MAUMIVU YA 18% YA MIAMALA YA BENKI KUANZA LEO RASMI.
Benki kuu ya Tanzania (BoT)
TABASAMU la wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi juu ya nafuu ya kodi ya mishahara, huenda likaondoka baada ya takribani benki zote nchini kutangaza ongezeko la asilimia 18 kwenye huduma za kuhifadhi na kutoa fedha.
Wachumi mbalimbali walisema jana kuwa mbali na wafanyakazi, ambao wataathirika na ongezeko hilo kwa sababu mishahara yao inapitia benki, pia watu wote wanaotumia benki, wakiwamo wafanyabiashara, wanafunzi na wengine wote wanaotumia huduma za kibenki, wataumia pia kwa kukatwa fedha zaidi wanapofanya miamala ya kibenki.
Walisema hali hiyo inaweza kufanya watu waamue kukaa na hela majumbani mwao, kitendo ambacho kitaongeza matukio ya uhalifu kwa majambazi kuvamia majumbani.
Ongezeko hilo limetokana na marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sura 148, yaliyotangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, alipokuwa akisoma bajeti ya serikali bungeni kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Alisema serikali inakusudia kutoza kodi ya ongezeko la thamani kwenye ada za huduma za kibenki zinazotozwa na benki zote nchini ili kupanua wigo wa kodi.
Kufuatia hali hiyo, takribani benki zote nchini zilitangaza ongezeko hilo la kodi walilosema linatokana na bajeti mpya ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/17, ambayo utekelezaji wake unaanza leo.
Katika tangazo la benki ya NMB jana, ilielezwa kuwa gharama zote za miamala na huduma za kibenki katika machapisho yaliyotolewa hapo awali zitakuwa na ongezeko la asilimia 18 ya VAT kuanzia Julai Mosi (leo).”
Pia matangazo ya benki za Standard Charterd, Akiba Commercial Bank (ACB) na CBA yalikuwa na maelezo kama lile la NMB, ingawa lenyewe lilieleza zaidi kuwa kodi hiyo haitahusu riba za mikopo.
Makato hayo yatagusa watu wengi kwani mishahara ya watumishi wa umma na ile ya wafanyakazi walioajiriwa kwenye sekta binafsi hulipwa kupitia benki mbalimbali nchini.
MAKATO MAPYA
Kwa upande wa ada ya akaunti ya benki kwa mwezi, baadhi ya taasisi hizo za kifedha humtoza kila mteja kati ya Sh. 1,500 mpaka Sh Sh. 2,000 kwa mwezi.
Kwenye upande wa miamala inayofanyika kupitia mashine za kutolea fedha (ATM), benki hutoza wastani wa Sh. 800 hadi Sh. 1,500 kutegemea na aina ya kadi ambayo mteja anaitumia.
Baada ya ongezeko la asilimia 18 ya VAT kwenye tozo za benki, gharama za kuhifadhi akaunti za mteja kwa mwezi zitakuwa kati ya Sh. 1,770 kwa mwezi mpaka Sh. 2,360.
Pia kwa watakaotumia ATM kutoa fedha, kila watakapoingiza kadi kwenye mashine na kutoa fedha, sasa watakatwa kati ya Sh. 944 mpaka 1,770 kutegemea na aina ya kati ambayo mteja anaitumia.
KUPUNGUZA PAYE
Wakati akisoma hotuba ya bajeti bungeni Juni 8, mwaka huu, Dk. Mpango alisema ili kuboresha kipato cha wafanyakazi, serikali inapunguza kodi ya mishahara (PAYE) kwa mishahara kutoka asilimia 11 hadi asilimia tisa kwa wanaostahili kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sheria.
Waziri huyo alisema watumishi wanaolipwa chini ya Sh. 170,000, walikuwa hatozwi kodi, wakati wale wenye mishahara ya zaidi ya Sh. 170,000 walikuwa wanatozwa kodi kulingana na makundi yao ya mshahara kwa mujibu wa sheria.
Kodi ya PAYE kwa watumishi hupangwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenye makundi matano ya mishahara ya chini ya Sh. 170,000 (hawalipi kodi), Sh. 170,001 hadi 360,000 (walikuwa wakitozwa asilimia 11 ya kinachozidi baada ya kutoa 170,000), wakati wenye mishahara inayozidi Sh. 360,000 hadi 540,000 walikuwa wanatozwa Sh. 20,900 jumlisha asilimia 20 ya kinachozidi baada ya kutoa 360,000.
Wenye mishahara inayozidi Sh. 540,000 hadi 720,000 walikuwa wanatozwa 56,900 jumlisha asilimia 25 ya kinachobaki baada ya kutoa Sh. 540,000, huku wale wanaolipwa zaidi ya Sh. 720,000 wakilipa Sh. 101,900 jumlisha na asilimia 30 ya kinachozidi baada ya kutoa 720,000.
PESA KUFICHWA MAJUMBANI
Profesa Lusato Kulwijira wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), alisema jana kitendo cha benki kuongeza gharama za miamala na huduma zake kitakuwa na athari kubwa kwa wananchi wanaotegemea huduma za kifedha za benki hizo.
Aidha, kutokana na kuongezeka huko kwa gharama za huduma za kibenki, msomi huyo alitahadharisha kuwa watu wengi watalazimika kuhifadhi fedha kwenye nyumba zao na kuhatarisha usalama wao.
"Ongezeko hili ni kuumiza mwananchi, hasa mwenye kipato kidogo. Maisha ya mlaji wa mwisho yatapanda sana.
Tulitegemea vitu vishuke bei, lakini kila kitu kimepanda na watu hawana fedha," alisema Profesa Kulwijira na kuongeza:
"Tunakoelekea watu wataficha fedha ndani ya nyumba zao na wataanza kuvamiwa na kuibiwa."
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi, aliliambia gazeti hili kuwa ongezeko hilo litaisaidia serikali kupata fedha na kuongeza mapato yake lakini akatahadharisha kuwa huenda watu wengi wataepuka kutumia za kibenki.
"Tutarudi kwenye 'cash economy' na kurejesha wizi wa watu kuvamiwa majumbani. Huenda watu wengi hasa wa kipato cha chini wakaachana na utaratibu wa kutumia huduma za kibenki na kuamua kutunza fedha zao wenyewe," alisema Profesa Ngowi.
Alisema kiasi kilichoongezwa na serikali kwenye mishahara ya watumishi kwa kupunguza Paye kwa asilimia mbili ni kidogo mno kulinganishwa na kodi ambazo wananchi wanaanza kutozwa leo.
"Ni kweli wamepunguza Paye hadi asilimia tisa, lakini ukienda benki na kwenye kampuni za simu, kodi ya miamala imeongezwa, ukienda kutalii, unakatwa kodi. Bajeti hii kila mtu itamwathiri kivyake," aliongeza Profesa Ngowi.NIPASHE
0 comments:
Post a Comment