Na Lilian Lucas, Morogoro.
Waziri wa Maliasili na Utalii,Profesa Jummane Maghembe amesema wizara yake imechukua hatua mathubuti na kufanya utafiti ambao umegundua baadhi ya watu wakiwemo wafugaji kufuga ndani ya hifadhi na kutoa taarifa kwa majangili mahali wanyamapori walipo wakiwemo Tembo na Nyati.
Profesa Maghembe pia amesema maeneo ya vijijini hasa vile vinavyopakana na hifadhi watu wake wamekuwa wakifanya biashara na kukodishwa kwa ajili ya kuuwa tembo jambo alilolikemea vikali.
Alisema hayo wakati akifungua mkutano wa watendaji wakuu wa wizara ya maliasili na utalii unaofanyika mjini Morogoro kwa siku mbili.
Waziri huyo wakati akiyasema hayo amezitangaza idara,Mamlaka na Hifadhi zinazojishughulisha na misitu na maliasili kuwa ni Jeshi la kulinda maliasili litakalojulikana kama Jeshi USU.
Alisema kuwa tayari mpango wa kuligeuza idara hizo umeanza kwa Shirika la Hifadhi za Taifa(Tanapa) baada ya watendaji wake wakuu na askari wa shirika hilo kupatiwa mafunzo ya kijeshi kuhusu kulinda hifadhi zote za Taifa kutokana na kuwepo kwa uvamizi wa idadi kubwa ya majangili.
Waziri Profesa Maghembe,alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016 hadi 2017 Wakala wa misitu Tanzania(TFS) na kuundwa bodi yake itageuzwa kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Misitu na baadaye kugeuzwa kuwa Jeshi la Usu litakalokuwa na jukumu la kulinda hifadhi za misitu za Taifa.
Profesa Maghembe pia amekemea vikali vitendo vya baadhi ya Watendaji wa Wizara hiyo na idara zake kuwa ni chanzo cha kufanya biashara na kuruhusu wananchi kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo uchomaji wa mikaa,ungizaji wa mifugo,kilimo ,ukataji wa magogo na uchimbaji wa madini.
Alisema kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikichangia uhalibifu mkubwa wa hifadhi hizo pamoja na kukaribisha majangili kufanya vitendo vya ujangili ndani ya Hifadhi hizo na kupekea kuwawa kwa wanyamapori wakiwemo tembo na nyati.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge,Ardhi ,Maliasili na Utalii,Mhandisi Atashasta Nditiye,alisema sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uvamizi wa mifugo katika Hifadhi,ujenzi wa makazi katika hifadhi na migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Aliwataka watendaji hao wa Wizara kufanya kazi kwa maelewano huku akionya baadhi ya watendaji wanaoikimbia kamati hiyo inapokwenda kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali kuacha kufanya hivyo na badala yake kujenga urafiki na kamati hiyo.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Meja Jenerali Gaudence Milanzi,alisema kuwa wamepokea changamoto kutoka kwa Wabunge katika bajeti ya wizara hiyo hivyo wamejipanga kuhakikisha wanatekeleza kulingana na maagizo yatakayotolewa na Waziri.
0 comments:
Post a Comment