UPOTEVU WA MAKONTENA 11,884 NA MAGARI 2,019 WAWATOKEA PUANI KAMPUNI ZA KUTOA MIZIGO 210 BANDARI YA DAR ES SALAAM.
UPOTEVU wa makontena 11,884 na magari 2,019 uliotokea bandarini umeifanya Mamlaka ya Bandari (TPA) kuzisimamisha kazi kampuni 210 za uwakala wa kutoa mizigo bandarini kutokana na kushindwa kuwasilisha vielelezo vya malipo waliyoyafanya wakati wa kutoa mizigo.
Kampuni hizo zinatuhumiwa kuhusika kutorosha makontena hayo kutoka katika Bandari Kavu (ICD) saba za jijini Dar es Salaam bila kulipiwa ushuru wa bandari, hivyo kuipotezea Serikali mapato ya Sh bilioni 48. Makontena hayo yalitoroshwa kati ya Julai 2014 na Aprili 2015.
Kutokana na kampuni hizo kutuhumiwa kutorosha makontena hayo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alitoa amri ya kuzitaka kuwasilisha vielelezo vinvyoonesha kuwa walifanya malipo wakati walipokuwa wanatoa mizigo bandarini.
Aidha, watumishi 15 wa TPA pia walisimamishwa kazi na kuhojiwa polisi na baadhi yao tayari wameshafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuhusika kutorosha makontena hayo na kuikosesha Serikali mabilioni ya fedha.
Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi jana aliliambia gazeti hili kuwa mawakala hao wamesimamishwa baada ya kupewa muda wa kuwasilisha nyaraka hizo mwishoni mwa Desemba mwaka jana na kushindwa.
Ruzangi alisema mawakala hao 210 ni kati ya mawakala 280 ambao waziri aliwataka kuwasilisha nyaraka za malipo kuonesha kuwa walishafanya malipo sahihi kwa mizigo ambayo waliiondoa ndani ya bandari hiyo kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana.
Profesa Mbarawa aliwapa siku saba mawakala hao wawe wameshawasilisha vielelezo vya malipo na wale ambao wanatambua kuwa hawana vielelezo hivyo walitakiwa kufanya malipo hayo ndani ya muda huo wa siku saba.
Kwa wale watakaoshindwa kufanya malipo hayo baada ya muda huo, aliagiza wakamatwe na kufikishwa Polisi ili walipe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa kufanya biashara na bandari.
Katika maelezo yake ya jana, Ruzangi alisema mara kampuni hizo za uwakala wa forodha zitakapowasilisha vielelezo hivyo vya malipo, bandari itawafungulia na kuendelea kufanya nao biashara. “Mawakala wa forodha ni wadau muhimu sana hapa bandarini, hivyo wakitimiza masharti tutawafungulia,” alieleza.
Upotevu wa makontena hayo ulijulikana baada ya TPA kufanya uchunguzi wa kina katika bandari kavu saba kubaini kama kuna upotevu mwingine wa mapato ya bandari mara baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kubaini awali upotevu wa makontena 2,400, ambayo hayakulipiwa ushuru.
0 comments:
Post a Comment