Mwanza. Mustafa Hussein (18) kutoka Mkoa wa Mara amejinyakulia zawadi ya pikipiki aina ya Toyo yenye thamani ya Sh2 milioni baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika fainali za kusoma Quran zilizofanyika jijini Mwanza.
Mustapha alipata zawadi hiyo baada kuhifadhi na kusoma kwa ufasaha Juzuu 30 katika mashindano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Msikiti na kushindana na vijana 25 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mshindi wa pili kwa kusoma Juzuu 30 ni Waziri Ramadhan wa Mwanza aliyejishinda Sh500,000, wakati nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Mukhsin Yunusu kutok Kagera aliyezawadiwa Sh450,000.
Mshindi wa Juzuu tano alikuwa Abdul Rashid kutoka Mara aliyejizolea kitita cha Sh200,000 na kombe.
Mshindi wa pili alikuwa ni Mahir Sultan wa Mwanza aliyepokea Sh150,000 na wa tatu ni Sadick Mudy kutoka Shinyanga, aliyepewa Sh100,000, huku Juma Hamis wa Mwanza akinyakua Sh300,000 baada ya kuibuka mshindi katika Juzuu 10.
Mshindi wa pili katika Juzuu 10 alikuwa Amir Hussein wa Mara aliyezawadiwa Sh250,000 na wa tatu ni Tawaqal Omary kutoka Kagera aliyeondoka na Sh200,000.
Bingwa wa kusoma Juzuu 20 alikuwa ni Farouk Swidiq kutoka Shinyanga aliyepata Sh450,000 na kombe, mshindi wa pili Ramadhan Rajab wa Mwanza aliondoka na Sh400,000, huku Abdulrahaman Hussein wa Mara akinyakua Sh350, 000 kwa kushika nafasi ya tatu.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Islamic Yatima, Sheikh Jabir Katura aliwataka Waislamu kuwapa watoto wao elimu ya duniani na akhera ili kuandaa jamii yenye wasomi wenye hofu na misingi ya dini.
“Wazazi na walezi wa Kiislamu hakikisheni mnapeleka watoto kujifunza elimu ya dini, msiishie kuwapeleka kwenye elimu ya dunia mkasahau akhera,” alisema Sheikh Katura.
Meneja wa Kituo cha Televisheni cha Mahaasin, Hajj Bajbel waliokuwa waandaaji wa mashindano hayo alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana, mashindano hayo bado yanakabiliwa na changamoto ya kukosa wadhamini wa kutoa zawadi kwa washindi.CHANZO:MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment