SERIKALI YA INDIA YAIPIGIA MAGOTI TANZANIA KWA KITENDO CHA RAIA WAKE KUMVUA NGUO MWANAFUNZI KATIKA MJI WA NAGALORE.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika, Kikanda na Uhusiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga
SERIKALI ya India imeiomba radhi serikali ya Tanzania, kufuatia kudhalilishwa na kupigwa kwa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika, Kikanda na Uhusiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, aliliambia Bunge, jana, mjini hapa, wakati akitoa taarifa ya serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa serikali ya India kufuatia tukio hilo.
Alisema tayari serikali ya India, imewachukulia hatua wote waliohusika na tukio hilo na wamefikishwa mahakamani.
Balozi Mahiga alisema serikali ya India, imeagiza kuwa wanafunzi wa Watanzania wapewe ulinzi maalumu kwenye maeneo wanakoishi na wasindikizwe wanapokwenda masomoni.
Aidha alisema serikali ya India ilimtaka balozi wa Tanzania afuatane na maofisa waandamizi, wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India kwenda Bangalore ili kukutana na wanafunzi wa Tanzania na wengine wa Afrika kufanya mikutano na wanafunzi hao.
Balozi Mahiga alisema tukio hilo lilitokea baada ya uendeshaji mbaya wa gari uliofanywa na mwanafunzi kutoka Sudan ambaye aligonga pikipiki tatu na baada ya hapo kumgonga mama wa kihindi aliyekufa papo hapo.
Alisema baada ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alikimbia na wananchi waliokuwa jirani walichoma gari lake moto na kwamba baada ya muda lilitokea gari lingine likiwa na wanafunzi wanne Watanzania akiwemo msichana mmoja.
Balozi Mahiga alisema wananchi hao walilisimamisha gari hilo na kuwatoa nje wanafunzi hao ambapo mwanafunzi wa kike alivuliwa nguo na kutembezwa mitaani uchi, huku wanaume wakipigwa sehemu mbalimbali za miili yao na gari lao lilichomwa moto.
“Katika gari hilo kulikuwa na simu zao na document (nyaraka) mbalimbali ambazo ziliteketea,” alisema.
Alisema baada ya muda, polisi walifika lakini walishindwa kutoa ushirikiano ingawa waliwachukuwa na kuwapeleka hospitali. Balozi Mahiga alisema, “Kule hospitali walionekana wana majeraha makubwa, walitibiwa lakini ikabidi waondoke kwa sababu walikuwa hawana fedha za kutosha za kugharamia matibabu”.
Alisema baada ya hapo, Balozi wa Tanzania aliyeko India aliandika dokezo la kidiplomasia kwa serikali ya India kulaani kitendo hicho na kuitaka serikali ya India, ichukue hatua za kisheria na za haraka katika kupeleleza tukio hilo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment