BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MATOKEO KIDATO CHA SITA YATANGZWA, WAVULANA WAWABURUZA WASICHANA KWA UFAULU WA JUU.


Wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi Mohamed Idd (kushoto) na Mwenzake Silaji Imani wakishangilia mara baada ya kukutana jana Shule waliyosoma, Feza Boys jijini Dar es Salaam. PICHA: MPOKI BUKUKU


HATIMAYE matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka huu, yametangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), huku wahitimu takribani 71,551 wakifaulu masomo yao kati ya 73,940 waliofanya mtihani wa kumaliza kidato cha sita.

Kati ya watahiniwa hao waliofaulu, 60,407sawa na asilimia 93.13 wamefaulu alama za daraja la kwanza hadi la tatu, viwango vinavyowawezesha kuendelea na masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini pindi udahili utakapofanyika.

Hata hivyo, kwa mujibu wa tangazo la Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuhusiana na taratibu mpya za udahili wa vyuo lililotolewa katikati ya wiki na kupatikana kwenye tovuti yao, wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu na kuwa na sifa ya kudahiliwa kwa ajili ya kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali nchini wanapaswa kuwa na walau na ufaulu wa alama mbili za ‘principal’ ambazo za chini kabisa ni za wastani wa D mbili, lakini jumla ya alama hizo mbili iwe ni 4.

Kwa kawaida, ushindi wa ‘A’ katika somo huwa ni sawa na alama 5; B ni alama 4; C alama 3; D alama 2 na E ni alama 1. Kwa sababu hiyo, wanafunzi wote waliomaliza mwaka huu na matokeo yao yaliyotangazwa jana kuonyesha kuwa wamepata walau jumla ya alama 4 katika masomo yao mawili ya michepuo watakuwa wamejipatia sifa ya kudahiliwa pindi watakapoomba kujiunga katika vyuo mbalimbali.

“Hata hivyo, mbali na ufaulu wao huo, kupata au kukosa nafasi katika vyuo huchangiwa pia na mambo mengine kadhaa ikiwamo aina ya kozi ambayo mwanafunzi huomba, ushindani uliopo kwa kulinganisha na waombaji wengine katika kitivo husika na pia jumla ya nafasi zilizopo kwa kila chuo,” afisa mmoja wa TCU aliiambia Nipashe jana.

Katika matokeo yaliyotangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, ilielezwa kuwa ufaulu wa jumla wa mwaka huu ni asilimia 97.94, ukiwa umeshuka kwa asilimia 0.93 kulinganisha na mwaka jana ambapo kwa ujumla ufaulu ulikuwa ni wa asilimia 98.87.

Sambamba na hilo, ubora wa ufaulu umezidi kuimarisha kwa kuwa idadi ya watahiniwa waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu, imeongezeka kwa asilimia 3.72 kutoka asilimia 89.41 mwaka jana na kuwa asilimia 93.13 mwaka huu.

Akitangaza matokeo hayo, Dk. Msonde alisema kati ya wanafunzi hao waliofaulu, wasichana ni 26,977 sawa na asilimia 98.31 na wavulana ni 44,574, sawa na asilimia 96.73.

WALIOONGOZA KITAIFA

Dk. Msonde alimtaja mhitimu aliyeongoza kitaifa kwa upande wa masomo ya Sayansi kuwa ni Hassan Bakari Gwaay wa mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) kutoka Shule ya Sekondari Tabora Boys ya Tabora.

Aidha, alimtaja aliyeongoza katika masomo ya Biashara kuwa ni Japheti Lawrance (ECA) kutoka Shule ya Sekondari ya Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam.

Kwa masomo ya Lugha na Sanaa, Dk. Msonde alimtaja aliyeongoza kuwa ni Edith Msenga (HKL) kutoka Shule ya Sekondari St. Mary’s Mazinde Kuu mkoani Tanga.

Kwa sababu hiyo, na kwa kuzingatia tangazo la TCU, Nipashe imebaini kuwa wahitimu hao 60,407 wa madaraja ya kwanza hadi la tatu ndiyo watakaokuwa na nafasi kubwa ya kudahiliwa na kuingia katika vyuo vikuu, hasa ikiwa alama zao za ushindi wa amsomo mawili ya michepuo zitafikia kiwango cha chini kilichotajwa cha ushindi wa jumla wa walau alama 4.

Wanafunzi hao watakuwa na nafasi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu zaidi ya 50 vilivyopo nchini hivi sasa, vikiwamo vya umma vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

“Ndoto yangu ni kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili ikibidi nikasomee masuala ya mafuta na petrol… hilo ndiyo chaguo langu,” mwanafunzi kinara katika masomo ya Sayansi, Hassan Gwaay aliiambia Nipashe katika mahojiano yake maalum akiwa kwao Mirerani, mkoani Manyara jana.

Mbali na Gwaay, aliyeongoza katika orodha ya wanafunzi 10 bora wa kiume katika mchepuo wa masomo ya sayansi, wengine katika kundi lake ni Mohamed Ally wa shule ya Feza Boys, Joshua Zumba(Uwata), Ntahondi Ernest (Mzumbe), Castory Munishi (Mzumbe), Zacharia Mwaipula (Ilboru), Deogratias Mwanjamila (Mzumbe), Silaji Andrea (Feza Boys), Saidi Mussa Saidi (Kibaha) na Enock Mwambeleko wa Marian Boys.

Aidha, kwa wasichana, mbali na Magreth Kakoko wa Shule ya Sekondari Marian Girls, wengine waliong’ara katika 10 bora kwa masomo ya Sayansi ni Bertha Nguyamu (St. Mary’s), Mary Kilapilo (St. Mary’s), Regina Lugola (St. Mary’s), Nola Matolo (Feza Girls), Selina Pius (PandaHill), Queenlisajoa Olan’g (Marian Girls), Nasma Nyindo (Kilakala), Sheikha Rashid (Feza Girls) na Lilian Hema (Tabora Girls).

Katika masomo ya Biashara, mbali na Lawrance wa shule ya Tusiime, wahitimu wengine walioingia 10 bora ni Juliana Mwalupindi (Weruweru), Arnold James (Umbwe), Halima Kulava (Al-Muntaliz Islamic), Fewdrick Laizer (Jude), David Swai (St. Joseph Cathedral), Albertina Mella (Kazima), Lucy Sanga (Alpha), James Albanus (Kibaha) na Mussa Ambika (St. Joseph Cathedral).

Katika kundi la wahitimu 10 - bora wa masomo ya Sanaa ambalo linaongozwa na Edith Msenga wa St. Mary’s Mzinde Juu, wengine ni Boniphac Kajaba (Manow Lutheran), Elikana Simon (Runzewe), Emanuel Msabi (Kisimiri), Stration Ngowi (Uru Seminary), Leonce Bizimana (Milambo), Emanuel Gewe (Mpwapwa), Zuhura Abdul (Feza Girls), Shamsi Salim (Ridhwaa Seminary) na Editha Mgina wa Morogoro.

25 WAFUTIWA MATOKEO

Dk. Msonde alisema Necta, limefuta matokeo yote ya watahiniwa 25 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani hiyo.

Alisema kati yao, 21 ni watahiniwa wa shule na wanne waliobaki ni watahiniwa wa kujitegemea.
Alitaja makosa ya wanafunzi hao kuwa ni pamoja na kuingia na majibu ndani ya chumba cha mtihani na pia kupeana majibu kwa njia ya simu za mkononi.

“Wengine waliingia na simu za mkononi ndani ya chumba cha mtihani… tuliwakamata na matokeo yao yote tumeyafuta,” alisema.

Aidha, Dk. Msonde alisema wapo watahiniwa 10 wa shule ambao walishindwa kufanya baadhi ya mitihani yao kutokana na matatizo ya kiafya na hivyo matokeo yao yamezuiliwa na kupewa fursa ya kumalizia mitihani hiyo Mei mwakani.

Alisema watahiniwa wengine 36 wa shule walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani ya masomo yote, hivyo nao wamepatiwa fursa ya kurudia mitihani hiyo Mei mwakani.

SHULE KUMI BORA

Dk. Msonde alisema shule kumi zilizofanya vizuri kuwa ni Kisimiri ya mkoani Arusha iliyoongoza yenye wanafunzi 63.
Shule iliyoshika nafasi ya pili ni Feza Boys ya jijini Dar es Salaam, yenye wanafunzi 91 wakati shule iliyoshika nafasi ya tatu kwa ufaulu ikiwa ni Alliance Girls ya Mwanza yenye wanafunzi 31.

Nyingine zilizoingia 10-bora na idadi ya wanafunzi wao kwenye mabano ni Feza Girls ya jijini Dar es Salaam (59), Tabora Boys ya mkoani Tabora (154), Marian Boys ya Pwani (126), Kibaha ya Pwani (165), Mzumbe ya Morogoro (119), Ilboru ya Arusha (223) na Tandahimba ya Mtwara yenye wanafunzi 49.

SHULE 10 ZA MWISHO

Aidha, katika matokeo hayo shule 10 zilizofanya vibaya katika mitihani ya mwisho ni Shule ya Mpendae (Unguja) yenye wanafunzi 100. Nyingine ziIizoshika nafasi za mkiani ni Ben Bella (Unguja) yenye wanafunzi 101, Tumekuja ya Unguja (178),

Green Bird Boys ya Kilimanjaro (37), Jang’ombe ya Unguja (46),
Kiembesamaki ya Unguja (123), Tanzania Adventist ya Arusha (65), Al-ahsan Girls ya Unguja (47), Azania ya Dar es Salaam (235) na Lumumba ya Unguja yenye wanafunzi 137. 


MATOKEO YA UALIMU
Katika matokeo ya mitihani ya ualimu ngazi ya cheti na stashahada, walimu wa ngazi ya daraja A waliofauli ni 10,9747, sawa na na asilimia 99.81 wakati walimu stashahada waliofaulu ni 337, sawa na asilimia 84.46.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: