UKIINGIA KATIKA ANGA LA BARAZA LA MITIHANI LA TAIFA HAYA NDIO MASWALI YA MITEGO KWA WENYE VYETI FEKI
HAWACHOMIKI! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na maswali ya mitego wanayoulizwa watu wanaofika ofisi za Baraza la Mitihani (Necta) kuomba kuhakikiwa na kupatiwa vyeti vipya kwa madai ya kupoteza vya awali walivyopatiwa baada ya kuhitimu masomo.
Tangu serikali ya awamu ya tano ilipotangaza uhakiki wa vyeti vya watumishi, Nipashe imebaini kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wanaofika kwenye ofisi za baraza hilo zilizopo Bamaga, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa malengo ya kupatiwa vyeti vipya (kwa waliopoteza au hawakuwahi kupatiwa vyeti tangu wahitimu) na kuhakiki taarifa za vyeti vyao (waliopoteza na waliosoma nje ya nchi).
Katika uchunguzi wake, gazeti hili limebaini kuwa si rahisi kwa mtu ambaye ana cheti feki kuvuka 'kigingi' cha maswali yanayoulizwa na maofisa wanaohakiki taarifa za vyeti kwenye baraza hilo kwa sasa.
Nipashe iliyopiga kambi kwenye ofisi za baraza hilo Alhamisi na Ijumaa kuchunguza namna uhakiki wa vyeti unavyofanyika, ilibaini maswali yanayoulizwa yamegawanyika katika sehemu kuu tano.
Kwanza ni historia fupi ya mtu husika anayeomba kuhakikiwa au kupatiwa cheti, inayohusisha majina yake halisi yaliyomo kwenye cheti pamoja na shule na vyuo alivyosoma.
Sehemu ya pili ni mazingira ya shule ambayo mwombaji wa cheti au uhakiki wa taaluma yake anapaswa kueleza, ilipo shule au chuo alichosoma.
Mwombaji pia anapaswa kuthibitisha uhalali wa cheti na taaluma yake kwa kutaja alama alizopata katika mitihani yake ya taifa bila kuwa na nakala ya matokeo yake.
Sehemu ya nne ni kutaja majina ya walimu wasiopungua watatu na wakuu wa shule na vyuo ambavyo mwombaji anadai kusoma.
Mwombaji pia anapaswa kutaja majina ya watu watano ambao alisoma nao shuleni au chuoni ambao kwa sasa ni wafanyakazi katika sekta yoyote (umma au binafsi).
Mmoja wa watumishi wa umma aliyefika kwenye ofisi za baraza hilo na kuhakikiwa Alhamisi iliyopita, alisema kuwa mbali na vipengele hivyo muhimu, kuna maswali mengine madogomadogo yanayotofautiana kwa kulingana na kiwango cha elimu cha mwombaji husika.
"Unapofika pale kuhikiki cheti kilichopotea au kuungua, ni lazima uwe na ripoti ya polisi na unatakiwa kulipia fedha (anataja kiasi cha fedha alicholipia) ili taarifa zako zitumwe kwa mwajiri," alisema.
Alisema kuwa kabla taarifa hazijatumwa kwa mwajiri, mwombaji huuingizwa kwenye chumba maalum kwa ajili ya mahojiano.
"Ukishaingia kwenye hicho chumba unakutana na maofisa ambao wanakuhoji. Wanakuuliza majina yako kamili wakiwa wamekunyang'anya nakala zote unazoingia nazo humo," alieleza.
"Baadaye wanakuuliza ulisoma shule gani, iko wapi, umbali na hata usafiri wa kuifikia shule hiyo. Ukimaliza hapo, wanakwambia utaje walimu watatu wa shule au chuo hicho; wanafunzi watano uliosoma nao ambao sasa wana mafanikio kazini au ni waajiriwa katika sekta yoyote.
"Unaulizwa tena masomo uliyofanyia mtihani wa taifa na anakuwa anataja somo mojamoja kwa haraka huku ukitakiwa kusema alama ulizopata. Wakati mwingine wanataja somo ambalo hukulifanyia mtihani. Baadaye wanarudia tena kukuuliza somo mojamoja kuangalia kama kweli utapatia.
"Unaulizwa pia ulianza kidato cha kwanza mwaka gani na swali moja linaweza kuulizwa zaidi ya mara tatu, lakini kwa nyakati tofauti.
"Wale jamaa si wa kawaida. Nafikiri wanatoka kitengo nyeti sana serikalini.
"Unatakiwa kutaja jina la mkuu wa shule na chuo pamoja na walimu na wakufunzi waliokufundisha. Na kilichonishangaza wakuu wa shule na chuo niliowatajia, wanawafahamu," alieleza zaidi.
Mwombaji mwingine aliyefika kwenye ofisi za baraza hilo na kuhojiwa Ijumaa, alisema watu wote waliohitimu kuanzia miaka 2010 wanapatiwa vyeti vipya kwa kuwa vyeti vyao vilitengenezwa vikiwa na picha.
Mei 26 wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka huu wa fedha, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema serikali imedhamiria kuboresha kiwango cha elimu nchini na kwamba hatua mojawapo inayochukuliwa kwa sasa ni kukagua uhalali wa vyeti vyote kwa watumishi wa umma.
Kutokana na kauli hiyo ya Profesa Ndalichako ambayo pia inaendana na dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kusafisha uozo katika kila sekta, ndipo harakati za ukaguzi wa vyeti vya shule na vile vya kitaaluma ziliposhika kasi na kuwafanya watu wengi wakimbilie Necta kuhakiki na kuomba vyeti vipya kwa madai ya kupoteza walivyopewa awali.
Hadi sasa, taasisi mbalimbali za umma zikiwamo halmashauri zinaendelea na uhakiki wa vyeti vya watumishi wao.
0 comments:
Post a Comment