BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HIVI MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI IMESHINDWA KUDHIBITWA MOROGORO ?.

Wafugaji wakiwa eneo la Mikumi tarafa ya Ifakara wilaya ya Kilombero tayari kusafirisha mifugo wakati la zoezi la kuondoa mifugo wilaya ya Kilombero katika bonde la Kilombero mkoani Morogoro mwaka 2012.Picha ya maktaba/MTANDA BLOG

Juma Mtanda, Morogoro.
Wilaya ya Malinyi ni moja kati ya wilaya changa zinazounda Mkoa wa Morogoro kutokana na eneo hilo kubarikiwa na mabonde ya ardhi yenye rutuba limekuwa kivutio kikubwa kwa shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji.

Kutokana na vivutio hivyo miaka ya hivi karibuni kumejitokeza matukio yanayosababisha ardhi kuwa chanzo cha migogoro na binadamu kupoteza maisha.

Kwa nini tunaruhusu ardhi iwe chanzo cha watu kupoteza maisha na wengine kuwa na vilema vya kudumu? Je, wawakilishi wa Serikali Kuu kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, tarafa, wilaya hadi mkoa wanakuwa wapi mpaka kunatokea vurugu au mauaji yanayosababishwa na ardhi?

Moja za kazi za viongozi hao katika jamii ni kusimamia miradi, kazi za maendeleo na kutatua kero na changamoto ili wananchi waweze kutumia vyema mwanya wa kusukuma gurudumu la maendeleo mbele kwa amani, umoja, upendo na utulivu.

Miaka ya hivi karibuni Malinyi imekumbwa na wimbi la mauaji na kutokana na uzembe wa viongozi kushindwa au kufumbia macho taarifa za kiintelejisia zinazoashiria uvunjifu wa amani na kushindwa kuchukua hatua kabla ya matukio ya namna hiyo hayajajitokeza na kusababisha athari kwa jamii.

Moja ya mifano hai iliyojitokeza ni watu kupoteza maisha na wengine kupatwa na ulemavu wa kudumu likiwamo tukio la wafugaji watano kupigwa risasi katika moja za operesheni za kuwaondoa wafugaji eneo la Maguba Malinyi mwaka 2012.

Wafugaji hao ni wakazi wa eneo la Maguba lililopo Kitongoji cha Lubemend, Kijiji cha Kiwale ambako tukio hilo lilitokea baada ya wafugaji kudaiwa kupinga kukamatwa kwa mifugo yao iliyodaiwa kuingia katika eneo la hifadhi jambo ambalo siyo kweli.

Tukio lingine lililowahi kutokea katika wilaya hiyo ni la mfugaji, Baya Kidiga (20) wa Kitongoji cha Lugengeni, Kijiji cha Ipera Asilia kudaiwa kupigwa risasi Januari 26, mwaka 2013 na askari polisi.

Mazingira ya tukio hilo inadaiwa yalitokana na askari kufyatua risasi iliyomlenga Kidiga wakati akilisha mifugo yake katika eneo hilo na kufa papo.

Wakati tukio hilo linatendeka kulikuwa na ziara ya maofisa kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya ikijumuisha askari mgambo na polisi wakati wakitoka kwenye zoezi la udhibiti na ufuatiliaji wa mifugo katika Bonde la Hifadhi Mto wa Kilombero.

Hayo ni baadhi ya matukio yaliyowahi kutokea yakihusisha moja kwa moja kwa watu kupoteza maisha na ardhi ikiwa chanzo kikuu na unaweza kuona viongozi kukosa sifa za uongozi katika kutumia jamii ambayo moja ya sifa ya kiongozi bora ni kuzifanyia kazi taarifa za kiintelijinsia zinazoweza kuzimwa kabla ya kuleta madhara upande mwingine.

Hivi karibuni imeripotiwa kuwapo kwa taarifa za wafugaji wa Kijiji cha Ipera Asilia, Kata ya Itete Njiwa wilayani humo katika eneo lililotengwa kwa ajili ya malishao kuvamiwa na wakulima na kufanya shughuli za kilimo.

Kutokana na hali hiyo tayari imeripotiwa kuwapo kwa mgogoro baina ya jamii ya wafugaji na wakulima wanaodaiwa kuvamia eneo hilo la malisho huku ikidaiwa kusababisha mfugaji mmoja kupoteza maisha.

Mmoja wa wazee wa Kijiji cha Ipera Asilia, Mipawa Chibubu Jilala (80) amewahi kunukuliwa akiitaka Serikali ya Mkoa wa Morogoro kuingilia kati kwa kuwaondoa wakulima waliovamia maeneo yaliyotengwa kwa malisho ya mifugo.

Katika mazingira hayo yanayotajwa kuwa na mgogoro tayari mmoja wa vijana waliokuwa wanachunga mifugo na kuweka kambi eneo la malisho la Ikotakota alivamiwa usiku na watu wasiojulikana na kufyatuliwa risasi na kufa.

Jilungu Ilindilo (30) alifariki dunia kwa kupigwa risasi tumboni saa 5 usiku na mtoto aliyekuwa na Jilala Jidasega (7) alijeruhiwa begani katika tukio hilo lililotokea April 18, mwaka jana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ipera Asilia, Selesus Likondeni (52) alithibitisha kutokea tukio hilo na chanzo kikielezwa kuwa ni kuwapo kwa mgogoro wa ardhi baina ya wafugaji na wakulima wa vijijini jirani ambao bado anadai haujapatiwa ufumbuzi wa kutosha.

Hii ni baadhi ya mifano kutoka Wilaya ya Malinyi, lakini migogoro kama hii ipo Wilaya za Mvomero, Kilosa na Morogoro Vijijini. Msimu wa kilimo haupiti katika maeneo hayo bila mkulima au mfugaji kufariki dunia kutokana na migogoro ya ardhi.

Ni Serikali pekee inayoweza kusimamisha mauaji hayo ambayo sasa yameanza kuwatia hofu wananchi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: