BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TUNDU LISSU AIPELEKESHA MAHAKAMA YA KISUTU KUFANYA KAZI HADI USIKU KATIKA KESI YA UCHOCHEZI JIJINI DAR ES SALAAM


Mbunge wa Singida Mashariki, ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, akiwasili katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, jana.

MBUNGE wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (48).

Aliibua mtikisiko wa aina yake katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana wakati alipofikishwa kukabiliana na tuhuma za uchochezi kabla ya kutolewa kwa uamuzi wa kumuachia kwa dhamana mishale ya saa 2:56 usiku.

Askari kadhaa wenye silaha walitanda kwenye mahakama hiyo na maeneo ya jirani kuanzia asubuhi na hata mishale ya saa 9:00 alasiri wakati mbunge huyo alipofikishwa chini ya ulinzi mkali.

Baada ya kupandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yake, ubishani mkali wa kisheria uliibuka na kudumu hadi giza lilipoingia mishale ya saa 2:25 usiku, ikiwa ni mojawapo ya kesi nadra za aina hiyo kunguruma hadi usiku.

Lisu alikamilisha taratibu za kujidhamini mwenyewe saa 2:56 baada ya kutimiza masharti kadhaa likiwamo la kusaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. milioni 10.

Lissu (48), alifikishwa mahakamani hapo kukabiliana na tuhuma za mashitaka matatu likiwamo la kutoa maneno ya uchochezi kwa nia ya kujenga chuki kwa wananchi dhidi ya Rais John Magufuli na serikali yake.

Upande wa Jamhuri ulimfikisha Lissu mahakamani hapo saa 9.02 na kisha akapanda kizimbani saa 9:26.

Lissu alifikishwa mahakamani hapo kwa gari dogo aina ya Toyota Corola, lenye namba T 517 DET.

ILIVYOKUWA KABLA YA KUWASILI
Kuanzia saa moja asubuhi, viunga vya Mahakama ya Kisutu vilifurika askari polisi wenye sare na pia askari kanzu waliotanda maeneo yote na pia magari kadhaa ya maji ya kuwasha yalikuwapo. Lango kuu la kuingilia mahakamani hapo lilikuwa na ukaguzi mkali kwa watu wote walioruhusiwa kuingia.

Awali, Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ZCO Cammilius Wambura, ndiye aliyeongoza askari wake kujipanga kwa kuimarisha ulinzi katika viunga vya mahakama hiyo kabla ya kuondoka saa 4.30 asubuhi kwenda kuendelea na shughuli nyingine.

Viongozi mbalimbali wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, walifika mapema katika mahakama hiyo na kubaki hapo hadi Lissu alipopandishwa kizimbani kwa ajili ya kusomewa mashtaka yake.

UBISHANI WA KISHERIA
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi na pia Mawakili wa Serikali Simon Wankyo na Paul Kadushi.

Nchimbi alianza kuwasilisha pingamizi la kuiomba mahakama kumzuia Wakili Kiongozi wa Utetezi, Peter Kibatala, kwa kudai kwamba ni shahidi wa upande wa Jamhuri na hivyo akiendelea kuwa katika jopo hilo ataathiri mwenendo wa kesi kwa upande wa Jamhuri.

Mabishano ya kuzuia uwakilishi wa Kibatala yaliendelea kwa muda wa masaa mawili hadi hakimu alipolazimika kuamuru upande wa Jamhuri kumsomea kwanza mshtakiwa mashtaka yake na ndipo uwasilishe pingamizi na pia kumuwezesha kuendelea na mwenendo wa kesi hiyo.

Kadushi alidai mshtakiwa alitenda makosa hayo Agosti 2 mwaka huu, katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Kadushi alidai mshitakiwa huyo, katika siku hiyo, akiwa katika mahakama hiyo ya Kisutu na huku akiwa na nia ya kujenga chuki kwa wananchi dhidi ya Rais na Serikali, alitoa maneno ya uchochezi akisema: “Ukitaka kujua Magufuli ni dikteta uchwara, ni pamoja na kauli zake”.

Pia mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa siku hiyo, kwa nia ya kuleta dharau katika mfumo wa utoaji haki ndani ya mahakama na kuidharau mahakama, alitoa maneno ya uchochezi kwa kusema “Kesi na mashitaka yenyewe ni ya kipuuzi na ya Kimagufuligufuli”.

Aidha, inadaiwa kwua siku hiyo kulikuwa na mwenendo wa kesi mbili za jinai ambazo zilikuwa zimekwishamalizika na akiwa na lengo la kudharau mienendo ya mahakama, Lissu alitamka: “Siwezi kufungwa, kesi na mashitaka yenyewe ni ya kipuuzi na ni ya Kimagufuli”.

Mshtakiwa huyo ambaye anatetewa na mawakili akiwamo Kibatala, alikana tuhuma hizo na baada ya hapo, Wakili Nchimbi aliwasilisha hoja kupinga uwakilishi wa Kibatala kwa kuwa ni shahidi wa upande wao.

MABISHANO JUU YA KIBATALA KUMTETEA LISSU
Wakili Nchimbi alipinga Kibatala kumwakilisha Lissu katika kesi hiyo kwa sababu za msingi juu ya shauri kwa upande wao.

Alidai akiwa kiongozi wa upande wa Jamhuri, alipitia jalada la upelelezi la Polisi kwa kina ambalo lilisababisha kuandaliwa kwa hati ya mashitaka, ambapo Kibataka, kutokana na mazingira yote ya tuhuma, alichukuliwa maelezo kama shahidi wa upande wao.

“Baada ya kuyapitia maelezo hayo, nilijiridhisha kwamba hakuna namna upande wa jamhuri utakwepa kumuita Kibatala kama shahidi katika shauri hilo,” alidai.

Alidai wanategemea kumuita Kibatala kama shahidi hivyo ni wazi kwamba kwa msimamo wa kisheria, Kitabala atalazimika kutoa ushahidi hata kama hatataka kufanya hivyo.

Wakili Nchimbi alidai wakati shauri linasikilizwa, shahidi hatakiwi kuwapo wakati mashahidi wengine wakitoa ushahidi wao na hivyo, ushiriki wa Kibatala katika mwenendo wa kesi unaathari kwa kuwa akiitwa atakuwa hastahili kuwa shahidi. Aliiomba mahakama itoe uamuzi kuwa Kibatala hastahili kuwa Wakili wa Lissu.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala alidai hoja zote za upande wa Jamhuri hazina mashiko na wala hazistahili kuitwa pingamizi la awali.

Kibatala alidai maelezo ambayo upande wa Jamhuri wanadai kuyatumia kama ushahidi, yanapaswa kuingizwa mahakamani kwa utaratibu wa kisheria, hivyo mahakama haiwezi kumlazimisha kujitoa kumwakilisha Lissu kwa maelezo ambayo hayajafanyiwa tathmini.

Pia alidai anayepima mtu ajitoe ni mahakama na kwamba yeye alihojiwa kama shahidi sawa, lakini kama wakili na hakuna uamuzi unaosema wakili akihojiwa haruhusiwi kumuwakilisha mteja wake.

“Hakuna mahala ambapo sheria inakataza kumwakilisha mshitakiwa kwa mazingira kama hayo. Naomba mahakama ilinde haki ya mshitakiwa kuwakilishwa na Kibatala na hoja za upande wa Jamhuri zitupiliwe mbali,” aliomba na Kibatala na kuongeza kwamba mahakama ikiona suala hilo ni zito ilipeleke Mahakama Kuu.

Akiwasilisha majibu ya upande wa Jamhuri kutokana na hoja za Kibatala, Wakili Kadushi alidai Kibatala wanatarajia kumuita wao kama shahidi, hivyo hawezi kucheza pande zote mbili.

Alidai pia hakuna mgogoro wa kikatiba kuifanya mahakama kupeleka shauri hilo Mahakama Kuu.

Baada ya kusikiliza mabishano hayo, Hakimu Mkeha alisema atatoa uamuzi Agosti 19, mwaka huu.

PINGAMIZI LA DHAMANA
Baada ya kuisha mabishano hayo, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika, wanaomba tarehe ya kutawa kukamilisha sehemu ya upelelezi uliobakia.

Nchimbi aliwasilisha pingamizi la dhamana kwa Lissu, akiiomba mahakama kuzuia dhamana yake kwa muda wa wiki mbili ambapo watakuwa wamekamilisha upelelezi.

“Tumepokea kiapo kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala, akiomba mshitakiwa asipewe dhamana kwa sababu kuu mbili,” alidai Nchimbi na kuwasilisha sababu hizo kwamba kwa mujibu wa hati ya kiapo, kuna taarifa za uhakika akipewa dhamana kuna uwezekano akarudia kufanya kosa hilo hilo.

Sababu nyingine ni kwamba endapo atapewa dhamana, kwa taarifa za uhakika walizonazo, kutakuwa na uingiliaji wa upelelezi unaoendelea, hivyo rai yao asipewe dhamana.

Aliiomba mahakama izuie dhamana kwa wiki mbili, kwa sababu ndani ya muda huo watakuwa wamekamilisha upelelezi wao.

Mshitakiwa Lissu aliomba kuwasilisha majibu ya pingamizi hilo yeye mwenyewe na kutaka maombi ya kunyimwa dhamana yakataliwe kwa sabau hakuna sababu za msingi katika sheria zilizopo nchini za kumnyima dhamana.

Pia alidai hakuna kifungu chochote cha sheria ambacho kinasema mahakama ikatae dhamana kwa shitaka kama hilo na sababu zilizotolewa na upande wa Jamhuri kwamba ana kesi nyingi, hizo zote ni tuhuma na hakuna uthibitisho.

WAFUASI CHADEMA WATAWANYWA
Tangu asubuhi, polisi kadhaa walikuwa wametanda mahakamani hapo wakiwamo wa kiraia ambao waliweza kuwadhibiti wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika mahakamani hapo kwa kuwatawanya.

Katika kuwazuia huko, Polisi waliwatia mbaroni watuhumiwa watano akiwamo anayedaiwa kuwa ni diwani na kisha kuwapeleka katika Kituo cha Polisi cha Kati.

Mbali na kuwazuia wafuasi hao wa Chadema, Polisi waliokuwa wakilinda katika lango la kuingilia mahakamani hapo walikuwa wakizuia pia magari kuingia lakini wakiwaruhusu viongozi wa Chadema akiwamo Mbowe na mwenyekiti mwenza wa muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia.

Viongozi wengine walioruhusiwa ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji na baadhi yao walilazimika kukaguliwa kwa mashine maalumu kabla ya kuruhusiwa. 


Mshitakiwa huyo akiwa amevalia magwanda meusi ya chama hicho na kofia yake alipelekwa katika chumba cha kuwasajili na kisha kumpeleka katika mahabusu ya mahakama.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: