MBIO ZA RAIS MAGUFULI ZAWASHINDA MAWAZIRI
WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli ikiendelea kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Imebainika kuwa baadhi ya mawaziri hawaonekani sana kwenye vyombo vya habari wakishughulikia masuala mbalimbali ya wizara zao kulinganisha na kasi waliyoanza nayo.
Aidha, uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kuhusisha kurasa nne muhimu za magazeti sita ya kila siku nchini, umeonyesha kuwa baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri hao, hadi sasa sura zao hazijawa maarufu machoni mwa wananchi walio wengi.
Umeonyesha kuwa baadhi ya mawaziri walioanza kazi kwa kasi kubwa, wakionekana kila mara kwenye vyombo vya habari kutokana na utendaji wao wa vitendo katika wizara walizopo, sasa hawaonekani mara kwa mara.
Badala yake, ni Rais Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ndiyo ambao wamekuwa wakionekana mara kwa mara.
Katika uchunguzi huo uliohusisha kipindi cha kuanzia Machi hadi Mei na kujumuisha ripoti kwenye kurasa nne muhimu za magazeti matano ya kila siku ya Nipashe, Mtanzania, Mwananchi, Uhuru na Tanzania Daima, imeonekana kuwa baadhi ya mawaziri ndiyo wanaoendeleza kasi yao na kuripotiwa zaidi kwa habari zinazohusiana na wizara zao huku wengine, hasa naibu mawaziri, wakikosekana kabisa kwenye kurasa hizo. Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri Desemba mwaka jana.
Alifanya pia mabadiliko madogo kadhaa yakiwamo ya kumtoa Mwigulu Nchemba kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kumpeleka Wizara ya Mambo ya Ndani kushika nafasi iliyoachwa wazi na Charles Kitwanga aliyeondolewa kwa ulevi.
Kwa ujumla, katika uchunguzi huo, Nipashe imebaini kuwa ni mawaziri na naibu mawaziri wachache ndiyo huonekana zaidi kwenye kurasa nne muhimu huku wengi wao wakionekana mara chache.
Kwa mfano, katika gazeti la Uhuru linalomikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ripoti zinaonyesha kuwa kipindi cha kuanzia Machi Mosi hadi Mei 31 kilihusisha ripoti za jumla ya mawaziri na naibu mawaziri 32.
Kati yao, aliyeongoza kwa kuonekana akiripotiwa mara nyingi zaidi katika kurasa nne muhimu za gazeti hilo ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliyeripotiwa mara 12 na Naibu Waziri wake, Dk. Hamis Kigwangallah aliyeripotiwa mara 11; Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe walioripotiwa mara tisa kila mmoja.
Wanaofuatia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora), George Simbachawene na Naibu Waziri wake, Suleiman Jaffo walioripotiwa mara nane kila mmoja.
Katika orodha hiyo katika gazeti la chama tawala kuanzia Machi hadi Mei, wengine walioonekana wakiripotiwa kujihusisha na masuala mbalimbali yanayohusiana na wizara zao na nafasi zao kwenye mabano ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge (mara moja); Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate Nashe (6), Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (3) na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo aliyeripotiwa mara saba.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustino Mahiga (2); Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki (4); Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani (6), Naibu Waziri wa Fedha, Ashatu Kijaji (5) na Nape Nnauye aliyeripotiwa mara 7. Hata hivyo, idadi ya namna alivyoonekana Nape haikuhusisha kurasa kuu za michezo ambako pia huripotiwa mara kwa mara.
Wengine walioonekana katika kurasa nne muhimu za gazeti la Uhuru katika kipindi hicho ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya uteuzi wake kutenguliwa, Charles Kitwanga (6); aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na sasa Mambo ya Ndnai, Mwigulu Nchemba(4); Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (3 ); Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ( 3 ),; Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage (5); na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (6).
Wengine ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi, Mawasiliano, Eng. Ediwn Ngonyani (7); Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Eng. Isack Kamwelew (2); Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Angelina Mabula (2) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussen Mwinyi (3).
Katika orodha hiyo, wamo pia Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina (2)1; Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde (2) na Waziri wa wizara hiyo, Jenista Mhagama (1); Waziri wa Elimu, Sayansi naTeknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (2); Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (4), Waziri wa Fedha, Dk. Phillip Mpango (1) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk. Abdallah Posi ( 3).
WASOMI WANENA
Wakizungumza na Nipashe kuhusiana na kupungua kwa kasi ya badhi ya mawaziri na naibu mawaziri wao kulinganisha na vile walivyoanza baada ya kuapishwa, badhi ya wasomi walisema hali hiyo inaonyesha kuwa baadhi yao walitaka kujenga misingi ya kazi kwenye wizara zao huku wengine wakidai kuwa hiyo ni dalili kuwa baadhi yao walitaka kuonyesha kuwa wankwenda na kasi ya Rais Magufuli.
Mhadhiri wa UDSM Idara ya Sayansi ya Siasa, Richard Mbunda, alisema kuwa awali, mawazi wengi walikuwa wanajituma kwa vile walitaka kuonekana kuwa wachapa kazi.
"Wengi wao ni wageni hivyo walitaka kuonyesha kuwa Rais hakukosea kuwateua,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema kwa sasa mawaziri hawaripotiwi sana kwa sababu mambo yameanza kunyooka na watu wamekuwa wawajibikaji wazuri kazini kulinganisha na hali waliyoikuta awali.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma katika Chuo cha UDSM, Dk. Bashiru Ally alisema jambo la msingi kwa mawaziri hao ni kufanyiwa tafiti kuhusiana na maagizo waliyoyatoa ili kujua kipimo chao cha utendaji kazi na siyo kuangalia ni kwa namna gani wameripotiwa kwenye vyombo vya habari.
"Unaweza kukaa kimya lakini ukawa unafanya kazi na unaweza ukawa unasikika lakini usiwe mtendaji… hapa tunachotakiwa kuangalia ni kufanyia utafiti yale maagizo yao ambayo waliyatoa awali na kuona kama utekelezaji wake umefanyika kwa kiwango gani," alisema Dk. Bashiru.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mshauri wa chama hicho, Prof. Mwesiga Baregu, alisema kupungua kwa kasi ya utendaji kwa baadhi ya mawaziri kunaashiria kuwa baadhi wanaogopa kutoa maamuzi ambayo yanaweza kutolewa muda wowote na rais.
Mhadhiri Mwandamizi katika Saikolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Kitila Mkumbo, alisema kilichopo sasa kwa baadhi ya mawaziri ni utendaji wa kazi zaidi kwa vitendo na siyo kujionyesha na kujitangaza kama ilivyokuwa awali na ndiyo maana hawaonekani sana.
0 comments:
Post a Comment