BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WANANCHI WA DAR ES SALAAM WAPIGWA STOP KUSHIRIKI MAANDAMANO BATILI NA KINYUME NA SHERIA

 
MKUU wa Operesheni katika Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Lucas Mkondya amewataka wananchi wa mkoa huo kutoshiriki maandamano ya aina yoyote ambayo yako kinyume na sheria, kwani jeshi hilo limejipanga kudhibiti maandamano yoyote.

Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika Makao Mkuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Mkoa kilichopo Ukonga katika Manispaa ya Ilala.

Kauli hiyo ya Mkondya imekuja baada ya Makonda kuwataka askari hao kuhakikisha wanapambana na vurugu zozote zinazoashiria uvunjifu wa amani ikiwemo maandamano yanayotarajiwa kufanyika ya Ukuta yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kuhakikisha mkoa unabaki kuwa na amani.

Alisema kumekuwa na maagizo yanayotolewa na wanasiasa kuhusu uwepo wa maandamano, lakini ni vyema wananchi wakapuuza na kuepuka kujihusisha na maandamano hayo kwani askari hao wamejipanga kudhibiti.

"Tumejiandaa vizuri tumeyasikia maandamano ya Ukuta niwatahadharishe tu wananchi msidanganywe mkakubali kufanya maandamano tumejipanga, tutawashughulikia hatuna mchezo ni lazima wananchi mtii sheria bila kushurutishwa," alisema Mkondya.

Kwa upande wake, Makonda ametaka askari hao kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanapambana na wavunja sheria wote bila kumuonea mtu na kufanya mkoa huo kuendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu.

“Hatuko tayari kuona amani ya Mkoa wa Dar es Salaam inavunjika kwa sababu ya watu wanaokataa kutii sheria ni lazima washurutishwe bila kumuonea mtu ili amani ya Mkoa huu ibaki kuwa ya mfano katika mikoa mingine,” alisema Makonda.

Pia Makonda amewaahidi askari hao kuwa, atafanya mazungumzo na viongozi wa juu ili kuwepo utaratibu wa asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa na Polisi yarudishwe kwao ili yatumike kuboresha mahitaji mbalimbali ya askari.

“Ninyi ni watu muhimu tunaowategemea kulinda amani yetu na mali zetu, mmekubali kula kiapo cha kifo kwa ajili yetu ni lazima tuhakikishe tunaboresha mahitaji yenu na kutatua changamoto zenu,” alisema Makonda.

Aidha, Makonda pia amewaahidi kupeleka gari la kubebea wagonjwa katika hospitali ya kikosi hicho lengo likiwa ni kuondoa adha wanayokutana nayo wakati wanapotaka kusafirisha wagonjwa walio katika hali mbaya.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: