Ni miezi takriban kama mitatu na nusu imesalia Watanzania wenye sifa za kupiga kura wakapige kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi, wakiwamo wabunge, madiwani na rais.
Uchaguzi ungekuwa soka, tungeweza kusema tupo katika dakika za majeruhi, lakini ukweli ni kwamba hata huo uchaguzi tunaouelekea upo katika dakika za majeruhi.
Nawaasa Watanzania wenzangu kwamba tusidanganyike na maneno ya wagombea. Tuyapime wayasemayo na tuyachuje kwa chujio lenye tundu nyembamba kwani wengine wanatumia kila namna mbinu ilimradi waingie Ikulu. Wako tayari hata kuhonga kufikia ndoto yao hiyo.
Jambo la kushangaza ni kuwa tabia ya kupokea hongo kutoka kwa wasaka uongozi imekuwa maarufu na inayokubalika na Watanzania wengi. Hadi imefikia kuwa asiyetoa rushwa hathaminiki na nafasi yake ya kupita katka nafasi yoyote ile ni ndogo.
Tena jambo la kushangaza miongoni mwa wagombea ambao wanataka kuongoza nchi, walishawahi kuwa viongozi tena walikuwa na nyadhifa za juu serikalini. Tujiulize pia wakati wanatuongoza kipindi kile walishindwa nini kuweka mambo sawa serikalini au hayo matatizo wanayoyaongelea leo ndiyo yanatokea wakati wao wapo nje ya uongozi?
Nawaonya Watanzania kuwa makini kwa kutokubali kuvurugwa na watu wanaotangaza nia ya kugombea urais na ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, badala yake tufanye uamuzi sahihi kwa kumchagua kiongozi atakayekuwa tayari kulinda rasilimali za nchi yetu.
Kabla ya kufanya uamuzi, tuwaulize watangazania je, wana mikakati gani ya kulinda rasilimali zetu na kuzitumia rasilimali tulizonazo kwa masilahi ya taifa?
Je, tutakuwa na uhakika gani kama tukiwapa dhamana ya kutuongoza, hawatatumia rasilimali zetu kujinufaisha wao, familia zao na rafiki zao?
Tuwasikilize kwa makini na baadaye tumchague mtu ambaye ataweza kulinda masilahi ya Watanzania wote siyo masilahi ya familia yake na kundi fulani lililokuwa likimshabikia wakati anaomba kura.
Tusimpime mtu uongozi kwa sababu tu katupa fulana, khanga, kofia, katununulia chakula na katupa nauli ya Sh20,000, kwani vitu hivyo dhalili vitatugharimu kwa miaka mitano ijayo. Kiongozi anayekushawishi umchague kwa kukupa zawadi ujue ana lake jambo, kamwe usimpe kura yako.
Sasa hivi mtawaona wagombea wengi wakija na nyuso za furaha mpaka nyumbani kwenu, wakiwasihi muwachague, huku wakitoa ahadi kedekede ambazo awali walizitoa na hawakuzitekeleza, hao msiwape nafasi, waogopeni kama ukoma.
Wananchi tunatakiwa kubadilika na siyo kila siku tunadanganywa na sisi tunakubali kama vile hatuoni mbele. Leo hii utachukua kitenge, sufuria, kofia au hata pesa ili umchague aliyekupa, lakini je, vitu hivyo utakaa nayo kwa miaka mitano? Je, shida zako za msingi zitakuwa zimetatuliwa? Jiulize kwanza kabla hujapokea hiyo rushwa na uipime rushwa hiyo na thamani ya maisha yako.
Haki ni kitu ambacho kinapiganiwa na siyo kutafutwa pekee. tuipiganie haki yetu ya kuwa na viongozi bora kwa kuchambua kauli zeo wenyewe.
Tuwasikilize na kuzichambua kauli zao ili tuweze kuwa katika mazingira mazuri zaidi ya kufanya uamuzi sahihi siku ya kupiga kura.
Nawasisitiza Watanzania tusipoteze haki zetu, tukajiandikishe kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili siku ikifika tutumie haki yetu ya msingi ya kuwachagua viongozi.
La muhimu siku hiyo ni kufanya uamuzi wa busara kwa kumchagua kiongozi bora.
Hussein Issa ni mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment