BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ZITTO KABWE WA JAKAYA KIKWETE NI ZITO KABWE WA RAIS DK JOHN MAGUFULI ?, NINI KIMEFIJICHA NDANI YAKE.


Kiongozi mkuu wa chama wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akihutubia wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho katika uwanja wa shule ya msingi Mwembesongo Manispaa ya Morogoro hivi karibuni.PICHA/MTANDA BLOG


Zitto Kabwe, mwanasiasa makini kama alivyo, mwenye upeo kama alivyo, mjenga hoja kama alivyo. Ni kipenzi cha mashabiki wengi wa siasa. Mimi ni mmojawapo. Ziwe nyakati zile amevaa kombati ya Chadema au nyakati hizi akiwa na suti za ACT Wazalendo. Zitto ana mvuto anapojenga hoja. Ana akili.

Nani hamuhitaji Zitto katika siasa za leo? Hakuna. Aliondolewa uanachama wa Chadema baada ya kushindwa kesi Mahakama Kuu asubuhi ya Machi 10, 2015 huku wanachama wengi wa kawaida wa chama hicho na wapenda harakati wa siasa za upinzani wakitamani aendelee kuwapo katika chama hicho.


Hata hivyo, kutoaminiana kati yake na wakuu wenzake wa Chadema kulikuwa kumefika katika hatua ya juu kabisa. Ilikuwa ni kesi ya Panya na Paka. Maisha yasingeweza kuendelea kuwa yaleyale tena, hata kama wangeamua kuwa wanafiki na kumaliza mambo nje ya ukumbi wa sheria.

Chadema walikuwa wanaamini Zitto alikuwa anawauza. Waliamini anawauza kwa CCM. Anawauza kwa Mwenyekiti wa chama tawala, Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa na cheo kingine kikubwa zaidi nchini, Rais. Inasemekana alikuwa rafiki yake wa karibu.

Waliamini kuwa Zitto alikuwa anauza siri zao kwa dola iliyopita. Na hata kabla mtu anayeitwa Edward Lowassa hajavua nguo za kijani za CCM, waliamini kuwa Zitto alikuwa rafiki mkubwa wa mtandao wake, ambao nyakati hizo ulikuwa tishio kwa Chadema.

Msumari wa mwisho katika hisia za mabosi wa Chadema dhidi ya Zitto licha ya kuwa tayari walikuwa wamemuondoa kwenye chama ni pale alipogoma kutoka kuambatana nao nje kususia hotuba ya Rais mpya, John Magufuli wakati akifungua Bunge. Ilionekana Zitto angeendelea kuwa mpinzani wa wapinzani.

Magufuli alisikika akimsifia Zitto kuwa alikuwa mpinzani halisi. Kamera za TBC zilimuonyesha Zitto mwenyewe akitabasamu. Kila kitu kilikuwa safi. Lakini ghafla kila kitu kimebadilika. Maisha ya Zitto katika siasa kwa sasa yapo matatani, kama yalivyo kwa watu wa Chadema ambao wamezoea maisha ya kuwindana na Serikali tangu waliposhika nafasi ya kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Kuanzia Magufuli alipotoa mguu wake bungeni na kuanza kazi yake ya urais, Zitto akiwa katika ubora wake wa kuchambua hoja kwa maneno mafupi amekuwa akituma mitandaoni ujumbe mfupi kukosoa vikali hiki na kile katika maamuzi ya moja kwa moja ya Rais Magufuli. Anapozungumza Zitto tunapaswa kusikiliza.

Katika utawala uliopita, Zitto aliibua mengi ambayo yalimpatia umaarufu mkubwa, lakini akipitia zaidi katika mgongo wa Bunge, mikataba ya kifisadi na mengineyo. Wakati fulani alikuwa katika korido za Bunge akikusanya saini za wabunge wa vyama vyote kwa ajili ya kumuondoa madarakani, Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda.

Hakumgusa Rais aliyepita moja kwa moja na sana sana alikuwa anaibua skendo au kujenga hoja za kumtaka Rais yule afanye mabadiliko ya hapa na hapa, au kuwataka wahusika wajiondoe katika nyadhifa zao moja kwa moja. Hakuwa mkali kwa Rais Kikwete. Kulikuwa na siri gani kati yao?

Kama ni udikteta au uminywaji wa demokrasia hata Kikwete alishutumiwa sana enzi zake. Mabomu dhidi ya Chadema yalikuwapo kama kawaida, Professa Ibrahim Lipumba naye alipigwa Mbagala. Sababu ni ile ile tu. Kuandamana bila ya kibali. Hata hivyo, hatuwezi kumchagulia Zitto marafiki.

Utawala huu, Zitto amegeuka kuwa pilipili moja kwa moja. Kwa Rais mwenyewe. Na hata utawala wenyewe umeshageuka pilipili kwake. Tayari amefungiwa bungeni. Lakini mitaani anatafutana na polisi na ameshaendesha mkutano na waandishi wa habari Jumanne akimbwatukia vikali Magufuli hata kudiriki kumuita dikteta.

Baada ya shutuma nyingi zilizoelekezwa na watu mbalimbali kwa Rais aliyepita, huku dunia ikiwa imeshazama katika masuala ya mitandao, bado Zitto hakuweza kuelekeza mashambulizi ya moja kwa moja kwa Kikwete kuliko Rais Magufuli. Kulikoni?

Na upande wa pili wa shilingi amejibu mapigo katika uzito ule ule kiasi kwamba Zitto ametwambia kuwa Magufuli alimuamrisha IGP amtie ndani wikiendi iliyopita. Kulikoni? Ile kauli ya Magufuli kuwa Zitto ndiye mpinzani mzuri, na lile tabasamu la Zitto kupokea kauli hiyo pale Dodoma vyote vimepotea.

Zitto huyu wa sasa ndiye ambaye Chadema walimuhitaji. Labda kama Magufuli angeingia madarakani baada ya Rais Benjamini Mkapa, huenda mpaka leo Zitto angekuwa Chadema. Hofu ya kwamba Zitto alikuwa anawauza katika utawala uliopita inaonekana kuzuka tena.

Si rahisi kuthibitisha sana, lakini ni wazi kwamba kihisia JK na JPM ni watu wawili wanaotofautiana katika misimamo, falsafa, na kauli za kuendesha nchi. Hata hivyo, bado unapokuwa mpinzani unaendelea kukumbana na kucha kali za Serikali tawala, hasa katika nchi za Kiafrika kama hii. 


Inakuwaje maisha yameenda kasi sana kwa Zitto? Ni kweli kwamba leo wabunge wa Ukawa watakapoamua kutoka bungeni wakati Zitto akiwa ndani ya Bunge na yeye atatoka au ataendelea kubaki kama ilivyokuwa katika utawala uliopita? Nyakati zinaendelea kutuelemea.

Kinachoonekana ni kwamba hatimaye Zitto na Chadema wamerudi kwa adui mmoja mbele yao. Adui huyo ni Serikali na Rais wake. Katika utawala uliopita maadui walikuwa wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya kutoamianiana mpaka pale Machi 10 mwaka jana ndoa yao ilipotenganishwa na mvutano wa siku nyingi.

Hata hivyo, Zitto na Chadema wamechelewesha mapambano ya harakati za kuiondoa CCM. Ni aibu. Kwa mwanasiasa mwenye kipaji, mvuto, haiba na elimu kama Zitto, ndoa yake na chama cha upinzani kilichojijenga katika kona nyingi za nchi kama Chadema ingesaidia kusogeza gurudumu mbele.

Kwa hali ilivyo sasa kila unapoona Zitto akiongea kwa furaha na Freeman Mbowe katika kamera za televisheni au picha za kurasa za mbele magazetini wakijadili harakati pamoja inakuwa sawa na kupiga hatua ishirini nyuma kisha ukapiga hatua tatu mbele ukajipongeza. 


Hata hivyo, sisi tunawatazama tu. Wenyewe wanasema ndio mchezo wa siasa ulivyo. Mwananchi wa kawaida anabaki mdomo wazi. Hata hivyo, wengine hatushangai sana. 

Mwanafalsafa mahiri wa zamani wa Italia, Niccolo Machiavelli aliwahi kutuambia ‘Politics have no relation to Morals’. Siasa hazina uhusiano na maadili ya kiutu.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: