KIVUKO CHA MV KILOMERO II CHAOPOLEWA MOROGORO
Kivuko cha MV Kilombero II kikiopolewa katika Mto Kilombero mkoani Morogoro juzi jioni. Picha na Juma Mtanda
By Juma Mtanda,Mwananchi jmtanda@mwananchi.co.tz Kilombero. Kivuko cha MV Kilombero II kilichozama katika Mto Kilombero baada ya kukumbwa na dhoruba Januari 27 mkoani Morogoro kimeopolewa.
Kivuko hicho kilichosababisha vifo vya watu wawili, kiliopolewa juzi na wazamiaji wa Kampuni ya M.Divers Limited.
Mkuu wa kikosi cha uzamiaji na uokoaji kutoka kampuni hiyo, Hafidh Seif alisema wamekabiliana na changamoto mbalimbali hadi kukiopoa kivuko hicho.
Seif alisema imechukua siku 10 kufanikisha kazi hiyo kutokana na juhudi na maarifa kuhitajika wakati wa kukiopoa.
Seif alisema walikiibua kivuko hicho kwa kutumia mbinu ya kuzamisha mtoni matangi mawili yenye ujazo wa lita 5,000 na mengine manane yasiyopungua ujazo wa lita 2,000.
Alisema zilifungwa nyaya chini ya kivuko kisha kuyaondoa maji kwa upepo na kusababisha matanki hayo kuibuka na kivuko
Meneja wa Wakala wa Umeme na Ufundi Mkoa wa Morogoro (Temesa), Mhandisi Magreth Mapela alisema , shughuli itakayofuata ni mafundi kukikagua kivuko hicho ili kuona kama kuna uharibifu.
“Kuna juhudi kubwa zimefanyika tangu Januari 29 baada ya kufika kwa kikosi cha uzamiaji na uokoaji kilichopewa jukumu la kuibua kivuko, tumeona kivuko kimekaa sawa baada ya kupinduka,” alisema Mapela.
Mapela alisema baada ya kazi ya kivuko kukamilika imebaki shughuli ya kuliibua lori aina ya fuso. Hata hivyo, Mapela alisema magari mengine mawili madogo yaliibuliwa na wazamiaji hao siku tano zilizopita na kuchukuliwa na wamiliki wake.
0 comments:
Post a Comment