TAASISI YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA YAMFIKISHA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA MAHAKAMANI
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Upendo Sanga.
Mbeya. Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), imewafikisha mahakamani watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya akiwamo Mkurugenzi mtendaji, Upendo Sanga kwa madai ya kuhujumu uchumi.
Awali, Sanga alifika mahakamani hapo kusikiliza hukumu ya kesi yake iliyofunguliwa na Takukuru mwaka 2014.
Baada ya hakimu kumwaachia huru, Takukuru walimzunguka na kumkamata tena na maofisa wake ambao walipandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Sarah Martin aliwasomea mashtaka washtakiwa hao, Mweka Hazina, Hafidhi Mgagi, Mhasibu Gershom Bwire na Sanga.
Sarah alidai kuwa washtakiwa hao walimdanganya mwajiri wao na kujipatia fedha kwa kutumia nyaraka za kughushi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh4 milioni.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa Sanga na Mgagi kati ya Novemba 23 hadi 28, 2012 waliidhinisha malipo ya Sh4 milioni kwa Gershom Bwire kutengeneza vitabu 150 vya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Alidai kuwa katika shtaka la pili mshtakiwa wa tatu, Bwire Novemba 23 na 28, 2012 alijipatia fedha isivyo halali, mali ya mwajiri.
Mwendesha mashtaka alidai kuwa washtakiwa hao wameitia hasara halmashauri kwa kujipatia Sh4 milioni. Washtakiwa walikana mashtaka na kuachiwa kwa dhamana.
Hakimu wa mahakama hiyo, Rashid Chaungu aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 17.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment