FAIDA LUKUKI ZA POLISI JAMII AMA ULINZI SHIRIKISHI
Polisi Jamii au Ulinzi Shirikishi(community policing) ni mkakati wa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi. Lengo kuu la mkakati huo ni kuweka mazingira ya ushirikiano wa dhati baina ya wananchi na Polisi.
Kwa misingi hiyo mpango wa Polisi Jamii ni utaratibu mpya wa utendaji kazi wa polisi. Ni mpango kamambe ambao unalenga kuleta mabadiliko ya namna Idara ya Polisi inavyohusiana na jamii, falsafa mpya inayopanua malengo ya Polisi kutoka kwenye mtizamo wa kadri (limited) unaolega kwenye tukio moja au pengine.
Ama aina moja tu ya uhalifu kwenda kwenye mtizamo mpana unaohamasisha Jeshi la Polisi kulenga kwenye ufumbuzi wa matatizo ya jamii kwa ujumla wake: ikiwemo uhalifu wenyewe, woga wa kudhurika na uhalifu (fear of victimization), vurugu na hali ya wasi wasi ndani ya jamii na kuzorota au kutojali kwa jamii.
CHIMBUKO LA DHANA NA IMANI (FALSAFA) YA POLISI JAMII.
Mpango wa polisi jamii ni mtizamo madhubuti wa jinsi ya kupanga mikakati ya utendaji ya polisi; msingi wake mkuu ukiwa ni imani kuwa askari Polisi wakifanya kazi pamoja na wananchi – raia wa kawaida, wanaweza kusaidiana kutatua matatizo yanayokabili jamii yanayohusu uhalifu, woga kuhusu uhalifu (fear of victimization), vurugu ndani ya jamii, pamoja na jamii kuzorota (social decay) kutokana na kutojali. Chini ya mpango huu polisi wanatakiwa kuweka misingi ya ushirikiano wa karibu kabisa baina yao na raia wema katika jamii.
Ushirikiano wa aina hiyo utawawezesha raia wema kuwa na kauli kubwa zaidi katika uwekaji wa mipango na malengo ya polisi na kwa njia hiyo kuwahusisha kikamilifu katika jitihada za kuboresha hali na thamani ya maisha (quality of life) katika sehemu wanazoishi.
Majeshi ya Polisi mengi duniani yameanza kutizama upya sera zake za kiutendaji kwa lengo la kuweka taratibu madhubuti zenye kuzingatia misingi ya Polisi Jamii. Wimbi la mabadiliko haya linatokana na kutambua uzito wa tatizo la uhalifu katika karne hii ya 21. Uhalifu na wahalifu katika ulimwengu wa sasa vimejitokeza kuwa ni changamoto la aina yake.
Uhalifu unafanyika kwa njia za kitaalam zaidi (sophisticated) na hasa kwa kutumia mitandao ya kisasa inayotokana na maendeleo katika nyanja mbali mbali za sayansi na teknolojia. Njia za jadi za kukabiliana na uhalifu huu zinaonekana kutokuwa jibu la kutosha.
Mathalan, doria ya polisi mitaani ni moja ya njia za jadi za kukabiliana na uhalifu. Lengo lake ni kuzuia uhalifu; kuwahi kwenye matukio ya uhalifu ili kuwahoji mashahidi, kukamata watuhumiwa, kupeleleza na kukusanya ushahidi. Uchambuzi hata hivyo umeonyesha kuwa ingawaje hatua zote hizo ni muhimu haziwezi kwa peke yake kuwa ni ufumbuzi wa tatizo la uhalifu.
MISINGI YA POLISI JAMII/ULINZI SHIRIKISHI:
Msingi mkuu wa mpango wa Polisi Jamii ni imani (falsafa) kuwa uboreshaji wa maisha ya jamii kwa kuiondolea jamii kero ya uhalifu; unaweza kupatikana kutokana na jamii kufanya kazi pamoja na Jeshi la Polisi. Polisi wanakuwa ni washauri, wawezeshaji, wasimamizi na waimarishaji wa jitihada za jamii za kuondokana na kero za uhalifu.
KWA NINI MPANGO WA POLISI JAMII NI MUHIMU?
Uanzishaji wa Polisi Jamii ni changamoto lisiloepukika kwa sasa. Mpango huu umejitokeza kuwa na umuhimu wa aina yake kwa sababu katika mazingira ya nyakati zetu hizi; ya maendeleo ya sayansi na teknologia wahalifu hutumia mbinu za kisasa kama vile teknologia ya mawasiliano, usafiri n.k. kufanikisha malengo yao maovu.
Aidha wahalifu nao ni watu wenye akili. Huunda asasi za aina mbalimbali zilizo rasmi na zisizo rasmi, pamoja na mitandao kemkem ya kufanikisha malengo yao ya kiuhalifu. Haya yametokea kwa sababu kuu tatu tutakazochambua hivi punde.
Kwanza wahalifu hutumia sheria kufanikisha maelengo yao na kwa hiyo sheria peke yake haiwezi kuleta ufumbuzi wa matatizo ya uhalifu. Kutokana na mapato ya vitendo vyao viovu wahalifu huweza kuwakodi washauri wa kisheria waliobobea ambao huwatumia kufanikisha malengo yao.
Mathalan, si aghalabu wezi wa magari kuhalalisha miliki au uuzaji wa magari waliyoiba kwa kutumia wanasheria. Vile vile wahalifu wanaelewa sheria za ushahidi hususan; wajibu wa mshtaki kuthibitisha shtaka bila kuacha mwanya wo wote wa mashaka (burden of proof).
Pamoja hayo wahalifu huunda asasi zilizo halali kisheria kama vile makampuni, shughuli za biashara (business enterprises) n.k kwa ajili ya kufanikisha malengo yao ya kiuhalifu; mfano mzuri ni usafishaji wa fedha haramu kwa kuziingiza katika shughuli halali za kibiashara (money laundering).
Pili wahalifu wanafahamu taratibu za kiserikali. Wanafahamu sheria zinavyotungwa na jinsi zinavyopaswa kutekelezwa. Wanafahamu mbinu za kuhamasisha maoni na mawazo yanayowaunga mkono. Wahalifu waliobobea huweza hata kupanga taratibu za kuwahamasisha wapiga kura ndani ya jamii na kwa hivyo kufanikisha malengo yao.
Sababu ya tatu ni kuwa uhalifu hutoa ajira kwa wale walioukumbatia. Hali hii hujenga mtandao wa utegemezi juu ya mapato yanayotokana na uhalifu. Kwa njia hiyo wahalifu huweka mazingira ambapo kuna kundi fulani miongoni mwa jamii litakalowaunga mkono.
Pengine mambo hayo matatu miongoni mwa mengine hufanya changamoto la kuanzisha mpango wa polisi jamii lisiweze kuepukika.
Kama wahalifu wanafahamu sheria na taratibu za serikali na huzitumia kwa manufaa yao, polisi wakitegemea sheria peke yake mafanikio yao ya kupata ufumbuzi wa matatizo ya uhalifu yatakuwa ni ya kadri kwa vile wanatumia chombo hicho hicho wanachotumia wahalifu.
FAIDA ZA MFUMO WA POLISI JAMII
Mfumo wa polisi jamii una faida kuu zifuatazo ambazo haziwezi kupatikana kikamilifu chini ya mfumo uliozoeleka wa utendaji wa kazi za polisi.
Faida hizi ni: polisi kufanya kazi na wananchi kwa pamoja, kujenga mazingira ya kuaminiana, kuweka mazingira ya ubia (partnership) baina ya polisi na jamii, kuhamasisha ubunifu na kupata ufumbuzi stahimilivu (sustainable) wa kero za wananchi. Tutachambua kwa ufupi faida hizi.
UBIA (PARTNERSHIP) BAINA YA POLISI NA JAMII
Tofauti moja kubwa iliyiopo kati ya utaratibu uliozoeleka na mfumo wa polisi jamii inahusu mipango ya utendaji ya polisi.
Wakati mipango ya polisi kwa utaratibu uliozoeleka huzingatia malengo na matakwa ya Idara ya Polisi peke yake, chini ya mfumo wa polisi jamii mipango ya utendaji hutia maanani matakwa ya jamii kwa vile huandaliwa na wananchi wa sehemu hiyo wakishirikiana na Askari Polisi Kata.
Mantiki ya utaratibu huu inaweza kutoeleweka vizuri katika utaratibu uliozoeleka (traditional policing). Inaweza ikatokea hisia kuwa jamii inaweza kukwamisha malengo na mipango ya polisi. Hii si kweli kamwe.
Kinachotokea, kinadharia ni kuwa askari polisi kata huwaelewesha wananchi katika sehemu au mtaa wake kuwa iwapo mtatoa ushirikiano na taarifa; matokeo yake mtakuwa na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kupanga malengo ya polisi katika mtaa wenu.
Askari Polisi Kata mzuri hufahamu na kukiri kuwa wananchi si kikwazo kwa malengo ya polisi. Badala yake ni hazina muhimu ambayo inaweza kuchotwa kwa njia ya jamii kushiriki kikamilifu katika mipango ya polisi kwa lengo ka kufanya jamii hiyo iishi katika mazingira ya utulivu. Mazingira ambapo uhalifu umedhibitiwa kikamilifu.
Utaratibu na dhana nzima ya wananchi kushiriki katika kuandaa mipango inatakiwa ifikishwe kwa wananchi ili waweze kutambua kuwa mchango wao unathaminiwa. Changamoto kubwa iliyopo kwa askari kata ni pamoja na kushirikisha wananchi moja kwa moja katika ufumbuzi wa matatizo yanayokabili mtaa wao au sehemu yao wanayoishi.
Mpango wa polisi jamii siyo tu huwafanya wananchi kuwa ni macho na masikio ya polisi kwa saa 24 kila siku bali pia huhamasihsa wananchi kushiriki katika ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza ndani ya jamii yao.
Pale ambapo mfumo wa polisi jamii umepokelewa kwa mafanikio na wananchi; baadhi yao wanaweza kujitolea katika mambo mbalimbali yaliyoko ndani ya mpango wao kama vile wazazi kusimamia mipango ya kuendesha michezo ya vijana wa mtaa huo; wafanya biashara kujitolea vifaa vya michezo n.k.
Lengo likiwa ni kuwashughulisha vijana waondokane na kukaa bure na hivyo kujiingiza katika matendo yasiyofaa kama vile: kuvuta bangi, unywaji pombe n.k., mambo ambayo baadye huweza kuzaa uhalifu.
Neno ‘community policing’ limekuwa na tafsiri ya ‘Polisi Jamii’ kwa muda. Kwa sasa kuna mwelekeo wa tafsiri mpya ambayo ni ‘Ulinzi Shirikishi’. Pengine tafsiri hii mpya ni nzuri zaidi. Maana haiathiriki kwa tafsiri zote mbili.
0 comments:
Post a Comment