BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAJANGA MATANO YATAYOZIKUMBA MAKAMPUNI YA SIMU, NI KUPATA HASARA BAADA YA KUZIMWA KWA SIMU FEKI TANZANIA





MTAALAMU wa masuala ya mawasiliano ya simu za kiganjani, Kelvin Twissa jana aliiambia Nipashe kuwa kuzimwa kwa simu feki kutaathiri mapato ya kampuni za mawasiliano ya simu kwa takriban asilimia 10.

Kupungua kwa mapato ya kampuni za simu ni kutokana na kushuka kwa idadi ya simu zinazopigwa na wingi wa miamala ya kutuma na kupokea pesa, ni moja kati ya majanga matano ambayo yataendana na zoezi la uzimaji simu feki, ambalo lilifanyika usiku wa kuamkia leo.

Twissa ambaye aliwahi kushika nyadhifa kubwa za uongozi katika kampuni tatu kubwa za mawasiliano ya simu za mkononi za Vodacom, Tigo na Airtel, alisema katika tathmini waliyoifanya miezi miwili iliyopita, waliibaini kuwa uamuzi huo wa serikali kuzima simu feki utapunguza mapato ya kampuni za simu kwa kiasi hicho.

“Kampeni za kampuni za mawasiliano ya simu kugawa simu kwa wateja wenye simu feki kumesaidia kupunguza hasara ambayo kampuni za simu zingepata kutokana na uamuzi wa serikali kuzima simu feki,” alisema.

“Katika tathimini tuliyofanya miezi miwili iliyopita, ilibainika kuwa simu feki zilikuwa zimebaki takriban asilimia 10 ya simu zote zilizopo nchini,” alisema Twissa. “TCRA wanaweza kutoa takwimu zaidi katika hili.”

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano, aliiambia Nipashe jana kuwa kuzimwa kwa simu feki kutapunguza mapato ya kampuni hiyo, lakini hakuwa tayari kuanika kwa kiasi gani uamuzi huo wa serikali utawaathiri kiuchumi.

“Wananchi watakosa mawasiliano na taarifa muhimu, mapato yatapungua mpaka pale wateja watakapoweza kupata simu halisia,” alisema Singano.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia, aliliambia gazeti hili jana jioni kuwa kuzimwa kwa simu feki kutakuwa na athari kwa kampuni hiyo kiuchumi kutokana na baadhi ya wateja wao ambao simu zao zitazimwa, kushindwa kuwasiliana na hata kufanya miamala ya simu.Aidha, uzimaji simu feki unatarajiwa kupunguza mapato ya seikali kwa njia ya kodi.

Akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016-17 katikati ya wiki iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema katika mwaka ujao wa fedha, serikali itatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma wa simu katika kutuma na kupokea fedha badala ya ushuru huo kutozwa tu kwenye kutuma fedha pekee.

Dk. Mpango alisema katika utaratibu wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa huduma zimetumia mwanya kwa kuhamishia sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.

“Hatua hizi za ushuru wa bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha Sh. bilioni 63.639,” alisema Dk. Mpango.

Majanga mengine ni pamoja na kuzagaa kwa taka za sumu mitaani katika simu feki ambazo wamiliki hawakuwa tayari kuziacha kwenye kampuni za simu na maduka makubwa hata baada ya kuzibadilisha jana, kwa mujibu wa uchunguzi wa Nipashe.

Mfanyabiashara mmoja katika duka la moja kubwa la simu lililopo Posta ambaye hakupenda jina lake litajwe katika gazeti, alisema wamepewa maagizo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), wateja waache simu zao katika maduka hayo pale wanapobaini kwamba ni feki na kwamba wameahidi kuwapa vyombo ambavyo vitakuwa vinatumika kuzihifadhi.Pamoja na maagizo hayo, alisema wateja bado hawakubali kuacha simu zao.

Zoezi la uzimaji simu feki pia limeacha kilio kwa wafanyabiashara ya simu kwani wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema kwa miezi miwili hadi mitatu iliyopita hapakuwa na wanunuzi wa kutosha katika biashara hiyo hivyo kuwapo kwa malimbikizo ya mzigo ambao bado haujauzika.

“Hasara tuliyopata kwa awamu hii ni kubwa na haijawahi kutokea,” alisema Frank Mwambona ambaye anauza simu ndani ya jengo la Mobile Plaza, lililoko Kariakoo.

"Kwa kipindi cha nyuma ulikuwa ukileta stock (mzigo) la simu halimalizi hata kipindi cha wiki moja, lakini huwezi amini tangu tulivyoleta limekaa kama lilivyo, ni hasara ambayo hatujawahi kupata.” 

Katika maduka ya simu hizo eneo la Posta mpya, karibu maduka yote ambayo gazeti hili lilitembelea wauzaji walilalamika kuwa biashara hiyo imekata na wanachosubiri ni kuzimwa kwa simu feki ili waone kama biashara inaweza kurejea katika hali ya kawaida.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: