
Na Juma Mtanda, Morogoro.
Watu zaidi ya 1500 kutoka katika kaya 250 kitongoji cha Mbwamaji wamekumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha hasara mbalimbali zikiwemo nyumba kubomoka na uharibifu wa mali kata ya Magomeni wilaya ya Kilosa jana mkoa wa Morogoro.
Mafuriko hayo licha ya kuharibu mali za wakazi hao pia zimeharibu miundombinu ya barabara ya Mikumi-Kilosa na mazao ya aina mbalimbali katika mashamba yanayokadiliwa kufikia heka 400.
Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Mbwamaji kata ya Magomeni, Abdalla Songoro (51) alimweleza mbunge wa viti maalumu kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Morogoro Devotha Minja kuwa wananchi zaidi ya 1500 wamekumbwa na mafuriko na kusababisha kaya 250 kukosa makazi sambamba na vyakula.
Songoro alieleza kuwa mafuriko hsyo yalianza kuingia katika makazi ya watu majira ya saa sita usiku jana (juzi) na leo (jana) saa 5 asubuhi baada ya maji kupasua mto mkondoa eneo la shamba la magereza na kusababisha athari hiyo.
“waathirika wote katika mafuriko haya wengi wao wanaishi katika majengo ya mahakama ya mwanzo, shule ya msingi Magomeni na jengo la boma la ofisi ya afisa mtendaji kata na mpaka sasa hivi bado hatujapata kesi ya kifo mpaka sasa.”alisema Songoro.
Kwa upande wa mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema mkoa wa Morogoro, Devotha Minja aliyewatembelea wahanga hao baada ya kukagua eneo lililokumbwa na mafuriko hayo aliwaeleza wananchi kuwa hali inatia majonzi na ipo haja kwa serikali kutoa huduma za dharura za kibinadamu.
“Nawapeni pole kwa tukio lililotokea lakini kutokana na hali halisi nawaombeni msirudi tena kwa wale wenye nyumba ambazo hazijabomoka kwani mvua inaweza kunyesha tena na kuweza kusababisha maafa katika upande wa vifo.”alisema Devotha.
Devotha alieleza kuwa taarifa aliyopewa na mwenyekiti wa kitongoji na diwani wa kata ya Magomeni, Abdallah Uweli kuwa kuna idadi ya kaya 250 zimeathirika zikiwa na zaidi ya watu 1500 kukosa makazi na kulazimika kujisitiri katika majengo ya serikali.
“Serikali unaitupia lawama kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kujenga tuta katika mto mkondoa ili kuzuia maji katika pande mbili na badala yake kujengwa tuta upande mmoja na kuwa chanzo cha mafuriko hayo".alisema Minja.
Mmoja wa wahanga hao, Jema Mduwile (25) alisema kuwa maji hayo yalivamia katika makazi yao wakati tayari wamelala na kazi ya kuwaokoa watoto ilikuwa ngumu kutokana na maji kuwa na kasi.
“Nilifanikiwa kuwaokoa watoto wangu wote wane kwa kuwabeba kutoka ndani ya nyumba hadi sehemu salama katika mazingira magumu lakini namshukuru mungu kwani maji baada ya kuingia ndani yaliingia kwa kasi na kufikia usawa wa madirisha”.alisema Mduwile.
Mduwile alisema kuwa baada ya kufanikiwa kuwaokoa watoto usiku ule mali kama gunia moja la chakula la mpunga, vyombo vya ndani na nguo pamoja na mali nyingine vimesombwa na maji.
Naye Julius Ndababisa (26) alisema kuwa yeye katika mafuriko hayo amepoteza mali nyingi ikimo nyumba kubomoka, magodoro, na uharibifu wa vitanda na mali nyingine.
Baada ya kutokea kwa mafuriko hayo kuna athari zinaweza kujitokea endapo juhudi za haraka hazitaweza kuchukuliwa hasa magonjwa ya mpuko kutokana na visima vya maji vinavyotumika na wakazi hao.
0 comments:
Post a Comment