MKULIMA WA DARASA LA SABA ACHUKUA FOMU RASMI ZA KUGOMBEA URAIS, AWAPIGA MKWARA MZITO AKINA LOWASSA, MEMBE MJINI DODOMA.
Elidephonce Bilohe akionyesha begi lenye fomu za kuomba kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM mjini Dodoma jana.Picha na Edwin Mjwahuzi.
Dodoma. Makada sita wa CCM jana walijitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama hicho kupitishwa kugombea urais, akiwamo mkulima mwenye elimu ya msingi, Elidephonce Bilohe ambaye alisema “haoni mtu tishio” kwake kwenye mbio hizo.
Makada wengine waliochukua fomu jana ni mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hass Kitine, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, Naibu Waziri wa Sayansa, January Makamba, mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Boniface Ndengo.
Bilohe awa kivutio
Uchukuaji fomu jana ulinogeshwa na Bilohe ambaye wakati anaingia kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, alishangiliwa kwa kuitwa “rais, rais, rais” na watu waliokuwa eneo hilo.
“Sioni mtu nayemuogopa, sioni tishio kwangu zaidi ya mimi kuwa tishio kwa wagombea wengine,” alisema Bilole baada ya kuchukua fomu.
Bilole alitinga kwenye ofisi hizo saa 10:00 jioni na kuchukua fomu yake kisha akataja vipaumbele vyake kuwa pamoja na ajira kwa vijana, kuboresha maisha ya wazee na wastaafu na akawataka Watanzania wamuombee.
Alipoulizwa kiwango chake cha elimu, alijibu, “nimesoma elimu ya Taifa ambayo ni darasa la saba, lakini mkumbuke sikuja hapa kucheza wala siigizi”.
Hata hivyo, katibu wa sekretarieti ya CCM, Dk Mohamed Seif Khatibu aliiambia Mwananchi kuwa huu ni wakati wa kupokea wagombea, lakini utafika wakati wa kuwachuja kwa kufuata vigezo vya kikatiba, likiwemo suala la elimu.
Kichekesho kikubwa kwa mgombea huyo kilikuwa wakati alipokuwa akisaini kitabu cha wagombea. Alianza kuzungumza na simu akitaarifu yanayoendelea mjini hapa.
“Shikamoo mzee, tayari nimechukua na hapa ndiyo nakabidhiwa hivyo kila kitu kinawategemea nyinyi,” alisema wakati akizungumza na simu hiyo.
Simu hiyo ndogo aina ya Nokia, maarufu kama tochi, iliendelea kuita wakati akizungumza na waandishi wa habari na hakusita kupokea.
Chikawe ajitosa
Chikawe alijitosa jana kwenye mbio hizo na kuwa waziri wa tano kuchukua fomu ya kuomba kugombea urais.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
“Nataka niwahakikishie tangu mapema kwamba mimi ni mwanachama muadilifu wa CCM na ninaomba urais ili niongoze utekelezaji wa sera za chama changu ambazo zitaainishwa na ilani ya chama,”alisema Waziri Chikawe ambaye hakuwa akitajwa wala hakutangaza nia ya kugombea urais.
Chikawe ni nani?
Chikawe alizaliwa Mei 30 mwaka 1951 katika kijiji cha Mnero Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi. Alisoma Shule ya Msingi ya Mkonjela iliyoko Nachingwea na Shule ya Msingi Police Line iliyoko Mgulani jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1959 na 1965.
Mwaka 1966 hadi 1969, alisoma Sekondari ya St. Joseph ya Dar es Salaam, kabla ya kwenda Shule ya Sekondari ya Mkwawa mkoani Iringa kati ya mwaka1970 na 1971 kwa masomo ya kidato ya tano.
Mwaka 1975 alimaliza Shahada ya Sheria Chuo Kikuu cha Dares Salaam na mwaka 1978 alihitimu Stashahada ya Juu ya Utawala nchini Uingereza. Chikawe pia ana Stashahada ya Juu ya Sheria za Kimataifa kutoka taasisi ya Elimu ya Jamii ya Uholanzi aliyoipata mwaka 1982
Mwaka 1976 alianza kazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu akiwa mwanasheria wa Serikali Daraja la III na baadaye kuhamishiwa wizara mbalimbali, ikiwemo Ikulu.
Amekuwa mbunge wa Nachingwea tangu 2005 na kuanzia hapo amekuwa akishika nafasi mbalimbali serikalini ikiwamo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Utawala Bora na Waziri wa Katiba na Sheria. Sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Nitakomesha Rushwa-Ndengo Kada mwingine, Ndengo alichukua fomu akiwa na kaulimbiu ya “gia mpya na kubadili taswira ya Tanzania”. Alisema maadui wakubwa wa Taifa ni rushwa na ujinga ambao leo hii vinazaa ufisadi. “Umaskini katika maana rahisi ni hali ya kukosa mali au kipato. Katika maana pana umasikini ni muunganiko wa mambo yanayosababisha ukosefu wa mahitaji muhimu kila jambo likikuza na kuongeza ukubwa wa tatizo,” alisema.
“Matokeo ya umaskini ni kwamba kizazi baada ya kizazi tutakosa elimu bora, huduma bora za afya, tutakosa makazi bora na lishe bora. Matokeo mabaya zaidi ni kukata tamaa, kukosa ubinadamu na hatimaye kukosa matumaini.
“Nikipata ridhaa ya wana-CCM nitapambana na kutokomeza rushwa katika kipindi cha mwaka mmoja.”
Alisema atatumia nyenzo ya uwajibikaji na uwekezaji wenye tija kufanikisha suala hilo.
“Tunayo sababu ya kuona aibu kwamba miaka hamsini ya uhuru bado wako Watanzania wanaoishi kwa kula mlo mmoja, bado kuna watoto wanaozaliwa wakiwa hawana uhakika wa kupata elimu bora,” alisema.
Sijathibitika na kashfa -Ngeleja
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Ngeleja alisema wakati akichukua fomu jana kuwa alikumbwa na kashfa lakini hajathibitika kuwa na upungufu. Aliwataja watu wa Afrika waliokumbwa na kashfa, lakini baadaye wakaja kuwa marais kuwa ni pamoja na Uhuru Kenyatta wa Kenya na Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
“Kwa mujibu wa taratibu za nchi yetu tunavyoziendesha, sijawahi
kuthibitika kuwa na mapungufu yote,” alisema waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini.
Kuhusu mgawo wa Sh40.4 aliopewa na mmoja wa wamiliki wa zamani wa kampuni ya IPTL, James Rugemalila, Ngeleja alisema alilipa kodi na alizitumia kwa maendeleo ya wananchi.
Makamba asema urais ni taasisi
Kwa upande wake Makamba, alisema urais si mtu bali ni taasisi yenye mamlaka na madaraka makubwa. Kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alisema endapo atapata nafasi hiyo ataenda mbele zaidi ya alipoishia Rais jakaya Kikwete.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment