Wakulima wa zao la pamba wameshauriwa kujenga makini wakati wanapopatiwa maelekezo na watalaamu juu ya matumizi sahihi ya viatilifu na vinyunyuzi vitakavyosaidia kudhibiti na kuwaua wadudu waharibifu wa mimea ya mazao hayo ili kupata mazao ya kutosha.
Akizungumza katika mafunzo ya siku moja na wakulima viongozi wa kanda ya mashariki mkoani Morogoro jana, Afisa Huduma za Usimamizi Bodi ya Pamba Tanzania, Mwangulumba Emmanuel alieleza kuwa ili mkulima apate mazao ya kutosha anapaswa kufuata maelekezo ya matumizi sahihi ya viatilifu na vinyunyuzi.
Mtafiti wa pamba Kilosa, Yassin Mashuhubu kushoto akimwangalia mkulima kiongozi, Said Mfaume wakati wa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yamelenga kuwafundisha wakulima mbinu sahihi za matumizi bora ya dawa mpya ya kuua wadudu waharibifu wa miche ya mazao ya pamba aina ya Ladex pamoja na matumizi ya pampu ya kuchanganyia dawa aina ya matabi.
Emmanuel alisema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakulima kushindwa kufuata maelekezo ya watalaamu juu ya matumizi sahihihi ya viatilifu na vinyunyuzi na endapo hesabu zitakosewa wakati wa matumizi hayo mkulima huambulia mazao kidogo.
“Wadudu waharibifu wa mazao ya pamba ni wakorofi na wasipodhibitiwa vyema wakati wa matumizi ya viatilifu na vinyunyuzi, mkulima ataambulia mazao kidogo”.alisema Emmanuel.
Emmanuel alitaja maeneo yanayolimwa zao la pamba katika kanda ya mashariki kuwa ni pamoja na Iringa Vijijini, Kilosa, Bagamoyo, Malinyi, Handeni na Same, Lushoto, Mvomero, Mwanga, Ulanga, Babati na Rufiji.
Maeneo hayo ndiyo tumelekeza nguvu ya kufufua zao la pamba baada ya wakulima kukatishwa tamaa kutokana na sababu mbalimbali.alisema Emmanuel.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Utafiti wa Zao la Pamba Kanda ya Mashariki na Mtafiti wa Wadudu wa Pamba kutoka kituo cha Utafiti wa Kilomo Ilonga, Dkt Furaha Mrosso alieleza kuwa mimeo ya miche ya pamba inapendwa wadudu waharibufu na wasipodhibitiswa husababisha hasara zaidi ya asilimia 70 ya mavuno.
Dkt Mrosso alieleza kuwa kuna aina mbalimbali za wadudu hatari waharibifu wakiwemo funza vitumba, wadudu mafuta, kanga mbili, funza mwekundu-mweupe (pink bollworm) na funza mwenye nywele (spiny boll worm).
Wadudu wengine wanaojitokeza kwa baadhi ya maeneo kanda ya mashariki ni vidung’ata na vithiripi na n:k.
Kwa upande wa mkulima kiongozi kutoka Ulanga kijiji cha Iputi, Said Mfaume alisema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwani kumekuwa na tabia ya kubadilika kwa dawa za kuua wadudu na wengi hawajui matumizi sahihi ya madawa.
“Tumepata elimu ya matumizi sahihi ya viatilifu na vinyunyuzi nasi tutaenda kutoa elimu kwa wakulima wenzetu ili kupata mazao ya kutosha na kuepukana na umasikini usio wa lazima.”alisema Mfaume.
0 comments:
Post a Comment