BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MKUU WA POLISI TANZANIA (IGP) MANGU AMEKASIRIKA KWELI KWELI

 
MAUAJI ya watafiti watatu wa kituo cha Selian cha mjini Arusha yaliyotokea mkoani Dodoma mwanzoni mwa wiki yamemlazimisha Mkuu wa Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu, kuonya kuwa jeshi hilo halitawafumbia macho watu wanaojichukulia sheria mkononi.

Katika mauaji hayo yaliyotokea wilaya ya Chamwino, watafiti wawili na dereva kutoka kituo cha kilimo cha Selian walikamatwa na kuchomwa moto hadi kufa wakihusishwa na vitendo vya unyonyaji damu.

Kutokana na mauaji hayo na mengine, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini amesema jeshi hilo halitamvumilia yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo na kwamba watakaobainika watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Mangu alisema hayo juzi wakati akizungumza na kituo cha Radio One kuhusu uamuzi wa wanachi kujichukulia sheria mkononi kama ilivyotokea wiki iliyopita wilayani Chamwino.

Alisema wananchi hao walikurupuka na kusababisha mauaji na hasara bila kuwa na ushahidi kama kuna aliyewahi kunyonywa damu katika kijiji hicho na kwamba hivyo ni vitendo visivyovumilika.

Mangu alisema popote polisi walipo, wanapojulishwa matukio yoyote ambayo ni tishio la kiusalama hufika na kuchukua hatua na kwamba hakuna uhalali wa kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa tu eneo husika hakuna kituo cha polisi karibu.

“Huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine. Linapotokea tukio hili au lingine lazima tuwakamate na kuwafikisha
mahakamani, pia tunatoa elimu kwa wananchi wanapohisi kuna tukio kama hilo ni hatua gani zichukuliwe,” alibainisha.
“Kwa karne ya leo ni ngumu sana kuamini kuna mtu anaweza kumnyonya damu mwenzake.

"Ni masuala yanahusiana na ujinga wa wananchi wanaamini vitu visivyo na msingi wowote. Ni kama yanayotokea Kanda ya Ziwa kuua vikongwe kwa madai ya ushirikina.”

Alibainisha kuwa idadi ya askari nchini ni ndogo lakini wataendelea kuwatawanya kwa kadri ya mahitaji, na wanapewa vifaa ikiwamo usafiri wa kuwawezesha kuyafikia matukio kwa haraka. 


Aidha, aliviomba vyombo vya habari na wadau wa usalama kwa ujumla kusaidia kutoa elimu kwa umma ili kuachana na uelewa mdogo ambao mwisho wa siku umesababisha madhara makubwa na kuongeza wategemezi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: