BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS KIKWETE: DK MAGUFULI NDIYE ATAKUWA MSHINDI UCHAGUZI MKUU OKTOBA 25.


Maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam wakiwa kwenye mkutano wa kampeni za CCM, viwanja vya Jangwani jana. (Na Fadhili Akida).

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amesema tayari mgombea urais wa chama hicho, Dk John Magufuli ameshashinda uchaguzi.

Amesema hatua hiyo inatokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kwa mgombea huyo kuzunguka nchi nzima na kuwahakikishia wananchi, bila kupepesa macho, kwamba atapambana na rushwa na ufisadi huku wagombea wengine wakisita kuzungumzia rushwa.

Katika hatua nyingine, Dk Magufuli ametaja mambo manne atakayoanza nayo kuwa ni umasikini, tatizo la ajira, mapambano dhidi ya rushwa na amani.

Pia, aliwapa pole Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Rais Kikwete kwamba katika utawala wao, bila kujua waliwaweka madarakani mafisadi waliochelewesha maendeleo ya serikali zao.

Rais Kikwete na Magufuli waliyasema hayo katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mkuu kwa Jiji hilo. Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya watu na viongozi mbalimbali wa CCM, Serikali na viongozi kutoka nje ya nchi.

Akimnadi Dk Magufuli, Rais Kikwete alisema kutokana na kampeni alizozifanya nchi nzima kwa gari, ni wazi kwamba mgombea huyo wa CCM ameshashinda uchaguzi huo. Alisema wagombea wengine pamoja na kutumia helikopta, lakini walishindwa kuzungumza majukwaani.

Alisema pamoja na kuelezea mambo mbalimbali atakayowafanyia wananchi kwa kila kundi, amekuwa mgombea pekee ambaye bila kupepesa macho amezungumza waziwazi azma yake ya kupambana na rushwa na kuwakabili mafisadi ili kuwatokomeza.

Alisema tangu kuanza kwa kampeni zake Dk Magufuli ametembea kilometa 46,000 nchi nzima, umbali aliosema umemwezesha kukutana na wananchi wengi vijijini. Alisema wakati yeye alipofanya kampeni mwaka 2005, alitembea kilometa 32,000 kwa gari na kuwa hoi katika siku za mwisho za kampeni.

Alisema pamoja na kuzungumzia rushwa, Dk Magufuli amezungumzia masuala mengine mengi kama kupambana na umasikini, ajira, amani, mikopo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji, kushusha kodi kwa wafanyakazi, kufuta ada kuanzia darasa la kwanza hadi kidato na nne, lakini pia kuanzisha viwanda.

Akirejea taratibu zilizomwezesha Dk Magufuli kuteuliwa na chama hicho kugombea urais, Rais Kikwete alisema hakuna jipya lililofanyika katika kumpata mgombea huyo, badala yake ni taratibu zile zile zilizotumika mwaka 1995 kumpata Rais mstaafu Mkapa na mwaka 2005 alipoteuliwa yeye.

“Ni taratibu zilezile ndizo zilizotumika, hakuna utaratibu mpya. Katiba ya CCM inasema Kamati Kuu itapitisha majina ya watu wasiozidi watano na kuyapeleka kwenye Halmashauri Kuu, inaweza kuwa chini ya hapo lakini wasiozidi watano,” alisema Rais Kikwete akimjibu Kingunge Ngombale- Mwiru anayedai kupitia majukwaa ya Ukawa kuwa CCM ilikiuka taratibu.

Akizungumzia mikopo kwa wanafunzi, Rais Kikwete alisema ni faraja kuona kuwa Dk Magufuli amepania kukabiliana na usumbufu wanaokumbana nao.

Alisema wakati alipoingia madarakani mwaka 2005, alikuta Sh bilioni 40 tu zikitolewa kwa wanafunzi, huku wanafunzi 16,000 tu wakinufaika, na sasa Sh bilioni 350 zinatumika na kuwanufaisha wanafunzi 98,000.

Dk Magufuli
Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk Magufuli alisema akipita mikoani aligundua wananchi kupendezwa na sera za kupunguza umasikini, tatizo la ajira, kuendeleza mapambano ya rushwa na ufisadi na suala la amani na kuahidi kutumia nguvu zote kuboresha maeneo hayo endapo atachaguliwa.

Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, aliahidi kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu ya barabara za kawaida na barabara za juu na pia kujenga upya maeneo yaliyojengwa kiholela katika Kata 14 za Jiji hilo.

Alisema barabara za Mwenge-Morocco, Barabara ya Kawawa, Barabara ya Nyerere na Barabara ya Kilwa, zitapanuliwa upya ili kuondoa msongamano wa magari. Alirejea tena kueleza mipango ya kujeng barabara za juu katika eneo la Tazara na Ubungo na pia kujenga barabara ya juu ya Selander.

Aliahidi kutumia nguvu zake zote katika kumaliza tatizo la maji, huku wakati wote akisifu jitihada zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne katika kupambana na changamoto hizo.

Katika hatua isiyotarajiwa, Dk Magufuli alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa marais Mkapa na Kikwete kwamba katika uongozi wao, waliwapa madarakani makubwa baadhi ya wanaCCM, wakidhani watawasaidia bila kujua kuwa watu hao ni mafisadi na hivyo wamechangia kuchelewesha mipango yao ya maendeleo na kuapa yeye kutofanya kosa hilo.

Kampeni Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimefunga kampeni zake kwa kishindo kisiwani Zanzibar na kuwahakikishia wanachama wake kuwa chama hicho kikongwe, kitashinda kwa kishindo Bara na Visiwani katika uchaguzi utakaofanyika kesho.

Mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Kibanda Maiti, ambao ulihutubiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan na Mgombea Urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ulihudhuriwa na maelfu ya wapenzi na wanachama wa chama hicho.

Akihutubia mkutano huo, Samia aliwashukuru Wazanzibari hasa wa CCM kufanya kampeni kwa amani na utulivu. Aliwaeleza wafuasi wa chama hicho kuwa amefanya mikutano 343 Tanzania nzima na sasa yuko tayari kuwatumikia Watanzania.

Alisema alichobaini ni kwamba vijana wengi wako CCM na ndio maana wanawachukulia kama raslimali zinazohitaji kuendelezwa ili wajiajiri na wajikimu na maisha yao.

Dk Shein
Kwa upande wake, Dk Shein alisema walifanya mikutano mikubwa 27 na akaongeza kuwa mahudhurio makubwa katika mikutano hiyo na kusikiliza jinsi CCM ilivyotekeleza ilani yake ya mwaka 2010 hadi 2015, anaamini chama hicho kitashinda.

Alisema Ilani ya mwaka huu imetaja sekta 23, ambazo watazitekeleza amekuwa anazielezea kwenye mikutano watazitekeza kikamilifu. Alisisitiza kuboresha elimu kwa kujenga Chuo Kikuu kipya huko Dole, maji kufikia asilimia 85 ya wananchi na huduma zingine.

“Endeleeni kutuamini tutatekeleza, nitatekeleza kama nilivyofanya miaka mitano iliyopita,” alisema Dk Shein ambaye pia aliahidi kulinda Muungano wa Serikali Mbili na Mapinduzi matukufu.

Aliahidi kusimamia amani, utulivu na mshikamano na akasema akichaguliwa atasimamia hilo kwani Zanzibar inaheshimiwa kwa umoja na ndio maana watalii wengi wanakuja Zanzibar na viongozi wakubwa duniani, wanakuja visiwani hapa kupumzika.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: