
Serikali ya Kenya na wadau wa michezo nchini humo wameichangia mamilioni ya shilingi timu ya Gor Mahia kuhakikisha inakuja Tanzania kuikabili Yanga na klabu nyingine katika michuano ya Kombe la Kagame 2015, itakayoanza Jumamosi jijini Dar es Salaam.
Wiki iliyopita Gor, timu iliyoshindikana kufungwa katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu huu (ikiwa imecheza mechi 18 bila kupoteza hata moja; imeshinda 14 na kutoka sare mara nne, ilitishia kujitoa kushiriki michuano ya Kombe la Kagame baada ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuweka wazi haliko tayari kuwalipia tiketi za ndege kuja Tanzania.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Kenya imejitosa kuokoa jahazi baada ya jana kutangaza kuwa italipa gharama za tiketi za ndege kukirudisha kikosi cha watu 30 cha mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya michuano ya Kombe la Kagame kumalizika huku wadau wengine wa michezo nchini humo wakichangia Sh. milioni 2.1 za Kenya ambazo ni sawa na Sh. milioni 40.1 za Tanzania. "Tumepokea msaada kutoka serikalini kupitia kwa Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni, wametulipia tiketi za kurejea nyumbani baada ya ushiriki wetu kwenye mashindano hayo ya ukanda wa bara letu na tunawashukuru sana.
Sasa tuko tayari kusafiri kwenda Tanzania," Katibu Mkuu Msaidizi wa Gor Mahia, Ronald Ngala, alikaririwa na moja ya mitandao ya michezo ya Kenya jana.
HARAMBEE MILIONI 40
Mtandao huo pia ulieleza kuwa jumla ya Sh. milioni 2.1 za Kenya (Sh. milioni 40.1 za Tanzania) zilipatikana katika haramabee ya kuichangia Gor Mahia iliyofanyika kwenye makao makuu ya klabu hiyo juzi Julai 14.
Ilielezwa kuwa klabu hiyo iliendesha haramabee hiyo ili kupata fungu la kuhakikisha inakuwa vizuri kiuchumi wakati ikisaka taji la nne la Kombe la Kagame.
KUTUA LEO, KOCHA ATAMBA
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Frank Nuttal, ametamba kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Yanga.
Gor wanatarajia kuanza safari yao kuja Dar es Salaam leo saa 6:10 mchana. CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment