BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UTII WA SHERIA WAMKUMBA KATIBU MKUU AFYA JENGO LILILOPO JIRANI NA HOSPITALI YA MUHIMBILI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya (mbele) akisaidia kuondoa vifaa jana katika jengo lililokuwa likitumiwa na wafanyakazi wa Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambalo Rais John Magufuli alisema juzi kuwa ndani ya siku mbili jengo hilo litumike kuwa wodi ya wazazi. Picha na Omar Fungo

Dar es Salaam.
Agizo la Rais John Magufuli la kubadili matumizi ya Jengo la Wizara ya Afya, Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto lililopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana lilimfanya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya kushiriki kubeba samani kupisha uwekaji wa vitanda ili kuanza kuwa wodi ya wazazi.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo juzi alipokuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Wazee wa Dar es Salaam na kutoa siku mbili kwa maofisa 70 waliokuwa wakitumia jengo hilo kuhamishwa kuwapisha kinamama ambao wamesongamana katika jengo la wazazi lililopo.

Jana licha ya kuwa siku ya mapumziko, Dk Ulisubisya alifika Muhimbili mapema asubuhi na kushirikiana na madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine kuondoa samani za ofisi na kuziweka nje ya jengo hilo.

Hakusimamia kazi hiyo tu, bali alishiriki moja kwa moja kubeba meza, viti, kabati na kompyuta na kuvitoa kwenye ofisi hizo ili kupata nafasi ya kuweka vitanda vya wagonjwa kazi ambayo ilikuwa ikifanywa kwa kasi huku yeye na watumishi wengine wakipishana bila kupumzika kama wafanyavyo nyuki.

Kasi hiyo ilimfanya katibu mkuu huyo kutokwa na jasho kiasi cha shati alilovaa kuloa chapachapa.

Dk Ulisubisya alisema kazi hiyo ingekamilika jana jioni na kwamba shughuli ya uwekaji wa vitanda itaendelea leo.

Alisema kati ya vitanda 250 hadi 300 vitawekwa katika jengo hilo huku akisema maofisa waliokuwa hapo watatafutiwa ofisi wizarani huku taratibu nyingine zikiendelea.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Mseru alisema, jana kusingekuwa na mgonjwa ambaye angelala chini: “Mbali na lile jengo ambalo alituagiza Rais, pia jengo letu la uzazi na mtoto tumepata sehemu ambayo tunaweza kuweka vitanda 50, kwa hiyo leo wagonjwa wote watalala kwenye vitanda.”

Alisema kulikuwa na wagonjwa 50 waliokuwa wakilala chini na kwamba tatizo hilo lingemalizwa jana. Profesa Mseru alisema wamefanya hivyo, kwa kuwa jengo hilo lina huduma muhimu kama vyoo na bafu za kutosha.

Alisema ili kupata nafasi hiyo, wamehamisha kliniki ya wajawazito na kuipeleka katika jengo la afya uzazi na mtoto.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: