WAZIRI AFARIKI DUNIA WAKATI AKIPANDA NGAZI ZA OFISI YAKE
Waziri wa zamani wa sheria nchini Rwanda Jean De Dieu Mucyo, ambaye amekuwa akihudumu kama seneta, amefariki dunia baada ya kuanguka kwenye ngazi akielekea ofisini mwake.
Idara ya mawasiliano ya Bunge la Rwanda imethibitisha kifo cha Seneta Jean de Dieu Mucyo kilichotokea Jumatatu asubuhi.
Kifo cha Seneta huyo kimeelezewa kuwa pigo kubwa kwa chombo cha kutunga sheria ikizingatiwa "mchango wake na nafasi alizochukua zenye uhusiano na masuala ya sheria".
Marehemu alikuwa waziri wa sheria mwaka 1999, wadhifa aliokalia mpaka mwaka 2003, kabla ya kuwa mwanasheria mkuu wa Rwanda alipokalia kiti hicho kwa miaka 3.
Bw Mucyo pia atakumbukwa nchini Rwanda kama mkereketwa wa kupambana dhidi ya mauaji ya kimbari.
Aliongoza tume iliyochunguza nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda na kuongoza tume ya taifa ya kupambana dhidi ya mauaji hayo.
Aliteuliwa kuwa Seneta wa nchi hiyo mapema mwaka jana.BBC
0 comments:
Post a Comment