BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SABABU ZILIMFANYA RAIS DK MAGUFULI AMFUKUZE KAZI RC ANNA KILONGO NDIYO.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela.

RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela (pichani), baada ya mkuu huyo wa mkoa kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari kuwa mkoani kwake hakuna watumishi hewa.

Dk Magufuli pia ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa huo wa Shinyanga (RAS), Abdul Dachi, kutokana na kile alichosema kwamba ameshiriki kwa namna moja kumpatia taarifa za uongo Malecela kwamba hakuna watumishi hewa mkoani humo.



Taarifa ya viongozi hao kuvuliwa wadhifa huo, ilitolewa jana na Rais Magufuli baada ya kupokea taarifa ya mwaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na taarifa ya Bunge katika kuitikia mwito wa Serikali wa kubana matumizi.

Alisema baada ya Kilango kutoa taarifa iliyoonesha kwamba mkoani kwake hakuna watumishi hewa, aliunda tume maalumu kwa ajili ya uhakiki na ndani ya siku moja, walibaini kuwepo watumishi hewa 45 waliokuwa wameshalipwa mishahara yenye gharama ya Sh milioni 333.9.



Magufuli alisema alishangazwa na taarifa za Mkuu wa Mkoa huyo kwamba mkoani kwake hakuna mtumishi hewa yeyote, wakati katika mikoa mingine, wakuu wa mikoa walikuwa kila siku wakitaja idadi ya watumishi hewa waliobainika.

“Nilikuwa mapumzikoni Chato nikifuatilia kila siku taarifa za maRC, wakitaja idadi ya watumishi hewa waliobainika, lakini nilishangaa kuona RC wa Mkoa wa Shinyanga akidai hakuna watumishi hewa.



Niliamua kuagiza timu yangu maalumu ika-verify (kuhakiki) kama kweli hakuna mtumishi hewa mkoani humo,” alisema. Alisema hadi usiku wa jana, timu hiyo ilimpatia taarifa kuwa mkoani humo wamepatikana watumishi hewa 45.

Timu hiyo ilisema bado wilaya mbili za mkoa huo, ambazo ni Ushetu na Shinyanga Vijijini hazijafikiwa na uhakiki huo. Alisema katika taarifa hiyo, watumishi hao hewa walikuwa wameshalipwa mishahara ya jumla ya Sh milioni 333.9. “Kwa kweli nimejiuliza sana tena kwa masikitiko kwa nini RC huyu alidai hakuna watumishi hewa mkoani kwake?

Lengo lake ni nini?
Na kama alidanganywa na watendaji kwa nini hakuhakiki taarifa hizo kwanza na badala yake akaamua kusema uongo?” Alihoji Magufuli.



Alisema kwa mujibu wa timu aliyoituma mkoani humo, ana uhakika baada ya uhakiki kukamilika katika wilaya zote mkoani humo, idadi ya watumishi hewa itaongezeka zaidi.

Magufuli alisema anafahamu tatizo lilivyo na ndiyo maana Machi, 15 mwaka huu, wakati akiapisha wakuu wote wa mikoa aliowateua, aliwapa siku 15 hadi Machi 31 , wawe wamewasilisha majina ya watumishi hewa waondolewe kwenye orodha ya watumishi wanaolipwa mishahara.

Alisema ameamua kulivalia njuga suala hilo la watumishi hewa kwa kuwa Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi zinazoweza kutumika katika maeneo mengine ya maendeleo na kuwakwamua wananchi wanaoteseka kwa umasikini.

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema wakuu wengi wa mikoa walifanyakazi nzuri kwani hata alipokuwa likizo nyumbani kwake Chato, alishuhudia wengi wao wakitaja idadi ya watumishi hewa waliobainika.

Siku 28 za Kilango Kilango aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Machi 14, mwaka huu na kuapishwa kushika wadhifa huo aliotumikia kwa siku 28 Machi 15, mwaka huu hadi jana alipotenguliwa kushika wadhifa huo.

Kabla ya uteuzi huo, mwanasiasa huyo alikuwa Mbunge wa Same Mashariki kwa vipindi viwili mfululizo; yaani miaka 10, hadi pale katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana alipoangushwa na jimbo hilo kwenda kwa Naghenjwa Kaboyoka wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akiwa mbunge, Kilango alishika pia nafasi ya Unaibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.



Bilioni 54/- zaokolewa Wakati huo huo, Rais Magufuli amesema hadi jana, jumla ya watumishi hewa 5,507 wamebainika huku kwa hesabu za haraka zikionesha Sh bilioni 54 zimeokolewa. Alisema watumishi hao hewa walitokana na watumishi waliokufa, kufungwa, kustaafu na kufukuzwa kazi.

“Serikali imekuwa ikitenga kila mwezi kiasi cha Sh bilioni 583 kwa ajili ya malipo ya mishahara ambayo ndani yake watumishi hewa wengi pia walikuwa wanalipwa.



“Nawaahidi kuwa baada ya operesheni hii tutachanganua fedha zilizookolewa na wahusika watatafutwa hadi wabainike. Lakini kwa hesabu za haraka kupitia operesheni hii jumla ya Sh bilioni 54 zimeokolewa. Hizi ni fedha nyingi sana kwa nchi kama Tanzania,” alifafanua.

Mwanafunzi alipwa mshahara Awali akizungumzia operesheni hiyo ya kusaka watumishi hewa, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi alisema wilayani Kibaha walibaini kuwepo kwa Ofisa wa Utumishi aliyetumia madaraka yake vibaya na kutumia mshahara wa mtumishi hewa kumlipa mwanafunzi na mstaafu. Alisema katika wilaya hiyo, mmoja wa watumishi alisimamishwa kazi.

Baada ya mwezi mmoja, Ofisa wa Utumishi huyo wa Kibaha, aliandika barua Utumishi akidai Baraza la Madiwani limemrejesha kazini mtumishi huyo jambo ambalo halikuwa kweli. Kwa mujibu wa Yambesi, Ofisa Utumishi huyo, alitumia fursa hiyo kumfungulia akaunti mwanafunzi ambaye alinufaika na mshahara wa mtumishi huyo.

Taasisi zote kumulikwa Alisema anatambua kuwa bado yapo maeneo mengi ambayo hayajafikiwa ipasavyo ikiwemo halmashauri, Serikali Kuu, jeshini, wizarani na hata Ikulu. Alionya kuwa katika maeneo yote ya utumishi yatakayohakikiwa endapo itabainika kuwepo kwa mtumishi hewa, wahusika watakuwa wamejifuta kazi wenyewe.

Rais Magufuli alisema nchi ili shafikia pabaya hivyo endapo Serikali itaachia hali iendelee kama ilivyo , haitafika mahali pazuri. Ukaguzi wa kushitukiza Alisema katika kudhibiti tatizo la watumishi hewa timu yake ya ukaguzi ya kushitukiza itapitia maeneo yote ya utumishi na kukagua. “Timu yangu inaongozwa na mwanamke jembe inafanya vizuri sana.

Kuanzia sasa naomba ipewe ulinzi ili ifanye kazi yake vizuri,” alisema bila kutaja jina la kiongozi huyo wa timu. Alisema Serikali yake ya Awamu ya Tano imeamua kuhakikisha inainua maisha ya Watanzania wanaoteseka kwa umasikini na ndio maana hata bajeti ya mwaka ujao ya 2016/2017 fedha za maendeleo zimepanda kutoka asilimia 26 ya bajeti ya mwaka huu ya 2015/2016 hadi kufikia asilimia 40.

Wanaolalamika wajiondoe “Nimeshaanza kusikia kuna watendaji eti wanalalamikia fedha za matumizi ya kawaida (OC) ni ndogo, natangaza hapa kama kuna mtendaji au Waziri anayeona OC hazimtoshi ajiondoe mwenyewe kabla sijamuondoa. Tena nitaweka wapelelezi wangu wawarekodi mawaziri wote wanaolalamika halafu nitawashughulikia,” alisisitiza.

Alisema katika awamu yake ya uongozi anataka kujenga Tanzania mpya kwa kununua ndege mpya za Serikali, kujenga reli za kisasa, kununua meli bora, kuongeza bajeti ya afya na barabara zijengwe katika mikoa yote ambayo hadi sasa haijafikiwa na barabara za lami.

“Nawaombeni Watanzania wenzangu mniunge mkono kwa hili, nafanya hili kwa faida ya Watanzania, najua kuna wale waliozoea vihela vya hovyo watachukia kweli waacheni wachukie wao ni wachache, lakini wengi watanufaika,” alisema Dk Magufuli.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: