Watoto hawa wanachanganyikiwa zaidi kuingia katika mazingira ya uhuru wa kupindukia unaoambatana na kuanza kupewa fedha nyingi za mikopo ya elimu ya elimu ya juu ili kujikimu na kugharamia mafunzo wakiwa vyuo vikuu bila kupata muongozo wala usimamizi.
Hali hii inaelekeza taasisi hizi kuwa na uangalizi zaidi kwani ni maeneo ambayo watoto wanaweza kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU), mabinti kupata na kutoa mimba, wasomi hawa wadogo kushiriki kwenye uhalifu iwapo vyuo vitaendelea kubaki kama vilivyo, bila kuandaa taratibu za kuhamasisha na kuwafunza maadili, kudhibiti mihemko na hata jinsi ya kupanga bajeti ya mkopo wanaopokea.
Makala hii inatizama jinsi vyuo vikuu vilivyo ‘hatari’ kwa mabinti ambao wanapata mimba zisizohitajika na kulazimika kuzitoa, lakini pia, wakiathirika na VVU pamoja na kuchanganyikiwa kisaikolojia na kitaaluma.
Katika mahojiano na baadhi ya wanafunzi sichana wanakiri kuwa wanakabiliwa na changamoto hii kwa kuwa hakuna elimu ya ujinsia, uzazi salama pamoja na maambukizi ya VVU wanayopewa wakijiunga na vyuo, hali inayowafanya kutumbukia kwenye kwenye maisha ya anasa kama ngobo na kupata ujauzito, wakati mwingine kutoa mimba kusiko salama.
Haya ni baadhi ya mambo yanayoibuka wakati wa mahoajiano baina ya Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi (Doso) ,wanafunzi , na wataalamu wa afya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kaimu Mratibu wa Masuala ya Afya kwenye Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi, Nashi Mnzava, kwenye mazungumzo hayo, yaliyolenga kufahamu iwapo kuna program za kuwaelimisha mabinti wanapoingia shuleni hapo kuhusu VVU , ujauzito na utoaji mimba usio salama, mtaalam huyu, anasema kwa sasa hakuna mikakati ya kushughulikia changamoto hiyo.
Mnzava anakiri kuwa wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wameambukizwa magonjwa na wengine wamo kwenye hatari ya kuambukizwa VVU na kwamba mabinti ndiyo wako kwenye kitisho zaidi kwani wanapata mimba zisizotarajiwa na kuzitoa hata bila usalama na kuathirika zaidi kitaalamu na kisaikolojia kuliko wanaume.
Anaeleza kuwa katika ofisi ya mshauri inayohusika na ustawi wa wanafunzi, wamegundua changamoto nyingi za mabinti hao wasomi. Wanazibaini wakati wa kushughulikia matatizo ya wasichana wajawazito ambao wanaripoti masuala ya afya pamoja na ujauzito kwenye ofisi ya Mshauri.
Anadokeza kuwa mara nyingi wanaripoti matatizo hayo ili kupewa nafasi nyingine iwapo watashindwa kufanya vizuri kwenye taalamu kutokana na matatizo ya ujauzito na uzazi, hivyo chuo kiwafikirie na kuwapa fursa nyingine ili kukamilisha masomo yao.
Mnzava anasema mabinti wengi wakiingia chuoni mwaka wa kwanza wanapata ujauzito. Kwa wale ambao wameamua kupata watoto, hufikisha taarifa kwenye ofisi hiyo ili kuomba msaada inapobidi.
Anatoa mfano kuwa mwaka huu wa masomo ulioanza Novemba mwaka jana umeshuhudia wanafunzi wa 20 wakiripoti kuwa wajawazito Januari mwaka huu.
“Ilipofika Februari wanafunzi saba wamefika kutoa taarifa kuwa ni wajawazito, Mwezi Mach walikuwa watatu, April wako 11 na Mei walikuwa 12. Hawa ni wale waliojitokeza kwenye Ofisi ya mshauri , wapo wengine ambao sina taarifa zao.” Anadokeza.
Anasema hata hivyo, mabinti hawa wanakuja peke yao hawaripoti habari za wenza wao na kikubwa kinachowafanya wajisalimishe ni kuepusha uwezekano wa kukwama kimasomo kutokana na ama kujifungua au kupata matatizo ya ujauzito.
ATHARI
Mabinti wanasema kuwa wanapojifungua hurudi kuendelea na masomo na hawana muda wa kupumzika wala kuwa pamoja na watoto wao wachanga. Wanasema hawafikishi siku 14.
Wengi hawachukui likizo ya uzazi ya miezi mitatu wala hawana lishe bora jambo wanaloeleza kuwaathiri mama pamoja na mtoto.
MAONI YA WANAFUNZI
Mmoja wa wanafunzi wa kiume anayesoma kozi ya uchumi mwaka wa pili, (jina linahifadhiwa) anasema:“Unapoingia chuo kikuu na kupokea posho za kujikimu, nyingine kwa ajili ya malazi na vitabu, unachanganyikiwa.
Kwa sababu umepata ‘mahela meng’, pia uko huru kupindukia huna mzazi wala mtu anayekuona unamalizika.”
“Haya ni mambo ambayo yanatufanya wanafunzi kutumbukia kwenye vitendo vya anasa kama kujamiiana ovyo, ulevi na kwenda kwenye muziki na hata kuharibikiwa.”
Anasema kitendo cha kushika bulungutu ambalo chuoni hapo huitwa ‘bumu’ kinasababisha wasomi hao wadogo kuchanganyikiwa na kujiona wako juu ya mwezi.
Wengine wanatumia sana vilevi, wapo wanaotumbukia kwenye ngono zisizo salama na kuambukizwa magonjwa kama VVU.
Kwa upande wa wasichana, ambao majina pia yanahifadhiwa wanasema, mara nyingine mabinti hutegemea kuwa wakifika vyuo vikuu ndilo eneo wanapoweza kupata waume.
“Unajaribu bahati yako lakini unaishia kupata mimba ya mwanafunzi mwenzako. Mwingine anakuacha, unaamua kupata mtoto ama kuchukua hatua nyingine ndiyo maana zinatolewa ovyo.”
Anaeleza zaidi kuwa kwa vile wana fedha au ‘bumu’ hawana hofu ya kupata mimba kwa vile wanajiamini kuwa watazitoa iwapo wenza watawakataa. Licha ya kwamba wanafunzi wengi ni wadogo wenye miaka kati ya 17 na 21 wanalazimika kushiriki utoaji mimba wakati mwingine usio salama.
“Msichana ana bumu kama Shilingi 600,000 anaweza kutumia Shilingi 50,000 kuondokana na mimba hiyo “ anaeleza binti huyo anayesoma kozi ya shahada ya Sanaa na Ualimu.
Anasema mara nyingi utoaji mimba hufanyika nje ya chuo na siyo kwenye kituo cha afya kwa vile huko siri zinaweza kuvuja na hatua zikachukuliwa dhidi ya wahusika.
Wasichana wanapoulizwa sababu za kufanya ngono zisizo salama wanaeleza kuwa mila na desturi na mienendo ya baadhi yao husababisha kuathirika kwa vile wamezoea kujifanya kuwa hawafahamu jambo lolote kuhusu ngono na kutii kila wanachoelekezwa na wanaume.
“Wanajifanya wenyenyekevu kwa vile wanakuja na ajenda ya kuolewa na wanajitahidi kuficha makucha wasionyeshe ukweli…”
Katika taasisi za elimu mara nyingi wanafunzi wanapewa wiki nzima ya mafunzo ya kufahamu mazingira ya shule pamoja na kupewa uzoefu na kanuni za kusoma, kuishi, kutumia huduma za chuo kama maktaba na mambo mengine ya kijamii.
Wiki hiyo ambayo kitaalamu huitwa ‘orientation program,’ huwaalika wataalamu wengi kuanzia wanataalamu na watumishi wengine ambao huwaelezea wanafunzi masuala mengi yanayowazunguka kama afya na suala VVU.
Hata hivyo, mara nyingi mabinti hawapewi elimu mahususi kuhusu suala la afya ya uzazi, mimba na utoaji mimba usio salama. Katika taasisi hizo kisa utoaji mimba ni jambo lisilo zungumzwa kwenye ‘program ya orientation’, anaongeza, Mnzava.
Lakini pia , Dk. Stephene Masule, ambaye ni daktari katika kituo cha afya cha UDSM anasema licha ya kwamba ni suala linalofanyika na limekuwa na athari kama vifo hakuna anayelisema.
Upataji na utoaji mimba ni kitu kisichozungumzwa kimeendelea kuwa mwiko jambo ambalo Mnzava na Masule waona linahitaji kuongezewa msukumo na kuendeleza uhamasishaji wa maadili na ulinzi wa maisha ya watoto hawa.
Licha ya kwamba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kila wakati Makamu wa Rais wa Chama Cha Wanafunzi (Daruso) ni mwanamke, suala la mimba na utoaji halizungumziki, hivyo wasichana kuendelea kuishi na changamoto hiyo.
Kwa jinsi ambavyo jitihada zinafanyika kuhakikisha kuwa idadi ya wanawake inaongezeka vyuoni ni vyema pia jitihada zikafanywa kuwapa mabinti nasaha kuhusu maisha mapya vyuoni yenye uhuru kupindukia, yasiyo na uangalizi wa wazazi au walezi.
Waelezwe pia kuhusu uwezekano wa kuambukizwa VVU, kupata ujauzito usiotarajiwa na wakati mwingine utoaji mimba usio salama unaoweza kuwaua na kuwavurugia masomo.
Suala la maambukizi yaVVU kwa mabinti hawa ambao ni wageni kwenye mahusiano na maisha ya kujitegemea linahitajika pia kupewa nafasi ili kuwasaidia kwa vile vyuoni hakuna sheria na kila mmoja anakwenda kama anavyojisikia.
Dk. Masule, anashauri kuwa vyuo vikuu vinahitajika kuwa na sheria ndogo ndogo za kudhibiti nidhamu na visiachwe kuwa maeneo yenye uhuru kupindukia.
Anataka kuwe na taratibu za kuwafanya wanafunzi kuwa na kazi nyingi za kufanya badala ya kuwaacha kwani ukibanwa na kazi za taaluma utakuwa huna muda wa ziada.
Mnzava anaeleza kuwa akiangalia takwimu za mimba na ujauzito, idadi kubwa ya wanaopata ujauzito ni wanafunzi wa kozi za sanaa lakini si wahandisi, sayansi wala sheria jambo linaloonyesha kuwa ugumu wa kozi na wingi wa kazi za kitaaluma unaweza kutumiwa kudhibiti nidhamu vyuoni.
Pengine ni wakati wa kuwashirikisha wazazi na walezi wa wanavyuo vikuu ili kusaidia juhudi za kuwa na vizazi salama vya wasomi.Nipashe

0 comments:
Post a Comment