BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAZIRI ALIYETIMULIWA UAZIRI KWA ULEVI BUNGENI NA RAIS MAGUFULI AKANA MCHANA KWEUPE AKIDAI AMESINGIZIWA TU.

 
KWA mara ya kwanza aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amefunguka juu ya kutimuliwa kwake kwa tuhuma za ulevi kwa kudai kuwa amesingiziwa.

Kitwanga, ambaye ni Mbunge wa Misungwi (CCM), aliteuliwa kushika wadhifa huo, Desemba 10, mwaka jana alitimuliwa kwa kosa la ulevi, Mei 20, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Misungwi mkoani Mwanza jana, Kitwanga alidai kuwa tuhuma za ulevi ambazo zilisababisha ‘atumbuliwe’ cheo chake, zilikuwa za uzushi ingawa hakufafanua zaidi. 


Kitwanga, hata hivyo, aliongeza kuwa tuhuma hizo za ulevi haziwezi kumkatisha tamaa kwenye shughuli zake za kisiasa.

KITWANGA APINGANA NA IKULU

Kauli hiyo ya Kitwanga ni kinyume cha taarifa ya Ikulu iliyotolewa Mei 20, mwaka huu kuzungumzia hatua ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wake, ambayo ilieleza wazi kuwa aliondolewa wadhifa wake huo kwa kosa la ulevi.

“Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mheshimiwa Charles Kitwanga kufuatia kitendo chake cha kuingia bungeni na kujibu swali lililohusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa amelewa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Ikulu juu ya kutenguliwa kwa Kitwanga na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.

Kitwanga alipatwa na mkasa huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema) ambalo liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema) .

KITWANGA ALIVYOBAINIKA AMELEWA BUNGENI
Kitwanga alidhihirika kuwa amelewa kufuatia kauli alizotoa wakati akijibu swali la nyongeza, Kiwanga alihoji Wilaya ya Kilombero ina miaka 55 lakini polisi hawana nyumba na matokeo yake wamepanga kwenye Jimbo la Mlimba ambako wanaishi kwenye nyumba za Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), hivyo serikali ipewe miaka mingapi kujenga nyumba na vituo vya polisi. Kitwanga alijibu:

“Kwani wewe una miaka mingapi? Usiulize miaka ya kujenga nyumba za Polisi na vituo. Amini tutajenga tu. Halafu wewe ni rafiki yangu lazima nikujibu hivyo.”

KUITWA NA WAZIRI MKUU
Baada ya hali hiyo kutokea kwenye kipindi cha Maswali na Majibu bungeni asubuhi ya Mei 20, Kitwanga aliitwa ofisini kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwemo bungeni pia ingawa mazungumzo hayakujulikana yalihusu nini.

Hata hivyo, baada ya mazungumzo yale, Ikulu ilitoa taarifa baadae usiku siku hiyo, juu ya Kitwanga kutenguliwa wadhifa wake.

MBUNGE WENZAKE WALIVYOMSIHI ASIINGIE BUNGENI
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa alikaririwa na gazeti hili Mei 21, mwaka huu akisema alijitahidi kumzuia Kitwanga kuingia kwenye ukumbi wa Bunge na badala yake kumtaka kuondoka kabisa eneo hilo la Bunge, lakini juhudi zake hazikuzaa matunda.

Alisema yeye (Ndasa) alimuona Kitwanga ana kila dalili kuwa amelewa na ndiyo maana alijaribu kumsihi asiingie bungeni, lakini hakuwa tayari baada ya kusisitiza kuwa “yuko sawa kabisa” Alisema alimuuliza Kitwanga kwa lugha ya Kisukuma;

“Ole sawa ielelo?" akimaanisha “uko sawa leo”, naye akamjibu pia kwa lugha ya Kisukuma:

“Nale sawa gete” akimaanisha yuko sawa kabisa. Ndassa alisema pia alimfuata baada ya kipindi cha asubuhi cha bunge siku hiyo lakini Kitwanga alimkimbia na kumsihi dereva wake amwondoe kwenye eneo hilo.

KITWANGA AKANA KUHUSIKA NA SUALA LA LUGUMI
Pia Kitwanga amekanusha kuhusika na kashfa ya ununuzi wa mashine za kuchukulia alama za vidole inayohusisha Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises.

Kitwanga alisema amevumilia kuhusiana na kashfa hiyo iliyochunguzwa na Bunge, hivyo kwa sasa ameamua alitolee ufafanuzi na Watanzania waliokuwa wakifuatilia waweze kutambua ukweli.

Kitwanga alisema kwa sasa hafahamu lolote kuhusiana na kampuni ya Lugumi, anashangaa jinsi wananchi wanavyopotoshwa kuhusiana na suala hilo, ingawa alikiri ni mwanzilishi wa kampuni ya Infosys.

Alisema kampuni ya Infosys ni kampuni ambayo alikuwa na hisa ya asilimia 30, lakini alijitoa mwaka 2010 kisha kumkabidhii mtoto wake, Lubango Kitwanga, hisa zake zote. 


Aidha, alisema kampuni ya Lugumi iliingia mkataba na kampuni ya Del ya Marekani ili kununua mashine zilizotakiwa kufungwa vituo vya polisi nchini kote, lakini walipohitaji wa kuzifunga waliamua kuingia mkataba na kampuni ya Infosys.

Hata hivyo, alisema kampuni ya Infosys haikuwa na uhusiano na Jeshi la Polisi wala mtu mwingine tofauti na Del ambayo ni kampuni namba moja duniani.

"Niseme wazi, toka 2010 nilijitoa katika Kampuni ya Infosys na hisa zangu zote nilimkabidhi mtoto wangu Lubango (Kitwanga) ambaye kwa sasa yupo Afrika Kusini, hivyo kama kuna lolote aulizwe yeye," alisema Kitwanga, ambaye pia alitoa msaada magodoro 150, mashine ya kuchomelea, kompressa moja na vyerehani 10 alivyovikabidhi kwa vikundi mbalimbali.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: