ZITTO KABWE AMWAGIA SIFA RAIS JOHN MAGUFULI KATIKA KUPAMBANA NA RUSHWA NA UFISADI.
CT- Wazalendo, Zitto Kabwe akielezea kwa waandishi wa habari jana maazimio yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwenye kikao chao kilichofanyika juzi Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Msafiri Mtemelwa.
CHAMA cha Wazalendo (ACT-Wazalendo) kimepongeza juhudi za Rais John Magufuli katika kupambana na rushwa na ufisadi na kumtaka pia kuangalia uwezekano wa kufuta posho za vikao katika mfumo wa utumishi wa umma, ikiwamo Bunge.
Hayo yamebainishwa na kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto alipokuwa akizungumzia mambo yaliyojadiliwa kwenye kikao cha Kamati Kuu, juzi.
“Rais anatakiwa kugeukia suala la posho, afute posho za vikao kwa mfumo wa watumishi wa umma, ikiwamo Bunge na kuachana na matumizi ya magari ya anasa (mashangingi),” alisema Zitto.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alisema Serikali pia inatakiwa kuleta mabadiliko ya kimfumo, ikiwa ni pamoja na kubadili mikataba ya kinyonyaji ya rasilimali kama ya madini na mafuta na kuachana na kuagiza sukari nje na kufanya mabadiliko katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
“Kamati Kuu ilipokea na kujadili utendaji wa serikali ya awamu ya tano na kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa na ufisadi nchini kupitia dhana ya ‘kutumbua majipu,” alieleza.
Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar, alisema pamoja na chama chake kuazimia kutoshiriki uchaguzi wa marudio, wanaamini suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar ni kufanya mazungumzo yatakayojumuisha wadau wote muhimu katika mchakato wa uchaguzi.
Kuhusu taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, alisema chama chake kimepokea na kupitisha taarifa ya mapato na matumizi katika Uchaguzi Mkuu ambapo aliainisha kuwa, ACT ilitumia Sh 656,625,000.
0 comments:
Post a Comment