Mgombea ubunge jimbo la Morogoro mjini kupitia chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema) Marcossy Albanie akiomba kura kwa wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ubunge na udiwani uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Kiwanja cha Ndege mkoani Morogoro, Picha na Juma Mtanda.
Na Juma Mtanda, Morogoro.
Umoja wa vyama vya kisiasa vinavyounda UKAWA umezindua kampeni ya ubunge na udiwani huku wakieleza Manispaa ya Morogoro kukosa wawakilisha katika ngazi hizo na kusababisha wananchi kuendelea kukumbwa na kero zinazoweza kutafutiwa ufumbuzi mkoani hapa.
Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo uwanja wa shule ya msingi Kiwanja cha Ndege mjini hapa, viongozi wa Ukawa walisema kuwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro wanakumbana na kero nyingi ikiwemo ya uhaba wa maji, ukosefu wa ajira kwa vijana na huduma duni za afya katika hospitali za serikali na miundombinu mibovu ya barabara.
Mgombea ubunge jimbo la Morogoro mjini kupitia chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema) Marcossy Albanie alisema kuwa dhamira yake kubwa kutumikia wananchi wa jimbo la Morogoro mjini kwa kusimamia zoezi la urejeshwaji wa viwanda 14 ndania ya miezi sita ili vifanye kazi na kutafutia ufumbuzi wa kero mbalimbali.
Albanie alisema kuwa viwanda vilivyokufa na vile vilivyobinafsisha na kushindwa kufanya kazi vinaweza kurejea na kuendelea kufanya kazi na wakazi wa Manispaa ya Morogoro na watanzania kiujumla ili kupunguza wimbi la watu kukosa ajira.
“Tunaomba watanzania wenzetu mtuingize kwenye madarakani Oktoba 25 kwa kutupigia kura za kutosha katika nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani ili timu ikamilike kuweza kuwatumikia ili kuweza kufanya kazi kama timu ili kufanikisha adhima yetu.”alisema Albanie.
Albanie alisema kuwa endapo wataingia madarakani, ndani ya miezi sita ya mwanzo Ukawa watahakikisha wanaibadilisha Manispaa ya Morogoro kwa maendeleo hasa kurejesha viwanda vyote ambavyo havifanyi kazi kwa sasa ili viweze kufanya kazi.
Mgombea huyo alieleza kuwa ajira kubwa iliyobakia kwa vijana ni kuendesha bodaboda lakini Ukawa wanaenda na kauri mbiu ya safari ya uhakika.
“Lengo letu Ukawa ndani ya Manispaa ya Morogoro na Tanzania kwa ujumla kuimarisha huduma za kijamii kwa kuvuta utaratibu wa akinamama kufuata maji mita 500, kujenga na kuboresha barabara zitazopitika muda wote na kusimamia huduma za afya kikamilifu”.alisema Mgombea huyo.
Aliongeza kuwa katika sekta ya afya endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Morogoro atasimamia kidete utaratibu wa upatikanaji wa matibabu ya bure kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, wazee na wanawake wajawazito.
“Ni jambo la kushangaza kuona vitambaa vya kupokelea watoto wachanga baada ya mama mjamzito anajifungua vinakosekana katika hospitali za serikali vikiwemo viwembe na nitahakikisha huduma hizo zinarejea katika kiwango cha ubora”.alisema Albanie.
Naye Katibu Mwenezi wa Chadema Manispaa ya Morogoro, Shabaan Dimoso alieleza umati wa watu waliohudhuria mkutano huo kuwa chama cha Demokrasi na Maendeleo hakikosei katika uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi.
“Tulianza kuwachagua viongozi mbalimbali katika nafasi za ubunge na udiwani katika uongozi wa umma na wameweza kufanya vizuri.”alisema Dimoso.
Aliwataja mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, John Mnyika, Halima Mdee na wengi wengi na wameweza kufanya vizuri katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania na baadhi za halmashauri hapa nchini kwa kusimamia vyema serikali ikiwemo kupinga mambo ya kiufisadi.
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Manispaa ya Morogoro, James Mkude alitoa pongeza kwa jeshi la polisi kwa kuimarisha ulinzi na kulitaka jeshi kuendeleza ukarimu huo katika kampeni na uchaguzi mkuu.
“Chadema hakitajihusisha na kampeni za matusi na tuwatake wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya udiwani na ubunge kusimamia vizuri uchaguzi huu kwa kutenda haki hasa maafisa watendaji na mkurugenzi.
0 comments:
Post a Comment