BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NI MATUMBO JOTO NA WIKI NGUMU KWA WATIA NIA 42 NDANI YA CCM, NANI ANAFAA KUPEPERUSHA BENDERA KATIKA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 25 ?.

 
Mtia nia Edward Lowassa.
 
WIKI hii ni ya mwisho kwa watia nia ya urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kurejesha fomu baada ya kuzunguka nchi nzima kuomba wadhamini, hata hivyo jana mwanachama mwingine wa CCM alichukua fomu na hivyo kufanya idadi ya watia nia hao kufikia 42.

Kada huyo Banda Sonoko alijigamba kuwa ana uwezo wa kuipeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu unataotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, kwani ana vigezo, sifa na uwezo wa kuvaa viatu vya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu kwenye makao makuu ya chama, alisema anajiamini kuwa ana uwezo wa kuongoza taifam jambo ambalo limemsukuma na kuamua kuchukua fomu.

Sonoko, ambaye kwa taaluma ni mwalimu, alisema ana uwezo wa kuvaa viatu vya Baba wa Taifa, ambavyo kwa sasa wengi wanavitamani. ‘‘Kwa sasa wengi wanatamani kuvivaa, lakini mtu pekee vinayemtosha ni mimi.” Alisema katika uongozi wake yeye ni muumini wa muda hivyo atahakikisha anafanya kazi ili kuiondoa nchi katika misukosuko ya kiuchumi.

Aidha aliahidi kuweka usimamizi madhubuti wa serikali yake katika uchumi wa kilimo na kufufua viwanda ili kuhakikisha nchi inarudi katika kilimo.

Pia alisema atahakikisha serikali yake inakusanya kodi ili nchi iweze kujiendesha kutokana na kodi inayokusanywa. Mwisho Alhamisi Ni siku nne zimebaki ili kufikia tamati ya kuchukua na kurudisha fomu.

Hata hivyo mgombea huyo urais hakueleza atatumia mbinu gani kwenda angalau mikoa 15 inayotakiwa na CCM kusaka wadhamini ili aweze kukidhi vigezo vya jina lake kujadiliwa na vikao husika.

Kila mwanachama aliyechukua fomu anatakiwa kuwa wadhamini 450 katika mikoa 15 ambapo mitatu iwe ya Zanzibar. Waliorudisha fomu ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Makongoro Nyerere, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Steven Wassira na Balozi Ally Karume.

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Balozi Amina Salum Ally, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Agustino Ramadhani, Leone Murenda, Profesa Mark Mwandosya na Boniface Ndembo.

Watia nia wazidi kujitapa Wakati hayo yakiendelea baadhi ya wagombea urais wamezidi kujitapa mikoani ambako wanatafuta wadhamini huku wakieleza yale ambayo wataenda kuyafanya mara watakapoteuliwa na chama chao kugombea urais na baadaye kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Fadhili Abdallah anaripoti kutoka Kigoma kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake, haviwezi kutishwa na mtu yeyote katika kutekeleza maamuzi yoyote kutokana na kuwa na historia ya kuwa na msimamo usioyumba na uongozi thabiti.

Membe, ambaye ni miongoni mwa wana CCM waliotangaza nia ya kuwania urais kupitia chama hicho, amesema yeye binafsi hatokuwa na kinyongo kwa maamuzi yoyote yatakayochukuliwa na chama hicho hata ikiwa yatakuwa maamuzi machungu kwake.

Akizungumza na wanachama wa CCM wa mkoa wa Kigoma waliofika kumdhamini juzi Jumamosi, Membe alisema Watanzania wakatae vitisho na ulaghai kutoka kwa mtu yeyote katika maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Watanzania tukatae aina yoyote ya vitisho wala ulaghai katika uchaguzi wetu. Sisi na wengine katika makundi yetu tutakaa kusubiri maamuzi sahihi ya chama chetu, ambacho hakikufanya makosa miaka yote ya nyuma… “Tutaheshimu maamuzi yatakayotoka Dodoma siku ile hata yangekuwa machungu kama pilipili.

Na ole wao ama ole wake mtu yeyote atakayejitia kuletaleta bughudha pale eti kwa kisingizio kwamba eti chama hakikuchukua hatua sahihi, mtachukua hatua sahihi maana mna uzoefu wa kufanya hivyo.

“Ndugu zangu Watanzania kataeni upuuzi wa aina hiyo, angalieni vigezo mkiangalia familia zenu kwamba na kuhoji kama nikimpa huyu kesho nitakuwa salama!” Alisema Membe huku akishangiliwa na wana CCM waliokuwapo.

Alisema ni wajibu wa wana CCM kumpa uongozi ambaye wakiangalia watakuwa na imani kwamba nchi na familia zao zitakuwa salama na heshima na amani ya nchi itakuwa katika mikono salama na si vinginevyo.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Kigoma alikomalizia mkoa wa 31, Membe alisema ataimarisha miundombinu ya reli na barabara na kuwasaidia kupata mwekezaji atakeyefanikisha mpango huo.

Alisema kampuni moja ya Kichina imeonesha nia ya kuboresha huduma ya reli ikiwa ni pamoja na kujenga reli ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Kigoma ambayo itawezesha safari ya siku moja.

Membe, ambaye amekuwa akiahidi kusimamia uchumi wa viwanda unaotegemea kilimo, alisema viongozi waliotangulia akiwamo Rais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, wameweka misingi imara katika maendeleo, na hivyo itakuwa ni rahisi kwake kuendeleza walipoishia.

Jana alipokuwa Sumbawanga na Mpanda, alimsifia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye alisema ni mmoja wa watangaza nia mwenye sifa za kuwa kiongozi wa nchi kutokana na historia yake ya uadilifu ndani na nje ya serikali na kwamba ingekuwa si mwanasiasa huyo angekwisha kujiona mteule ndani ya CCM.

Makamba Naye John Mhala anaripoti kuwa Mgombea urais kupitia CCM,Januari Makamba amesema anaamini kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitawaletea Watanzania mgombea urais atayekubalika mbele ya wananchi wote na sio vinginevyo.

Kauli hiyo alisema hayo katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Arusha mara baada ya kupata wadhamini 2,237 waliojitokeza kumdhamini nafasi hiyo ndani ya chama.

Makamba alisema CCM haiwezi kuteua mgombea ambaye hakubaliki na wananchi kamwe; bali itamteua mgombea wake ambaye anakubalika na wananchi na watamkubali kwa asilimia kubwa.

Alisema kwa sasa Watanzania wanataka mabadiliko ndani ya chama na mabadiliko hayo ni kumtaka mgombea mpya mwenye mtazamo mpya na malengo mapya kwa maslahi ya nchi sio wale wale wa miaka yote.

Makamba ambaye alikuwa akihutubia kwa umakini mkubwa, alinukuu hotuba ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1995 katika mkutano mkuu wa chama ambapo alisema kuwa nanukuu, Alisema kutokana na hali hiyo chama kitafanya mabadiliko ndani ya chama kwa kumteua yeye kuwa mgombea urais kwani Watanzania wana imani naye kwa kuwa atakuwa na mambo mapya na mitazamo mipaya ya kuiongoza nchi hii.

Akizungumza ajira kwa vijana alisema Mkoa wa Arusha una vitu vingi kwa vijana kupata ajira akiwemo Utalii, madini, viwanda, kilimo na biashara ndogo ndogo na kusema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa mgombea urais ana uhakika wa kubuni mambo mapya kwa vijana kupata kupitia vitu hivyovitano.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: