Rais Jakaya Kikwete.
Membe (62) ambaye Juni 8 mwaka huu alitangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na kisha jana kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea kiti hicho, alisema ingawa amekuwa akifananishwa na Rais Kikwete mara kadhaa; hakuna ushahidi wowote wa kibailojia unaothibitisha kwamba wana uhusiano wa kindugu.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukuwa fomu hiyo kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma jana, Membe alisema baadhi ya watu wamekuwa wakimfananisha na Rais Kikwete lakini hawana undugu wowote baina yao.
“Kungekuwa na aibu gani au hasara gani kuficha kwamba mimi ni ndugu wa damu wa Rais Jakaya Kikwete. Mimi siyo ndugu wa mheshimiwa Rais, lakini binadamu tunafanana…rangi yangu, sura yangu na ufupi wangu nimeuchukua kwa mama yangu,” alisema Membe na kuongeza:
”Aliyekuwa Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika (sasa marehemu) wakati fulani pia aliwahi kunifananisha na Rais Kikwete. Naomba nitamke wazi kwamba sina undugu wa damu na mheshimiwa Rais.”
Alisema hali hiyo pia iliwahi kumkuta baada ya Wamarekani weusi (Afro Americans) kumkaribisha Marekani wengi walimuomba kupiga naye picha wakidhani ni Rais Kikwete lakini baadaye aliwaeleza ukweli kwamba yeye hakuwa Rais Kikwete.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kisesa (CCM) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara; Luhaga Mpina ambaye naye ametangaza nia ya kuwania nafasi ya Urais kupitia chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu mjini hapa jana alisema akipata ridhaa ya chama chake na baadaye watanzania wakimwamini na kumchagua atahakikisha anasimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali ili yapande mara mbili au tatu zaidi ya sasa pamoja na kusimamia rasilimali za umma ziwanufaishe wanyonge badala ya wachache.
“Mimi si mdogo wala mtu wa kudharauliwa katika wagombea waliotangaza nia ya kugombea urais. Mkitaka kujua mimi naweza fuatilieni, mimi ndiye mbunge wa kwanza Afrika kusimama hadharani na kuzungumzia utoroshaji wa mabilioni ya fedha kwa nchi za Afrika kwenda ughaibuni. Ndiye
niliyesababisha Afrika ikaunda kamati iliyoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini, Thabo Mbeki kushughilikia suala hilo kwa nchi za Afrika,” alisema Mpina.
Hadi kufikia jana mchana makada wa CCM waliotangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho na kisha kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania kiti hicho walifikia 20. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment