Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (Nec), Julius Malaba, amesema kuwa, vifaa vya kupigia kura vikiwemo vile vya kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki katika zoezi hilo, vinatarajia kuingia nchini mara baada ya zoezi la uteuzi wa tume kukamilika. Malaba alisema vifaa hivyo vimeshaagizwa na vitatumiwa na watu wenye ulemavu waliotimiza umri wa kupiga ambao wameshajiandikisha.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, alisema mara baada ya vifaa hivyo kuingia, ndipo watatoa elimu kwa wahusika.
“Kundi hili la walemavu tutalipa elimu mara baada ya vifaa hivi kuwasili, kwa sasa hatujaanza kuitoa,” alisema.
Wakati mkurugenzi huyo akitoa kauli hiyo, mwaka 2010 watu wenye ulemavu walishiriki kwenye zoezi la upigaji kura bila ya kuwa na elimu kitendo kilishosababisha vifaa maalum vilivyoletwa kwa ajili ya kupigia kura watu wenye ulemavu, kutotumika.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, mwaka huu takriban walemavu milioni nne wanakusudiwa kupiga kura.
Mwezi Mei, mwaka huu, Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu John Mkwawa, aliliambia gazeti hili kuwa, katikati ya Juni walitarajia kufungua zabuni za uagizaji wa vifaa hivyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Sauti ya Wanawake Tanzania (SWAUTA), Stella Jailos, aliliambia NIPASHE kuwa, mwaka 2010 watu wenye ulemavu walishiriki kwenye zoezi la upigaji kura bila kupata elimu.
“Ilikuwa kama vichekesho maana unafika kituoni huku wakijua una ulemavu wa kutoona huna elimu ya kifaa cha kupigia kura, unaambiwa chora chora, sasa hofu yetu ni kwamba si ajabu zile kura zilizotangazwa zimeharibika zilitokana na sisi maana unachora hujui umechora kwenye sura ya mtu au jina, haya ndiyo yaliyotukuta,” alisema. CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment