BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAFUGAJI KUTIMULIWA KWA NGUVU WILAYA BAGAMOYO NDANI YA SIKU 30 MKOANI PWANI


Picha ya maktaba/MTANDA BLOG


JAMII ya wafugaji waliovamia kwenye vijiji na vitongoji mbalimbali vinavyounda kata katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wamepewa siku 30 wawe wameshafungasha kila kilicho chao kisha kurejea walikotoka, lengo ikiwa ni kuondoa hali ya tishio la uvunjifu wa amani wilayani hapa.

Hatua hiyo imefikia katika mkutano ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga uliokutanisha jamii za wakulima, wafugaji na viongozi mbalimbali kutoka katika ngazi za Vijiji, Vitongoji, Kata, Tarafa na wilaya.


Mkutano huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa ADEM uliopo mjini hapa na kuhudhuriwa na watu wengi ukiwa na madhumuni ya kupunguza kama si kumaliza kabisa migogoro, inayohusisha mifugo kuingia katika mashamba.


Akizungumza katika mkutano huo, Mwanga alisema wakulima na wafugaji walikuwepo miaka na miaka na kwamba katika vipindi vyote walikuwa wanaheshimiana na hakukuwepo na matukio ya uvunjifu wa amani.


Alisema anashangazwa kuibuka kwa migogoro mingi wilayani hapa na kuwa viongozi wanashindwa kufanya shughuli za kimaendeleo, badala yake wanashughulika na migogoro hiyo.


“Katika sekta ya elimu, baada ya kukamilisha kazi ya madawati katika shule zetu za msingi na sekondari, hivi sasa tuna mikakati ya kuboresha majengo pamoja na mashimo ya vyoo katika baadhi ya shule zetu.


“Lakini cha kusikitisha baada ya sisi viongozi kuelekeza nguvu huko, tumekuwa na kazi ya kusikiliza migogoro ya wafugaji kila kona hali inayokwamisha juhudi za uboreshaji wa sekta hiyo, sasa nimeitisha mkutano huu ili kwa pamoja tuweze kulipatia ufumbuzi,” alisema.


Naye Mohamed Leboi ambaye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji mkoami Pwani, alisema kila upande uheshimike kwamba unafanya shughuli halali katika nchi na ipewe mahitaji yake kwa kutumia wataalamu wa ardhi na si kwa kutumia mikutano ya ardhi.


Alisema kama itatumika kwa kura hawatapewa nafasi katika maeneo hayo na kuwa maeneo ya vijiji 22 ni kweli yametengwa, lakini haikuheshimika na badala yake sehemu kubwa ipo kwa wawekezaji na matajiri kutoka jijini Dar es Salaam.


Wakichangia mada katika mkutano huo, Said Mnagusi ambaye ni Kaimu Ofisa Tarafa Miono, alisema katika eneo lake kuna matukio mengi ya uvunjifu wa amani yanayosababishwa na jamii ya wafugaji Wamang’ati, ambao wanaingiza mifugo katika mashamba kisha kushambulia wakulima.


Kwa upande wake Katibu wa Ofisi ya Mbunge Jimbo la Chalinze, Idd Swala alishauri iwekwe faini kubwa ili kukomesha vitendo vya baadhi ya jamii ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba kwa makusudi.


Akihitimisha mkutano Mwanga alisema kwa kiongozi yeyote ambaye atashindwa kusimamia, au kutekeleza maazimio hayo hatamwonea haya na kwamba serikali iliyopo madarakani ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwatetea wananchi wanyonge ambao ni wa hali ya chini wakiwemo wakulima.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: