Juma Mtanda.
Ifakara-Kilombero. Vilio na Simanzi vimetawala wakati wa ibada ya mazishi ya mfanyakazi wa benki ya CRDB tawi la Ifakara, Dastan Rwegasira(31) anayedhaniwa kufa maji katika tukio la kupinduka kwa kivuko cha MV Kilombero II Januari 27 mwaka huu mkoani Morogoro.
Ibada hiyo ilifanyika juzi majira ya jioni kando ya mto Kilombero mita chache kutoka kivuko cha MV II Kilombero kilipopinduka na kuhudhuriwa na ndugu, jamaa, mafariki na wafanyakazi wa benki ya CRDB.
Tukio la kusomwa kwa ibada hiyo ni la pili kufanyika kufuatia ibada nyingine ya kumuombea dua marehemu huyo kwa mwenyezi mungu iliyofanyika Februari mosi nyumbani kwa wazazi wake mtaa wa Nyamvisi kata ya Ruaha wilaya ya Kilosa.
Baada ya ibada hiyo, wazazi wa Dastan Rwegasira wakiongoza na baba mzazi na mama Francis Fwegarisa, na Flora Hamadi walianza kutupa sanda majini katika mto Kilombero na baadhi za nguo za kijana huyo kama ishara ya mazishi yake na kusafirishwa na maji hayo.
Tukio lingine lililofanyika ni ndugu,kuchota mchanga nchikavu na kumwaga kwenye maji katika mto huo na sehemu za mila la kabila la wahaya.
Akizungumza na mwananchi mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo eneo hilo, Baba Mkubwa wa,Dastan Rwegasira, Melchlor Muangi (66) alisema kuwa tukio la kupinduka kwa kivuko hicho serikali ilipaswa kuwa na vifaa maalumu vya kupima hali ya hewa katika maeneo ya vivuko ili kunusuru majanga yanayoweza kuepukika huku wakimpoteza mtoto wao.
Muangi alisema kuwa ukiangalia ajali ya tukio la kukipinda kwa kivuko utaona kumesababishwa na upepo mkali na kama serikali ingekuwa na vifaa vya hali ya hewa eneo la kivuko, ajali hiyo isingeweza kutokea na kusababisha vifo na harasa nyingine ikiwemo wananchi kukosa huduma ya kivuko kwa zaidi ya wiki tangu kimetokea.
“Tumepoteza mtoto wetu mpaka sasa hajaonekana lakini kama serikali ingekuwa makini eneo hili pangekuwa na vifaa vya utambuzi wa hali ya hatari hasa upepo na mawimbi makubwa yanayoweza kusababisha majanga kwa vyombo vya mto Kilombero.”alisema Muangi.
Mama mzazi wa, Dastan Rwegasira, Flora Hamadi (57) alisema kuwa mtoto huyo amekuwa tegemeo ndani ya familia ya Francis Fwegasira (62) kutokana na moyo wa upendo kwa ndugu zake.
Flora alisema hayo wakati akiangua kilio katika ibada hiyo na kumuelezea mtoto huyo alikuwa na moyo wa huruma kwa ndugu, jamaa na marafiki lakini ibada iliyofanyika ni miongoni mwa kumuombea kwa mwenyezi mungu ili apumzike kwa amani maana hawajui kama aliweza kuomba dua njema kabla ya kukutana na umauti.
Ibada hiyo iliendesha na kaka mkubwa wa Dastan, Felician Rwegasira ambaye ni Mhasisi wa vyama vya kitume katika kanisa katoliki parokia ya Ruaha wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Felician alisema kuwa katika ibada hiyo kuwa mwanadamu anapaswa kujiandaa na safari ya kifo kwa maana ya hajui saa wala dakika.
Wakati huo huo zoezi la kukinasua kivuko cha MV II Kilombero kilichopinduka, tayari juhudi za kukiibua kivuko hicho nchikavu zimeanza kuonekana baada ya kuibuliwa nusu.
Kuibuka nusu kwa kivuko hicho kunatokana na kazi ya kampuni ya uzamiaji na uokoaji ya M.Divers Ltd kuzamisha matanki mawili yaliyofanikisha kukiibua nusu baada ya matanki hayo kutolewa maji yaliyoibuka na nusu ya kivuko hicho.
Mkuu wa kikosi cha uzamiaji na uokoaji kutoka kampuni ya M. Divers Ltd ya Dar es Salaam, Hafidh Seif aliliambia gazeti hili kuwa jana (juzi) walizamisha matanki mawili ya lita 5000 kila moja kisha matanki hayo kufungwa nyaya chini ya kivuko na maji yalipoondolewa kwa upepo kutumia kompresa kiliibuka nusu.
“Kazi hii ni ngumu kinachofanyika ni kutumia sayansi na hesabu ili kukiibua kivuko na mambo hayo yote yanaenda pamoja ili kufanikisha kazi ya kukiibua kivuko.”alisema Seif.
Seif alisema kuwa baada ya kufanikiwa kazi hiyo na kivuko kuibuka nusu, wameongeza matanki mengine tisa ambayo yamezamishwa leo (jana) na kazi itapoanza kutolewa maji kivuko hicho kitaibuka bila pingamizi.
“Tayari matanki tisa yenye ujazo wa lita 2000 na lita 3000 yamezamishwa kisha kufungwa nyaya chini ya kivuko na yatapotolewa maji kwenye matanki hayo yataibuka juu ya maji pamoja na kivuko hicho.”alisema Seif.
Meneja wa Wakala wa Umeme na Ufundi mkoa wa Morogoro (Temesa) Mhandisi Magreth Mapela aliwaomba wananchi kuwa na subira wakati watalaamu mbalimbali wakifanya kazi ya kuibua.
Mapela alisema kuwa baada ya kuibuka kwa kivuko hicho mafundi wa Temesa watakuwa na jukumu la uchunguzi wa kina wa kukagua kivuko hicho ili kukifanyia marekebisho yatayojitokeza ili kifanyiwe matengenezo kisha kukirejesha majini ili kiendelee na kazi kuvusha watu pamoja na mali zao.
"Juhudi zimeanza kuonekana baada ya kivuko kwa sasa kuibuliwa nusu na juhudi hizi nina imani zitaendelea kuzaa matunda na leo (jana) tutapata majibu ya kuibuka chote endapo mambo yataenda vizuri”alisema Mapela.
Mapela alisema kuwa baada ya kivuko kuibuka chote kazi itayofuata ni kukivuta kwa kutumia magari matatu, mawili yakiwa ya kunyanyua vitu vizito yenye uzito wa tani 25 kila moja wakati gari lingine lina tani 35 kwa pamoja yatashirikiana kukivuta nchikavu.
0 comments:
Post a Comment