Na Juma Mtanda, Mwananchi.
Zaidi ya wakazi 15,000 kati ya 24,560 katika Kata za Kibati na Pemba wameshindwa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza mkoani Morogoro.
Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Pemba na Kibati wilayani Mvomero, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Suleiman Sadiq alisema kutokana na idadi hiyo kuwa kubwa, ipo haja ya kurudisha zoezi hilo katika vijiji hivyo ili wananchi hao waweze kupata haki ya msingi ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mkutano huo ulilenga kuimarisha uhai wa chama sanjari na kuhamasisha wananchi kujua umuhimu wa kutunza vitambulisho vya Taifa vya mpigakura na wenye sifa na uwezo wa uongozi kujitokeza kuwania nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema Kata ya Pemba pekee ina wakazi 8,000 na waliojiandikisha ni 3,772 huku Kata ya Kibati ikiwa na wakazi 16,560 na waliojiandikisha ni 5,692.
“Nawahakikishie, nawasiliana na uongozi wa wilaya akiwamo mkurugenzi na mkuu wa Wilaya ya Mvomero ili kurudisha zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura katika vijiji hivyo,” alisema Sadiq.
Sadiq alisema kuwa, mkutano huo ni mwendelezo wa ziara iliyoanza tangu Juni 20 ya kutembelea Tarafa ya Mgeta ingawa katika tarafa hiyo hakukutana na malalamiko ya idadi kubwa ya wasiojiandikisha kama ilivyo kwenye vijiji vya Turiani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibati, Selemani Sudi akizungumza katika mkutano huo alisema kuwa, Serikali itilie mkazo suala la urejeshwaji wa mashine hizo katika kata hiyo kwani itasaidia watu wengi waliokosa kujiandikisha kupata nafasi hiyo.
“Nitahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari hilo pindi litakaporudi kwani shahada hizo zina muhimu na vinaweza kutumika kama kitambulisho cha Taifa.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM wilayani Mvomero, Abdalah Mtiga ametangaza kuwasamehe madeni ya ada ya uanachama wale ambao hawajalipa kwa kipindi cha miaka mingi na kuwataka walipe ada ya mwaka mmoja ili wapate nafasi ya kuchagua kiongozi anayefaa katika nafasi ya udiwani na ubunge kwenye kura ya maoni ndani ya CCM.
Mtiga alisema kuwa, wanachama wa CCM katika maeneo mengi wamekuwa wavivu kulipa ada na badala yake hulimbikiza madeni yanayokuja kuwashinda kulipa kwa wakati mmoja.
Alisema kwa kutumia sheria za chama na heshima yake ameamua kuwapunguzia madeni hayo ili waweze kupata fursa ya kuingia kwenye upigaji wa kura za maoni.

0 comments:
Post a Comment