
Jimbo la Sikonge
Jimbo la Sikonge ni mamlaka yote ya Wilaya ya Sikonge yenye kata 20, vijiji 71 na vitongoji 281. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, jimbo hili lina wakazi 179,883, wanaume wakiwa 88,947, wanawake 90,936 na wastani wa watu ni 5.9 katika kila kaya.
Jimbo la Sikonge lilishiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 likijulikana kama “Tabora Kusini” na lilikuwa kati ya majimbo manne yaliyokuwa yanaunda wilaya ya Tabora wakati huo. Hapakuwa na sababu yoyote ya vyama vya upinzani kulikosa jimbo hili. Vilikuwa na kila kitu na wananchi waliviunga mkono vyama hivyo kuliko kitu chochote, lakini kulikuwa na tatizo moja, “mgawanyiko wa vyama vya upinzani” ambao ulikuwa mkubwa kupita kiasi.
Jumla ya vyama 11 vya upinzani vilikuwa hapa bila kujali kuwa Tadea na mgombea wake walionekana kuwa imara na walistahili kuungwa mkono, lakini sijui kama pia Tadea ilitaka ingwe mkono au la.
Mwanasiasa machachari na maarufu sana kutoka hapa mkoani Tabora, Christopher Kasanga Tumbo, akiwa amejipanga vilivyo, ndiye alitarajia kushinda uchaguzi huu kwa sababu mgombea wa CCM, Chifu Haroun Msabila Lugusha alionekana hana ubavu wa kumshinda Tumbo. Kilichotokea baada ya matokeo ya mwisho kilimgutusha kila mtu, CCM ilishinda kwa chini ya asilimia 50. Mgombea wake alipigiwa kura 9,382 sawa na asilimia 46.1 na Tumbo wa Tadea akapigiwa kura 7,098 sawa na asilimia 34.9, vyama vingine 10 (UPDP, NLD, NCCR, UDP, NRA, UMD, TPP, CUF, Pona) kwa ujumla vilipata asilimia 20 ya kura zote.
Ndio kusema kuwa ukijumlisha ushindi wa Tumbo wa Tadea na wa wagombea wengine 10 wa upinzani unapata jumla ya kura zilizopigwa kuwa asilimia 54. Hii ina maana kuwa hapa Sikonge mwaka 1995, upinzani uliishinda CCM kwa zaidi ya asilimia 8 lakini haukupata mbunge kwa sababu ya mgawanyiko na mtawanyiko wa kura.
Mwaka 2000 jimbo hili ndipo rasmi liliitwa Sikonge na kwenye uchaguzi wa mwaka huo CCM ikamleta kada wake kijana, Juma Said Nkumba, ambaye kitaaluma alikuwa mwalimu wa shule ya msingi (wakati huo). Kwa sababu ya vyama vya upinzani kuwa katika likizo isiyoeleweka jimboni hapa, Nkumba alirejesha heshima ya CCM na kupata ushindi mkubwa kupita ule wa mwenzie wa mwaka 1995.
Mwaka 2005, Juma Said Mkumba, alipitishwa kwa mara nyingine na CCM, kulinda nguvu ya chama hicho. Utitiri wa vyama 12 wa mwaka 1995 uliporomoka hadi kuwa vyama 8 mwaka huo 2005. Chama ambacho kilikuwa kimejimaarisha vilivyo mahali hapa ni CUF, lakini CCM ilionyesha kuwa imejipanga zaidi. Ndiyo maana matokeo ya mwisho yalimfanya Nkumba wa CCM apigiwe kura 24,804 sawa na asilimia 70.6 akifuatiwa kwa mbali na Abdallah Kanenda Seif wa CUF aliyepigiwa kura 8,666 sawa na asilimia 24.7, vyama vingine 6 vilivyobakia (Chausta, NCCR, SAU, TLP, UDP na UPDP) kwa ujumla vilichukua asilimia 5 ya kura zilizobaki.
Mwaka 2010 utitiri wa vyama ulishuka zaidi hapa Sikonge, kutoka 8 mwaka 2005 hadi 6 mwaka 2010. Kama kawaida, kwa mara ya tatu, CCM ilimweka Nkumba, lakini mara hii akionyesha kuchokwa zaidi, kada huyo pamoja na nguvu zote aliibuka na kura 12,025 sawa na asilimia 63.8. Mpinzani wake mkubwa likuwa ni Mtinya Edward David wa CUF aliyepigiwa kura 5,682 sawa na asilimia 30.15 ya kura zote, wagombea wa vyama vingine vinne (UDP, DP, UPDP na UMD) walipigiwa asilimia tatu ya kura zote.
Taarifa za wazi kutoka hapa Sikonge zinaonesha kuwa mbunge wa sasa ambaye anamaliza muda wake, Said Juma Nkumba ana nafasi ndogo sana ya kurejea tena katika uwakilishi wa CCM. Lakini lililo kubwa zaidi ni kukua kwa nguvu ya Chadema na CUF ambao wamo kwenye umoja wa Ukawa. Vyama hivi vya Ukawa vimeshinda kwa kiasi kizuri hapa Sikonge, kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 2014 japokuwa ushindi ule haukufikia wa CCM.
Jimbo hili ni gumu sana kwa upinzani lakini ni gumu pia kwa CCM hasa ikimsimamisha tena Said Mkumba, ambaye bila shaka wananchi wanaelekea kutosheka na uongozi wake wa miaka 15.
Tathmini ya jumla inaweza kuhitimishwa kwamba hapa Sikonge CCM itakuwa na nguvu ya kuutisha upinzani ikiwa itaweka mgombea mpya, lakini ikiwa atarudi Said Mkumba halafu upinzani ukapata mgombea mzuri na anayekubalika, nina uhakika kuwa hali itakuwa ngumu kwa CCM. Ndiyo maana jimbo hili naliwekea akiba ya maneno maana naona liko kwenye “mtanziko” wa wapi litakwenda kutegemeana na makosa ya Ukawa au CCM.
Jimbo la Urambo Magharibi
Jimbo la Urambo Magharibi kuanzia uchaguzi wa mwaka huu litaitwa jimbo la Kaliua. Jimbo hili ni sehemu yote ya mamlaka ya wilaya ya Kaliua na linaundwa na kata 18, vijiji 71 na vitongoji 289. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Kaliua ina wakazi 393,358, kati yao wanaume ni 196,369, wanawake ni 196,989 na kuna wastani wa watu 6.2 katika kila kaya.
Katika uchaguzi wa kwanza hapa Urambo Magharibi, CCM ilipata wakati mgumu sana mwaka 1995. Vyama vya upinzani vikiongozwa na NCCR almanusura vilichukue jimbo hili na kufanya ushindani kuwa juu sana. Hata hivyo Prof. Juma Athumani Kapuya wa CCM alitumia nguvu kubwa hadi kufanikiwa kushinda uchaguzi huo.
Lakini mwaka 2000 Prof. Kapuya hakuwa na mashaka juu ya ushindi wake kutokana na kuporomoka kwa NCCR ambayo ilikuwa imejijenga kiasi ambacho ilipitiliza wakati huo. Ushindi wake wa mwaka 2000 ulikuwa mkubwa kupita ule wa 1995 na hiyo iliipa CCM matumaini kuwa kazi ya ushindi wa baadaye itakuwa rahisi zaidi.
Mwaka 2005 uchaguzi mkuu ulipoitishwa, CUF ikiwa na kada wake, Kirungi Amir Kirungi ndicho chama pekee kilichoonesha kuwa kinaweza kuiondoa CCM hapa. Watu wa Urambo Magharibi wakati huo walikuwa wanamwamini Kirungi kupita kiasi na alikuwa na ushawishi mkubwa. Hali hiyo ndiyo ilisaidia kujenga matumaini makubwa kwa CUF ambapo Kirungi alipigiwa kura 11,890 sawa na asilimia 26.5 huku vyama vya Chadema, Chausta, Jahazi Asilia na TLP kwa pamoja vikapata asilimia 2.6 ya kura zote, huku mgombea wa CCM, Prof. Kapuya, akiwa mshindi wa jumla, kwa kura 31,301 sawa na asilimia 68.9 ya kura zote zilizopigwa na akawa mbunge rasmi kwa mara ya tatu.
Wingi wa vyama kuweka wagombea hapa Urambo Magharibi ulishuka sana mwaka 2010 ambapo kulikuwa na vyama vitatu tu, Jahazi, CCM na CUF lakini mvutano mkubwa ukionekana dhahiri kuwa ungeimarika kati ya “mafahali wawili wa Urambo Magharibi”, Kirungi wa CUF na Prof. Kapuya wa CCM.
Kuchokwa kwa Prof. Kapuya hapa Urambo Magharibi kulidhihirika kwa sababu jedwali lake la ushindi lilishuka sana. Mwaka huo wa 2010 Kapuya alipigiwa kura 18,691 sawa na asilimia 59.15 akivutwa shati vya kutosha na Kirungi wa CUF aliyekuwa na kura 11,733 sawa na asilimia 37.13. Baadhi ya wanachama wa CUF walioshiriki kwenye uchaguzi ule wanasema kulikuwa na rafu nyingi ambazo ziliondoa ushindi wa Kirungi.
Siasa za Urambo Magharibi au “jimbo jipya la Kaliua” mwaka huu 2015 zimeshabadilika sana. Kwanza, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Desemba 2014 yanaonesha kuwa vyama vya upinzani vimeongeza vijiji zaidi kutoka kwa CCM japokuwa bado CCM ina vijiji vingi. Lakini ongezeko la vijiji na vitongoji vipya limekuwa likihusisha mchanganyiko wa vyama vya Chadema, CUF, ACT na (sina uhakika sana na ADC).
Lakini pili, mgombea wa CCM ambaye bado ana nguvu na ameongoza jimbo hili tangu mwaka 1995 – 2015, Prof. Kapuya anakabiliwa na changamoto ya kuchokwa sana ndani ya CCM na hata nje ya CCM (Kwa wananchi) na ushindi wake kwenye kura za maoni ndani ya chama chake mwaka huu utategemeana zaidi na kundi lipi litashinda kura ya maoni ya Urais ya CCM. Kapuya ni mtu muhimu sana katika harakati za mgombea mmoja wa urais na ikiwa kundi hilo litaanguka naona na yeye ataangushwa kwenye kura za maoni.
Tatu, Kirungi (mgombea wa CUF katika chaguzi zilizopita) aliondoka CUF na kujiunga ADC katika vuguvugu la Hamad Rashid na baadaye ameondoka ADC na kujiunga ACT – Wazalendo na atagombea ubunge kupitia chama hicho kipya.
Nne, mbunge wa viti maalum wa CUF tangu mwaka 2005 – 2015 kutoka hapa Urambo Magharibi, ambaye pia ni Naibu Katibu wa CUF Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, ndiye anaonekana kuwa mgombea wa Ukawa anayeungwa mkono sana mahali hapa.
Kutokana na sababu hizo nne ambazo lazima zitaleta migawanyiko mikubwa, jimbo hili litakuwa kwenye wakati mgumu sana kutwaliwa na CCM au Ukawa, na najua halitaweza kabisa kutwaliwa na ACT ikiwakilishwa na Kirungi. Tunahitaji muda zaidi na kusubiri kujua CCM, Ukawa na ACT vitamsimamisha nani ili kutoa tathmini mpya ya siasa za hapa Kaliua (Urambo Magharibi). Naliweka jimbo hili “Njia Panda” hadi tutakapofanya uchambuzi mwingine mkubwa wa majimbo yote, hivi karibuni.
Jimbo la Urambo Mashariki
Jimbo la Urambo Mashariki kuanzia uchaguzi wa mwaka huu 2015 litajulikana kwa jina la “jimbo la Urambo” na ni sehemu yote ya mamlaka ya wilaya ya Urambo (baada ya kuondolewa sehemu iliyounda jimbo la Kaliua). Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 jimbo hili lina wakazi 192,781 ambapo wanaume ni 95,997, wanawake ni 96,784 na kuna wastani wa watu 5.9 katika kila kaya.
Je, wangapi wanamkumbuka Jacob Abraham Msina wa Urambo Mashariki (linaitwa jimbo la Urambo kuanzia uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015)? Huyu ndiye alikuwa shujaa aliyeushangaza ulimwengu wa Watanzania. Msina ni kada wa NCCR ambaye alibadilisha kabisa siasa za hapa Urambo Mashariki mwaka 1995 kwa kumwangusha mmoja wa majemedari wa siasa za Tanzania, Samuel Sitta. Sita huyuhuyu wa CCM tunayemjua, alikuwa kwenye wakati mgumu kwenye uchaguzi wa mwaka huo baada ya wananchi wa jimbo hili kumpa kura 9,497 huku NCCR chini ya Msina ikipewa kura za ushindi 10,788. Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, Samuel Sitta, akaangushwa.
Lakini CCM kwa mipango ya kurejesha majimbo ambayo huporwa na upinzani, hawajambo. Mwaka 2000 kwenye uchaguzi mkuu mwingine na baada ya kuzorota kwa NCCR, chama hicho kikongwe (CCM) kilimsimamisha kada wake mwingine wa kupigiwa mfano, Amani Karavina. Huyu aligeuza kile ambacho upinzani ulipanda hapa kati ya 1995 – 2000 kwani aliipa CCM ushindi wa kura 19,947 sawa na asilimia 70.47 na kulirejesha jimbo hili mikononi mwa chama hicho.
Baada ya Karavina kutuliza hali ya mambo hapa Urambo Mashariki, Sitta akarejeshwa tena na CCM mwaka 2005, akakutana na vyama vingine vitano lakini NCCR na CUF ndivyo vikimtisha zaidi. Hata hivyo Sitta alipata ushindi hapa wa kura 28,660 sawa na asilimia 72.3 akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa NCCR, Lumatiliza Yotamu Lubungila akiwa na kura 6,636 sawa na asilimia 16.7 huku vyama vilivyobakia (Jahazi, NLD, SAU na UDP) kwa pamoja vikiwa na asilimia 2 ya kura zote na baada kuchaguliwa huku, kiongozi huyu alipewa fursa kubwa ya kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, na azma hiyo ilitimia.
Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahaman Mtemelwa (Chadema) na Zombwe Lotto Edward (CUF). Sitta alipigiwa kura 19,947 sawa na asilimia 70.47, Mtemelwa akapigiwa kura 5,134 sawa na asilimia 18.14 na Zombwe wa CUF akapigiwa kura 1,009 sawa na asilimia 3.56.
Baada ya ushindi huu Rais Jakaya Kikwete alimtangaza kuwa Waziri wa Wizara ya Afrika Mashariki, wadhifa aliodumu nao hadi mwaka huu 2015 mwanzoni alipobadilishwa na kupelekwa wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Hadi nikamilishapo uchambuzi huu, Sitta amekwishawaaga wana Urambo (Urambo Mashariki) na hawezi tena kugombea ubunge hapa. Ndani ya CCM makada wengi wanalinyemelea sana jimbo hili huku kinara akiwa ni Magreth Sitta, mke wa Sitta ambaye ni mwana CCM mkongwe aliyewahi kushikilia nyadhifa nyingi serikalini.
Kwa upande wa upinzani naona Ukawa ikizidi kujiimarisha hapa bila kuwa na shaka lakini huenda kura zake zikapunguzwa na mgombea wa Chadema wa mwaka 2010, Mtemelwa, ambaye uwezo wake kisiasa siyo wa kubeza hata kidogo huku hivi sasa akiwa ndiye Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha ACT na ambaye nimeambiwa anajiandaa kugombea tena ubunge hapa.
Yaliyojiri kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa hapa Urambo Magharibi ni CCM kupoteza viti vingi zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2009 na jambo hilo lina ishara mbaya kwa chama hicho. Hata hivyo, bado natoa uwezekano mkubwa wa CCM kulitwaa jimbo hili ikiwa haitaathiriwa na siasa za makundi ya urais. UKAWA ina nafasi ya kipekee tu ikiwa itasimamisha mgombea bora huku CCM ikifanya makosa.
Hitimisho
Jumatano ya wiki ijayo, Julai 8, 2015, tutarudi Unguja Magharibi na kugusa majimbo ya Fuoni, Kiembesamaki, Magogoni na Mfenesini, kisha, Jumamosi ya Julai 11, 2015 tutaendelea na majimbo ya Mtoni, Mwanakwerekwe, Amani, Chumbuni, yote ya mkoa wa Unguja Magharibi.(Uchambuzi huu unafanywa na Julius Mtatiro “Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB (Student)”: +255787536759, kuelekeamajimboni@yahoo.com, https://www.facebook.com/julius.mtatiro, - ni maoni binafsi ya mwandishi).

0 comments:
Post a Comment