BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DILI LA MFANYABIASHARA LA KIIBIA SERIKALI SH7 MIL KWA DAKIKA MOJA LATIBULIWA.

 
RAIS John Magufuli jana alilitangazia taifa kuwa vyombo vya dola vinamshikilia mtu aliyekuwa akiibia serikali mapato yatokanayo na kodi zinazolipwa kulingana na matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD) na kujiingizia Sh. milioni saba kwa dakika.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya kuapishwa kwa wakuu wapya wa mikoa na ulaji wa viapo vya uadilifu kwa wakuu wa wilaya aliowateua Jumapili, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli hakutaja jina la mtu huyo, lakini akasema alikuwa anashirikiana na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kufanikisha ufisadi huo wa kutisha.

Alisema mtu huyo ameipotezea serikali trilioni nyingi katika shilingi, baada ya kuwa anauza risiti za EFD kwa wafanyabiashara kwa tozo ya kodi ya asilimia tano.

Ukijumlisha na asilimia 18 ya tozo halali ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), alisema Rais Magufuli kwa masikitiko, mtu huyo alikuwa anaikosesha serikali mapato ya asilimia 23 ya kodi za kila mfanyabiashara.

Alisema wamebaini mtu huyo alikuwa anaingiza Sh. milioni saba hadi nane kwa dakika moja kutokana na mchezo huo mchafu wa kuchakachua risiti za EFD za wafanyabiashara.

"Bahati nzuri yuko kwenye mikono salama... Hiyo ndiyo Tanzania," alisema Magufuli.

Kutokana na changamoto hiyo, Rais aliwaagiza wakuu hao wa wilaya kwenda kusimamia vizuri mapato ya serikali.

Alisema baadhi ya wakurugenzi wa wilaya wamekuwa wakitumia vibaya mapato ya serikali kana kwamba ni mali yao.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli aliwataka wakuu wapya wa wilaya kuhakikisha wanawasimamia vizuri kwa mujibu wa sheria.

...'AWANANGA’ MA-DC WA JK

RAIS John Magufuli amesema wakuu wa wilaya 74 aliowaacha katika uteuzi wake mpya, hawakukidhi vigevyo anavyovitaka.

Jumapili, Rais Magufuli aliteua wakuu wakuu wa mikoa watatu na wakuu wa wilaya 166 huku akiwatema wakuu wa wilaya 74 walioteuliwa na Rais wa nne, Jakaya Kikwete, maarufu 'JK'.

Katika hafla ya kuapishwa kwa wakuu hao wapya wa mikoa na kiapo cha adilifu kwa wakuu wa wilaya Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema kazi ya uteuzi huo haikuwa nyepesi na alilazimika kuwatema baadhi ya wakuu wa wilaya kutokana na kutokidhi vigezo vilivyokuwa vinahitajika.

“Ilikuwa kazi ngumu, tulihitaji kujua historia ya kila mmoja,” alisema.

“Ndiyo maana mnaona ma-DC 39 au 38 hivi waliokuwapo wamebaki. Wengine hawakufikia vigezo tulivyovitaka.”
Rais aliwataka wakuu hao wa wilaya kuiga mfano wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye alifanya vizuri alipopewa nafasi hiyo.

"Wakurugenzi 22 waliofanya vizuri katika maeneo yao, tuliwapandisha," alisema Rais Magufuli.


“Ukuu wa wilaya ni nafasi kubwa. Nendeni mkafanye kazi vizuri kwenye maeneo yenu, mfano mzuri ni mkuu wa wilaya mstaafu ambaye sasa ni Waziri Mkuu (Majaliwa). Alitimiza vizuri wajibu wake na leo yuko hapa.”

Awali Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakuu hao wa mikoa na wilaya kwenda kutatua changamoto ya uhaba wa madawati na chakula katika maeneo yao.

"Kikubwa, nawaomba msome alama za nyakati, someni kwa waliopo, mjifunze kwa wengine. Kazi ya ukuu wa wilaya haina cha umri mdogo," alisema.

Naye Majaliwa aliwataka vingozi wpaya hao kutambua maeneo yao wanayoyaongoza, wasaidizi wao, Kamati ya Ulinzi na Usalama, kusimamia fedha za halmashauri na kufuatilia miradi ya maendeleo badala ya kukaa ofisini.

Kiongozi huyo wa serikali pia aliwataka wakuu hao wa mikoa na wilaya kuisoma na kuifanyia kazi hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa wakati wa kufungua Bunge la 11 mwishoni mwa mwaka jana.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: