BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ASKOFU GWAJIMA AIKIMBIA NCHI NI BAADA YA JESHI LA POLISI KUMSAKA USIKU NA MCHANA.


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima

WAKATI Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, likiendelea kumtafuta kwa udi na uvumba Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, vyanzo vya uhakika vinadai kuwa ametimka nchini tangu Jumatano.

Juzi, askari kadhaa wa jeshi hilo waliweka kambi katika nyumba ya Askofu Gwajima iliyopo kwenye Mtaa wa Kealanda, Mbezi Salasala jijini Dar es Salaam kutokana na kile kilichodaiwa kuwa anasakwa kwa ajili ya mahojiano.

Hata hivyo, taarifa rasmi za Polisi kutoka kwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime, hazikueleza sababu za kutafutwa kwa askofu huyo.

Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana kuwa askofu huyo aliondoka nchini Jumatano ambayo ni siku moja kabla ya polisi kufika nyumbani kwake. Inadaiwa kuwa alitumia usafiri wa ndege ya shirika moja kubwa la Uarabuni iliyokuwa ikielekea Dubai, Falme za Kiarabu.

“Ni kweli Polisi wanaendelea kumtafuta… hata hivyo, alishaondoka nchini tangu Jumatano na hivyo sidhani kama huko aliko ameshapata taarifa kuwa anatafutwa,” chanzo hicho cha uhakika kiliiambia Nipashe.

Hata hivyo, hadi kufikia jana jioni, Nipashe haikupata taarifa zaidi kuhusiana na undani wa safari hiyo, ikiwa ni pamoja na nambari ya ndege na siti aliyoketi.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda Fuime alisema kuwa Askofu Gwajima bado hajapatikana, ingawa jeshi hilo lilianza kumtafuta tangu Alhamisi.

“Bado hatujampata na tunaendelea kumtafuta… atapatikana tu. Isipokuwa tunakomtafutia siwezi kuweka wazi. Sisi tunajua, na Jeshi la Polisi huwa halimuonei mtu,” alisema Kamanda Fuime na kuongeza: “ Mtu mpaka utafutwe ujue kuna kitu umefanya.

Hatuwezi kuanza kumsaka mtu kati ya Watanzania mamilioni waliopo kama hajakosea kitu.” UTULIVU NYUMBANI KWA GWAJIMA Jana alasiri, Nipashe ilifika katika nyumba ya askofu huyo na kushuhudia ukimya mkubwa ukitawala katika mazingira ya ndani na nje ya nyumba hiyo.

Mwandishi wa Nipashe alijaribu kugonga geti la kuingia ndani ya nyumba ya Askofu Gwajima kwa dakika kadhaa bila ya kujibiwa, huku kukiwa na kila dalili kuwa wakati huo hakukuwa na mtu.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliokutwa katika maeneo ya jirani na mahala hapo na kukataa kujitambulisha majina yao lakini wakidai kuwa wao ni majirani wa Askofu Gwajima, walisema wanashangazwa na kitendo cha Polisi kupiga kambi mahala hapo kumtafuta askofu huyo kwa namna walioonekana juzi. Mmoja wa majirani hao, alisema ameshangazwa na hatua ya Polisi kumtafuta askofu huyo wakati ana mawasiliano ambayo ni dhahiri jeshi hilo lingeweza kuyatumia ili kumpata.

“Walifika hapa na kuizingira nyumba yake. Baadaye nikasikia wanamtafuta. Nashangaa ni kwanini walitumia mbinu hiyo wakati askofu ana simu ya mkononi na pia ana ofisi ambako anaweza kupatikana kirahisi,” alisema mmoja wa watu hao.

“Ilitakiwa kabla ya kufika kwa nia ya kumkamata wampe taarifa, waone kama atashindwa kuripoti ndipo itumike njia nyingine. Sidhani kama hatua zote hizo zilifuatwa,” aliongeza.

Mtu mwingine aliiambia Nipashe kuwa hiyo siyo mara ya kwanza kwa Askofu Gwajima kufuatiliwa na vyombo vya dola, na hivyo hawakustushwa sana ingawa wanaamini kuwa polisi wangeweza kutumia njia nyingine za kumpata na kuhojiana naye badala ya hiyo ya kuweksa kambi kwake kwa saa kadhaa.

MISUKOSUKO
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa hii siyo mara ya kwanza kwa Jeshi la Polisi kuizingira nyumba ya Askofu Gwajima. Aliwahi pia kutafutwa akidaiwa kutoa kauli za kumkashifu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinali Pengo.

Askofu Gwajima alituhumiwa kumkashifu Askofu Pengo wakati alipodai kuwa amewasaliti viongozi wenzake wa Kikristo kwa kuwataka waumini wa dini hiyo kuamua wenyewe suala la Katiba inayopendekezwa kinyume cha msimamo wa waraka wa kupinga katiba hiyo uliotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (CCT).

Katika tukio la juzi, Fuime alisema Jeshi la Polisi lilitumwa kwenda katika nyumba ya sskofu huyo ili kumchukua na kumpeleka katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kuhojiwa. 


Hata hivyo, taarifa zaidi zilihusisha kuzingirwa kwa nyumba ya Askofu Gwajima na sauti yake inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikitoa tuhuma kadhaa dhidi ya Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete; yakiwamo ya kuwapo kwa mpango wa kutaka mwenyekiti huyo wa CCM aendelee kubaki madarakani ndani ya chama chake badala ya kumpisha Rais John Magufuli anayepaswa kuwa na kofia mbili za uongozi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: