BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WALIOZIMIWA SIMU FEKI NA TCRA WAVAMIA KAMPUNI ZA SIMU

 
WAKATI baadhi ya kampuni za simu zikikiri kupata hasara baada ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuzima simu bandia, idadi kubwa ya waliokumbwa na kadhia hiyo wamemiminika kwenye makampuni hayo kununua bando ili kupata simu halisi bure.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando, alisema ni kweli wamepata hasara lakini mwitikio wa wateja waliokumbwa na tatizo la kuzimiwa simu zao ni mkubwa na wamejitokeza kwa wingi kununua bando na kupata simu halisi za bure.

“Siwezi kukataa kwamba Airtel hatujapata hasara, hasara ipo lakini ni vigumu kuainisha ni kiasi gani, tunajua idadi ya wateja wamepungua baada ya kukubwa na tatizo hili ingawa leo (jana) kupitia ofisi zenu na wakala wetu wamemiminika kununua bando ili kupata simu za bure,” alisema.

Alisema wateja waliozimiwa simu zao wamemiminika kununua vifurushi vya Sh 22,000 na kisha kupewa simu za bure ambazo ni halisi.

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Kampuni ya simu ya Vodacom, Rosalynn Mworia, alisema kuwa, wamelazimika kuuza simu bei nafuu nchi nzima ili kuziba pengo la hasara lililotokana na wateja wao kuzimiwa simu zao.

Alisema kwa sasa ni mapema kueleza ni hasara kiasi gani waliyoipata baada ya hatua hiyo ya uzimaji wa simu feki kufanyika.

“Hasara za haraka kampuni imezipata ambazo pia zipo kwa upande wa serikali kutokana na wateja wetu kuzimiwa simu zao na kushindwa kufanya mawasiliano na kufanya miamala ya kifedha kwa sasa ni mapema kuzieleza,” alisema.

Alisema wateja waliozimiwa simu wamekuwa wakimiminika kwenye ofisi za kampuni hiyo wakitaka kupewa simu za bure kama ilivyo kwa kampuni za Tigo na Airtel.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezima simu bandia 600,000 nchi nzima.
Meneja wa Mawaliano wa TCRA, Innocent Mungi, alilieleza Nipashe jana kuwa, jumla ya IMEI laki sita ndizo zilizozimwa katika mpango wa ukomo wa simu bandia.

Alisema IMEI zilizozimwa ni zile zilizoko kwenye Modem, Tablet na simu ambazo zilihamishwa kutoka kwenye daftari jeupe kwenda daftari la kijivu kabla ya kuingizwa kwenye daftari jeusi tayari kwa kuzimwa.

“Kazi ya kuzima IMEI tuliifanya jana saa 6:00 usiku hadi saa 10:00 alfajiri kwa kushirikiana na kampuni za simu ambazo zilizima mtandao kwa IMEI bandia na hatimaye TCRA nasi tukaziingiza kwenye mfumo wa kuzizima rasmi,” alisema Mungi.

Alisema pia IMEI zilizozimwa ni zile ambazo zilitumiwa ujumbe mfupi wa maneno, kuwa simu zao ni bandia na waliohakiki na kubainisha simu zao siyo bandia hawajazimiwa.

“Kama simu ya mtu haikutumiwa ujumbe kama ni bandia hatujazizima kwa sababu leo tumepokea jumbe za watu wakisema simu zao ni bandia lakini hazijazimwa na kumbe siyo bandia na hawakujua kama siyo bandia kwa sababu hawakuhakiki,” alisema.

Mungi alisema mara baada ya kuzizima simu hizo kwa kutumia mfumo maalumu nyingine zilizima muda huo huo na nyingine zimekuwa zikiendelea kuzima taratibu kulingana na ufanyaji kazi wa mfumo.

Aidha, alisema mpango wa kutoa elimu ili watu wazime simu bandia wenyewe, ulifanikiwa kwa asilimia kubwa na kwamba hadi juzi ni asilimia 2.96 pekee ya simu bandia ndio zilisalia. 


“Tangu kutangaza kuzima simu bandia soko la simu bandia lilikuwa asimilia 30, baadae lilipungua na kufikia asilimia 18, asilimia 13 na hadi juzi siku moja kabla ya kuzima zilisalimia asilimia 2.96 pekee,” alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: