BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MA-DC WA RAIS MAGUFULI RUKSA KUPOKEA ZAWADI YA FEDHA ISIYOZIDI SH50,000 LAKINI

Baadhi ya wakuu wa wilaya wapya wakila kiapo Ikulu Dar es Salaam jana.

MSEMO wa ‘kunyang’anywa tonge mdomoni’ umezoeleka kwa walio wengi, lakini sasa, Emile Ntakamulenga, anaweza kuuzungumzia kwa kina, baada ya kutaarifiwa sekunde za mwisho kabla ya kula kiapo cha maadili cha kutumikia wadhifa wa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, kuwa uteuzi wake ulitangazwa kimakosa.

Msemo wa ‘kunyang’anywa tonge mdomoni’ umezoeleka kwa walio wengi, lakini sasa, Emile Ntakamulenga, anaweza kuuzungumzia kwa kina, baada ya kutaarifiwa sekunde za mwisho kabla ya kula kiapo cha maadili cha kutumikia wadhifa wa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, kuwa uteuzi wake ulitangazwa kimakosa.

Hali hiyo ilijitokeza jana jijini Dar es Salaam, baada ya Rais John Magufuli, kuwahutubia wakuu hao wa Wilaya wateule juu ya kile ambacho anataka wakafanye kwenye maeneo yao.

Baada ya hotuba hiyo, Rais Magufuli alipiga picha ya pamoja na wakuu hao wa wilaya wateule, akiwamo Ntakamulenga, na baada ya hatua hiyo waliingia kwenye chumba maalumu kula kiapo cha maadili.

Baada ya kukabidhiwa nakala za viapo kila mmoja akiwamo Ntakamulenga, sekunde chache kabla ya kuapa na kusaini viapo hivyo, ndipo zilipokuja taarifa mbaya kwa mteule huyo aliyefaidi jina la ‘mheshimiwa’ tangu Jumapili iliyopita, majina ya wakuu wa wilaya wateule yalipotangazwa.

Wakati kukiwa na utulivu wa hali ya juu kwenye ukumbi huo, ndipo Kamishna wa Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alipotangaza kwamba kuna marekebisho ya wateule ambayo yamefanyika.

Alisema katika uteuzi huo, jina la Ntakamulenga liliingia kimakosa hivyo nafasi yake imechukuliwa na Nurdin Hassan Babu ambaye kwenye orodha iliyotolewa na Ikulu Juni 26, hakuwepo.

"Naomba niwatangazie kuwa idadi ya wakuu wapya wa Mkoa walioapishwa leo wote wamefika, lakini katika orodha ya wakuu wa wilaya, kuna DC mmoja uteuzi wake ulikosewa ambaye ni DC wa Serengeti. Hivyo naomba asimame atupishe tuendelee na utaratibu wetu," alisema Jaji Kaganda.

Wakati Ntakamulenga akitoka nje ya ukumbi huo, Jaji Kaganda alimwambia "Pole sana, usijali ni mambo ya kawaida tu na huwa yanatokea hapa duniani."

ATOA YA MOYONI

Mara baada ya kutoka nje ya ukumbi huo, Ntakamulenga aliiambia Nipashe kuwa "Nilikuwa sijui lolote."

"Na nimekuja hapa kama mteule pekee wa wilaya ya Serengeti, na nilikuwa nasubiri kuapa, hayo mengine siyajui na wala siwezi kuzungumza chochote."

Katika orodha ya wakuu wa wilaya wateule, jina la Ntakamulenga lilikuwa la pili kwenye orodha ya wakuu wa wilaya wa Mkoa wa Mara.

Katika orodha hiyo, jina la kwanza lilikuwa la Mkuu wa wilaya ya Rorya, Simon Chacha, huku la tatu likiwa la Mkuu wa wilaya ya Bunda Lydia Bupilipili, likifuatiwa na lile la Mkuu wa Wialaya ya Butiama, Anarose Nyamubi.

Wakuu wengine wa wilaya za mkoa wa Mara ni Glodious Luoga (Tarime) na Dk. Vicent Naano (Musoma).

MTU MMOJA KAZI MOJA

Awali akihutubua wateule hao, Rais Magufuli alizungumzia pia, makosa yaliyofanyika kwa uteuzi wa Mkuu wa Wialaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na Ikungi, mkoani Singida.

Akizungumzia nafasi ya aliyeteuliwa awali kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Rais Magufuli alisema, jina la Fikiri Said lilitangazwa kimakosa na hivyo Mkuu wa Wilaya halali wa wilaya hiyo ni Lukaturu.

Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Rombo mteule aliyetangazwa awali, Fatma Hassan Toufiq, Rais Magufuli alisema makosa yalifanyika kwenye kutangaza jina lake kwa sababu tayari ni mbunge.

Alisema katika utawala wake anataka mtu mmoja awe na nafasi moja tu ili kuleta ufanisi kwenye kazi.

"Haiwezekani katika Watanzania milioni 50 tukose watu hadi turundikie watu vyeo. Tunataka tuchape kazi kwa ufanisi na ufanisi hauwezi kuja kwa kumrundikia mtu vyeo," alisema.

"Rombo tulimteua Toufiq tukimhamisha kutoka Manyoni lakini pia huyu ni Mbunge. DC wa Rombo ni Hokololo. Mtu mmoja kazi moja," alisema.

SH. 50,000
Jaji Kaganda aliwaonya wakuu hao wa wilaya kutopokea zawadi inayozidi thamani ya Sh. 50,000 kwa kificho, bali wanapaswa kuitangaza.

Alisema ahadi za uadilifu zinapaswa kuwekwa ukutani katika ofisi zao pamoja na kuzisoma kila siku.

"Msitumia vibaya madaraka yenu, msipokee zawadi ovyo ovyo, leo utaletewa zawadi ya ngo'ombe 70 hadi 80, hiyo ni rushwa ya kuwekeza kwani huyo mtu aliyekupa zawadi akikufuata siku nyingine umsaidie huwezi kukataa," alisema Jaji Kaganda.

Aidha, aliwaonya wakuu hao wa wilaya kuwa makini na kutojihusisha na vitendo vya ngono na watoto wa shule kwani inaliweka doa serikali.

WAHUSIKA WAZUNGUMZA

Mkuu wa Wilaya Mteule wa Chato, Shaaban Ntarambe, aliwataka wananchi wa wialaya hiyo kumpa ushirikiano katika kuimarisha ulinzi na usalama.

Alisema atashirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuhakikisha ulinzi unakuwapo muda wote.

Naye Mkuu wa Wilaya Mteule wa Kaliua, Busalama Yeji, alisema atakwenda kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwapatia mahitaji muhimu na kutatua migogoro ya ardhi.

Mkuu wa Wilaya Mteule wa Kasulu, Kanali Martin Mkisi alisema atatumia medani za kijeshi katika kuhakikisha suala la ulinzi na usalama inapatika wilayani humo.

Alisema atashirikiana na Kamati ya Ulinzi na usalama katika kutatua kero za wananchi na kuwapatia huduma wanazozihitaji.

Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Kanali Elisha Gaguti alisema heshima aliyopewa na Rais Magufuli ataitumia vizuri bila ya kumwangusha.

Alisema wilaya ya Buhigwe ni wilaya inayohitaji msaada mkubwa wa kimaendeleo hivyo atahakikisha anatatua kero zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo. 


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi mteulwe, Luteni Kanali Denis Mwila alisema atafuata maagizo aliyopewa na Rais Magufuli ikiwamo la kupambana na rushwa pamoja na kumaliza migogoro ya ardhi.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: