BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAMA SI WAZEE, CCM INGEFIA MIKONONI MWA RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE.

Rais mstaafu awamu ya nne, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Vwawa. Mbunge wa zamani wa Mbozi Magharibi (CCM), Eliakim Simpasa amesema bila ushauri wa wazee, CCM ingekufa mikononi mwa mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete.

Simpasa alisema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi yaliyofanyika nyumbani kwake Vwawa, Mbeya wiki iliyopita.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Bunge na ambaye aliwahi kuongoza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, alisema ushauri wa wazee hao wa CCM akiwamo John Malecela, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pancras Ndejembi (aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Dodoma, Kingunge Ngombare-Mwiru.

Makada hao ndiyo walioshauri kurejeshwa kwa Phillip Mangula kwenye uongozi wa CCM akishika nafasi ya makamu mwenyekiti, huku Abdulrahman Kinana akipewa nafasi ya katibu mkuu baada ya chama kuwa katika hali mbaya.

Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mbozi Magharibi,
Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mbozi Magharibi, Eliakim Simpasa akizungumza wakati wa mahojiano maalumu, nyumbani kwake Vwawa, Mbeya. Picha na Reginald Miruko.
 
“Ninachokumbuka kwa ndugu yangu Kikwete, kama Serikali walijitahidi kuweka mtandao wa barabara, lakini enzi hizo, kama chama tulidorora sana. Chama kilidorora sana. Chama kilikosa mwelekeo. Nusura kife,” alisema Simpasa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Momba.

“Yaani sisi wengine ambao ni wa zamani tulifika mahali mpaka unatoa machozi, kwamba ni CCM ambayo naifahamu hii, ambayo anybody can do anything (yeyote anaweza kufanya chochote!) halafu basi. Ukafika wakati akaweka katibu wa ajabu, muweke huyu anacheza ngoma yake, mlete huyu akacheza ngoma yake. Kwa kweli chama nusura kife.

“Na unajua kwa nini tumeshinda? Kwa sababu yeye Ndugu Kikwete naona alisikia, lakini chama, wazee, tuwaheshimu wazee, wote hawa kina Malecela, Ndejembi, wazee wa kaskazini, kuna wazee wengi sana wa chama. Wengi sana nadhani mnawafahamu, hata Kingunge waliona chama kinakufa. Walimshauri, rudisha watu wakusaidie.

“Kwa hiyo tumeshinda, sifa zote zimwendee Kinana. Kinana amezunguka nchi nzima mpaka tukaanza kumwonea huruma afya yake itakuwaje. Sidhani kama ana hamu tena ya kushughulika na chama. Kinana amefanya kazi jamani na ametukomboa na Mangula wake.”

Mangula alikuwa katibu mkuu wa CCM kuanzia mwaka 1997 hadi 2007. Baada ya kushinda urais mwaka 2005 na kuwa mwenyekiti wa chama, Kikwete alimchukua Yusuf Makamba kushika nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa CCM, huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikienda kwa Pius Msekwa.

Lakini baada ya kushinda tena urais mwaka 2010, Kikwete alimrejesha Mangula kwenye chama mwaka 2012 akipewa nafasi ya makamu mwenyekiti, huku Makamba akimpisha Kinana katika nafasi ya katibu mkuu, kazi ambayo ameifanya kwa kuzunguka nchi nzima akiwapachika jina la “mizigo” mawaziri waliokuwa wakilalamikiwa na wananchi kutokana na kutowajibika ipasavyo.

“Kwa hiyo Kinana ametembea nchi nzima, amerudisha wananchi,” alisema Simpasa.

“Lakini hata ushindi mwingine tumekuja kuupata kwa sababu (Rais John) Magufuli mwenyewe amejua wananchi wanataka nini, wameshakerwa wapi. Kwa sababu hata ufisadi ulioingia pale haukuwa wa Serikali tena, ni ufisadi kwenye chama.” Alisema zamani ilikuwa mtu akiwa fisadi kwenye Serikali, kiongozi wa chama anamwondoa, lakini sasa mtu anashindwa kukusanya kodi hakuna kinachofanyika.

“Sasa watu wamekuwa fisadi. Mtu anakusanya siku tano bilioni kadhaa, wakati nyie mmekaa miaka yote mnacheka tu. Kwa hiyo yule (Magufuli) ametusaidia na kuna Mungu amemjalia kwa sababu ameingia pale with a serious agenda,” alisema.

Alifafanua kuwa hata ajenda hiyo maalumu ameitumia vizuri kuwaambia wananchi kwamba anataka kutumbua majipu, kuunda mahakama ya rushwa na kushughulika na mafisadi.

Makundi ndani ya chama
“Vitu hivi vilikuwa vinawakera watu, maana chama kilikuwa kimekufa. Na hata hivyo chama kile kina makundi mengine yaliyokuzwa sana baada ya ule uchaguzi wa 2005 lilipoanza kundi la wanamtandao na CCM Original. Kuna vitu ambavyo hata wewe hujui. Huu mtandao ulifika mahali nao ukagawanyika,” alisema.

Alisema kutokana na ahadi za vyeo, baada ya uchaguzi mtandao huo uligawanyika na kuendelea kugawanyika hadi kukawa na makundi saba.

“Huyu anakwambia nilitaka kuwa waziri wa mambo ya nje, hakupata, ananuna. Huyu anasema sikutaka kuwa naibu waziri, naye ananuna,” alisema.

“Nataka nikueleze, watu wamenyanyasika katika kipindi hicho. Yaani mtu alikuwa na sifa zake, alikuwa na heshima zake na staha zake, lakini ananyanyasika. Unajiuliza, mbona huyu anatoka kwenda chama kingine, anakwambia tumedharauliwa mno, tumenyanyasika mno.

“Inafika mahali mpaka kina Kingunge wanatoka, kwanza haiingii akilini kwamba mpaka Kingunge anasema anatoka kwenye chama hicho, wakati Kingunge ndiyo chama, ndiyo viongozi waanzislishi.”

Hata hivyo, Simpasa alisema Serikali ya Awamu ya Nne na Tatu zilijitahidi kuweka mtandao wa barabara, wakati ya awamu ya pili ilijikita kwenye kujenga mtandao wa elimu kwa mikakati kama MMEM na MMES.

“Kwa hivyo, awamu hii ina sifa ya kujenga mtandao wa barabara, imejitahidi sana. Lakini ina sifa kuwa iliachia mno mianya ya rushwa,” alisema.

“Ilikuwa kama vile watu walikuwa wanatoa fadhila, wanatoa shukurani kwamba ulifanya vizuri kwenye shughuli zangu nenda na wewe ukajikatie mkate, bila kujali unakata mpaka wapi.

“Tembo yule kakate tani yako. Hivi inawezekana ndege inafika mgodini inabeba inaondoka, inafika kwenye mbuga za wanyama inabeba twiga inaondoka, halafu wanasindikizwa... Palepale kiwanjani vitu vinapita, dawa za kulevya, sijui ghasia. Kwa kweli hapana jamani. Sisi wa zamani tunaona hapana.”

Kuhusu barabara alisisitiza kuwa pamoja na kuwapo madeni ya nje, anashukuru kwamba “hawakumaliza (fedha) zote” kwa kuwa waliweka mtandao wa barabara.

“Serikali naikumbuka kwa hilo, lakini kwa kuua chama imejitahidi sana,” alisema.

Magufuli na mapambano
Akimzungumzia Rais Magufuli, mbunge huyo wa zamani alisema katika kipindi kifupi amekaanga miguu ya watu wengi, wakiwamo watoto wa wakubwa na hivyo kinachotakiwa ni kumwombea ili aweze kutekeleze malengo yake.

Kuhusu safari za nje, alisema Rais Magufuli amekaa nchini kwa zaidi ya siku 100 bila kwenda nje ili ajifunze na kuelewa matatizo mbalimbali yaliyopo ndani, hivyo muda huo unatosha na sasa anaweza kutoka.

Alisema kutokana na kutokwenda nje kwa muda mrefu ameshakuwa kama mwali, hivyo akienda huko atapokewa kwa shangwe na viongozi wenzake wenye kiu ya kumwona.

Simpasa pia aliafiki uamuzi wa Kikwete kutaka kumkabidhi Magufuli kijiti mapema, akisema ndiyo utamaduni.

Alisema Magufuli akiendelea kuwa rais bila kushika chama, watu wanaoumizwa na uamuzi wake wanaweza kujiunga pamoja na kuunda mkakati dhidi yake ili aenguliwe kwa kunyang’anywa uanachama, kitendo alichosema kilimkuta aliyekuwa Rais Afrika Kusini, Thabo Mbeki na sasa kinamkabili mrithi wake, Jacob Zuma.

Uchaguzi Mkuu
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu uliopita, Simpasa alisema ulikuwa mgumu kwa sababu hawakuwa na fedha na kulikuwa na usaliti mwingi.

Alisema watu walikuwa wamekata tamaa na kugawanyika sana.
“Watu walikuwa wanapenda hela sana, atakayetoa hela ndiyo wanakwenda wake. Kwa hiyo tulipata shida. Ndio maana katika jimbo letu pale Tunduma tulipata shida, alipita mtu wa Chadema na huku Momba (pia Chadema) bado tuna kesi, hatujui itakuwaje,” alisema

Alisema ubunge wa sasa ni gharama sana na unahitaji fedha nyingi kwa ajili ya mgombea kutembea nazo kwa kuwa akienda vijijini kwa wapigakura anaulizwa “umetuachaje” tofauti na zamani walipokuwa wanachinjiwa mbuzi.

Alisema hiyo inatokana na wananchi kupata taarifa kuwa wabunge wanapata fedha nyingi, hivyo nao wanataka kupata sehemu ya fedha hizo.

Simpasa ambaye kwa sasa anashughulika na kilimo cha mpunga na mahindi na yuko mbioni kuanza ufugaji wa nyuki.MWANANNCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: