WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAKAZI AWAFANYA WAKAZI 4000 KATA YA BUNJU KUKENUA MENO NJE KISA KUTATUA MGOGORO NA MWEKEZAJI DAR.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi, hatimaye amewezesha kufikia tamati mgogoro wa ardhi wa muda mrefu uliohusisha wakazi wa Chasimba kata ya Bunju Wazo jijini Dar es Salaam.
Mgogoro huo umemalizika baada ya mwekezaji ambaye ni mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Twiga, kuitoa kuwa makazi ya watu.
Ardhi hiyo imetolewa kwa wakazi zaidi ya 4000 huku serikali ikiirasimisha rasmi kutoka eneo la machimbo ya kokoto na chokaa na kuwa makazi.
Waziri Lukuvi, alitangaza neema hiyo jana kwa wananchi husika ambao ni wa eneo la Cha Simba, Cha Tembo na Cha Chui.
Katika mkutano na wananchi hao, Lukuvi aliambatana na Naibu wake, Angela Kairuki, Katibu wa Wizara hiyo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Alfonso Rodriguez na watendaji wengine wa serikali.
Lukuvi alisema muafaka wa kurasimisha eneo hilo umetokana na serikali kukaa na mwekezaji huyo na kukubaliana chini ya masharti kadhaa.
Alitaja masharti hayo kuwa ni wananchi watakaohusika na eneo hilo ni wale tu ambao walikuwepo wakati upigaji picha za anga na tathmini ulipofanyika.
“Cha Tembo tumeona watu wanauza ardhi za wenzao na wengine kujiongezea, nawaomba muwe walinzi wa makubaliano tuliyofikia leo,” alisema na kuongeza:
“Tumekubaliana pia kuanzia leo eneo hili litakuwa la makazi na sio madini, kwa hiyo shughuli za uchumbaji eneo hili hazitakiwi tena mlindane na yale magari yanayopandisha huku kuchukua kokoto myapige stop,” alisema.
Lukuvi alisema mwekezaji huyo alilalamika kuwa wananchi wanachoronga mlima ambao una madini ya chokaa ambapo ni kinyume kwa sababu mwenye kibali na hati ya ardhi hiyo ni Rodriguez.
Aliwataka uchimbaji wamuachie mwekezaji huyo ambaye amekubali kutoa ardhi hiyo ambayo kila mwaka huilipia kodi.
Alisema mwekezaji huyo amekubali kusaidia eneo hilo kuwa na huduma za kijamii kama barabara, shule na zahanati.
Lukuvi alisema utaratibu utakaofanyika kwa wananchi watakaokutwa na sifa za kuishi hapo, watapewa leseni za kuishi ambapo shughuli zitakazotakiwa kufanyika hapo ni za kawaida.
Alisema kinachofuata ni uundwaji wa kamati ndogo za wawakilishi kutoka kwa wananchi wataalam kutoka wizara hiyo ambao watapanga makazi na maeneo yatakayojengwa huduma za kijamii.
“Msishangae wengine mkapangiwa maeneo mengine ya kujenga itakapotokea pale ulipo pakaonekana panafaa kuwa barabara au shule, wito wangu kamati hii ifanye kazi kwa haki na sio fitna na upendeleo wa kuangalia nani ni wa chama gani,” alisema.
Kwa wakazi wa Cha Tembo, Lukuvi alisema kuanzia wiki ijayo mwekezaji ataenda kuvunja nyumba kwa wale ambao hawaishi kihalali. Pia alisema kutakuwa na timu ya kupima ardhi kwa sababu wengine wana maeneo makubwa.
Alisema serikali imeamua kuwa atakayemilikishwa ardhi atalipa kodi kila mwaka na asilimia 30 itaenda Manispaa ya Kinondoni.
Naye, Rodriguez aliwaeleza wananchi hao kuwa wameamua kutoa eneo hilo na kwamba kiwanda kinatambua umuhimu wa huduma za kijamii kwao.
Mdee alisema wajibu wa kiongozi ni kuwapa raha wananchi na kwamba anaamini serikali itafanya hivyo. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI.
0 comments:
Post a Comment