
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (kushoto) akishiriki usafi wa mazingira na wananchi katika eneo la Soko la Mboga Mombasa Mjini Zanzibar ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Picha na Ikulu).
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusherehekea maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi yanayoanza leo.
Dk Shein alisema wananchi wana kila sababu za kushiriki maadhimisho hayo kwa kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ndiyo yaliyoleta Uhuru kwa wananchi wa Unguja na Pemba kutoka kwa wakoloni.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kushiriki kufanya usafi katika soko la matunda la Mombasa mjini Unguja jana, Dk Shein alisema wananchi wanaelewa vyema historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba wanajua wajibu wao katika kuyalinda na kuyadumisha.
Dk Shein alisisitiza kuwa kila mtu ana haki na wajibu wa kuenzi na kuendeleza Mapinduzi kwa kuwa hakuna mwananchi asiethamini uhuru wake. Alisema mapinduzi ya mwaka 1964 yameleta maendeleo kwa kila mwananchi.
Alisema wapo wanaoyakumbuka kwa furaha na wengine wamenuna, lakini Mapinduzi yalikuwa ni lazima ili kuwaweka Wazanzibari huru.
Aliwataka wananchi kushiriki katika ratiba mbalimbali za maadhimisho hayo ikiwemo mashindano ya mpira wa miguu ya Kombe la Mapinduzi yanayoanza leo katika uwanja wa Amaan Zanzibar.
Wakati huo huo, Rais Shein alitaka mamlaka zinazohusika na afya na usafi wa mazingira kuhakikisha kuwa suala la usafi linakuwa endelevu ili kulinda afya na kuepusha magonjwa ya kuambukiza. Alisema usafi ni lazima uimarishwe katika maeneo yote yakiwemo makazi, sehemu za kazi na maeneo ya biashara yakiwemo masoko.
“Si kitu kizuri hata kidogo kuwa usafi unafanyika kwa nadra kama hivi wakati wa maadhimisho wakati moja ya kanuni za afya ni usafi wa binadamu mwenyewe na mazingira yake,” alisisitiza Dk Shein.
Dk Shein alitoa mfano wa kitendo cha soko la samaki la Malindi kurejea katika hali ya uchafu wakati jitihada kubwa zilichukuliwa kulifanyia usafi wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru wa Tanganyika, Desemba 9 mwaka jana ambapo pia alishiriki.
Aliwataka wataalamu wa afya pamoja na watumishi wa Manispaa wanaokusanya kodi na ushuru katika sehemu za biashara kama masoko kuhakikisha kuwa suala la usafi wanalipa kipaumbele katika mipango yao kwa kuwa bila ya usafi katika maeneo ya biashara ni rahisi kusababisha maradhi ya kuambukiza kama kipindupindu.
“Watu wa sheria wasimamie sheria, wataalamu wa afya wawaelimishe wananchi na wananchi ni lazima wafuate maelekezo ya wataalamu hao kwa faida yetu sote kujilinda na maradhi,” alisema.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment