YES HII NDIO TANZANIA ! MUHAMED MURTAZA ALLI AMEDAKWA KWA TUHUMA NZITO ZA KUIBIA SERIKALI SH7 MIL KWA SAA MOJA
MOHAMED Murtaza Yusuph Alli ni mtu aliye katikati ya tuhuma nzito zaidi za ufisadi kuwahi kutokea nchini, na swali ambalo Watanzania wengi wanajiuliza ni mtu mmoja aliwezaje kufanikisha wizi wa kati ya Sh. milioni saba mpaka nane za kodi kwa dakika?
Kwa mujibu wa Rais John Magufuli, mtandao wa Alli unatuhumiwa kuiibia serikali kati ya Sh. milioni saba mpaka nane kwa dakika, kwa kutumia mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFDs).
Rais alibainisha mtandao huo wa kifisadi unajumuisha wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
Alibainisha hilo Jumatano katika hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa wapya watatu, na ulaji wa viapo vya uadilifu vya Wakuu wa Wilaya 139 aliowateua Jumapili iliyopita.
Ingawa Rais Magufuli hakutaja jina la Alli wakati akitoboa kuwapo kwa ufisadi huo, juzi Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kamishna Valentino Mlowola alisema ndiye kinara wa mtandao uliokuwa ukiiba mapato ya serikali kwa kiwango hicho cha kutisha.
Kufuatia kubainika kwa wizi huo na kukamatwa kwa Alli ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya uarabuni, Takukuru imesema inachunguza pia kampuni 300 zilizokuwa zikishirikiana naye, na kwamba nne tayari zimebainika kukwepa kodi ya Sh. bilioni 30.
Zimetakiwa kuzilipa fedha hizo mpaka ifikapo Julai 7.
ALIZALISHA RISITI
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar ea salaam juzi, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata alisema kwa tumumia mashine za EFDs zilizo nje ya mfumo wa Mamlaka yake, mtuhumiwa huyo alizalisha risiti za mazuzo na kuziuza kwa makampuni hayo 300 bila yenyewe kufanya biashara.
Alli, alidai Kidata, alikuwa akiuza risiti za EFds kwa bei ya asilimia tano ya kodi.
Baada ya kuzinunua kwa bei ndogo, alisema zaidi Kidata, kampuni hizo zilienda kudai marejesho ya asilimia 18 kamili TRA, hivyo kuiibia serikali.
Kwa mchezo huo, kampuni hizo zilishirikiana na Alli kukwepa kodi kwa kupewa risiti feki zinazojumuisha VAT na kodi ya mapato.
Kidata alitaja kampuni nne ambazo zimeshabainika kucheza mchezo mchafu huo na kuibia TRA jumla ya Sh. bilioni 30 kuwa ni pamoja na Skol Building Material Ltd.
Skol, Kidata alisema, kati ya mwaka 2012-2013 haikulipa VAT ya Sh. bilioni 5.46 na kodi ya mapato ya Sh. bilioni 10 na kufanya iwe imekwepa jumla ya Sh. bilioni 16.425 katika kipindi hicho.
Alisema kampuni nyingine ni Farm Plant Ltd ambayo kati ya 2010-2014 haikulipa VAT ya Sh. bilioni 5.93 na kodi ya mapato ya Sh. bilioni 4.948 na kufanya idaiwe jumla ya Sh. bilioni 10.878 ilizokwepa.
Kampuni nyingine, alisema Kidata, ni A.M Steel and Iron Mills Ltd, ambayo "kuanzia mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa VAT ya Sh. milioni 79.016 na kodi ya mapato ya Sh. milioni 131.69."
Kidata aliitaja kampuni nyingine kuwa ni A.M Trailer Manufactures Ltd ambayo kati ya 2013-2015 haikulipa VAT ya Sh. Milioni 638.221 na kodi ya mapato ya Sh. bilioni 1.063 hivyo kukwepa jumla ya Sh. bilioni 1.701
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Mlowola alisema kampuni hizo zimepewa hadi Julai 7 ziwe zimekamilisha kulipa malipo hayo vinginevyo hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.
Alisema kwa sasa Takukuru inaendelea na uchunguzi wa kuzibaini kampuni nyingine zaidi ya 300 ambazo zinajihusisha na ukwepaji kodi.
MATRILIONI
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuapisha Wakuu wa Mikoa, Rais Magufuli alisema mamlaka inamshikilia mtu aliyekuwa anachakachua mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) na kuisababishia hasara ya matrilioni ya shilingi serikali.
"Tumepoteza matrilioni ya shilingi na alikuwa anashirikiana na TRA na Brela. Bahati nzuri yuko kwenye mikono salama.
Hiyo ndiyo Tanzania," alisema Rais Magufuli.
Kutoknaa na changamoto hiyo, Rais aliwaagiza wakuu hao wa wilaya kwenda kusimamia vizuri mapato ya serikali.
Mbali na agizo hilo kwa Wakuu wa Wilaya, Serikali itaanzisha kikosi maalum cha kufuatilia kwa karibu matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) za kutoa risiti kila mfanyabiashara anapouza bidhaa au huduma.
Taarifa ya kuundwa kwa kikosi hicho ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, katika hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la 11 mjini Dodoma juzi.
Waziri Mkuu alisema uanzishwaji wa kikosi maalumu hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na udhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Serikali pia inataraji kuwajengea uwezo watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato na wanaohusika na uchunguzi na ukaguzi wa ndani wa taasisi zinazokusanya mapato," alisema Majaliwa.
"Aidha, Serikali itaimarisha usimamizi wa uadilifu na maadili ya maofisa wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ya Serikali."NIPASHE
0 comments:
Post a Comment