RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete, juzi alisafiri nje ya nchi baada ya baadhi ya watu waliokuwa katika ujumbe wake, kukamilisha taratibu ambazo hapo awali zilishindikana na hivyo kuachwa na ndege.
Kikwete na ujumbe wake ambao walikuwa wakielekea nchini Abu Dhabi (Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu – UAE), walishindwa kusafiri Jumamosi iliyopita kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates, iliyokuwa inaondoka saa 10:30 jioni baada ya baadhi ya wajumbe hao kutokuwa na viza.
Chanzo cha habari kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kililidokeza gazeti hili kuwa Kikwete ambaye alikuwa ameongozana na mke wake, Salma pamoja na ujumbe wa watu wengine wane, alilazimika kuondoka juzi saa 6:20 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Oman (Oman Air).
Taarifa hizi mpya zinathibitisha kile ambacho kiliripotiwa na gazeti la MTANZANIA Jumapili, kwamba Kikwete na wasaidizi wake huenda wangeondoka Jumapili baada ya kuwa wamekamilisha taratibu.
Gazeti hili kupitia kwa vyanzo vyake, lilithibitishiwa kwamba Kikwete na ujumbe wake walikwama kusafiri kwa takribani saa nane, na alilazimika kufanya hivyo baada ya watu wanaoitwa ‘washauri’, kumshauri kuweka sawa tatizo lililojitokeza.
Tangu MTANZANIA Jumapili litoe habari hiyo, kumekuwa na shauku kubwa ya kujua kilichotokea kwa rais huyo mstaafu hadi kushindwa kusafiri.
Miongoni mwa waliofuatilia kwa ukaribu ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kupitia mtandao wake wa twitter, kilionyesha mshangao wa kuwapo kwa tukio hilo, hasa baada ya JK kuwa amekwishafika Abu Dhabi.
Jana gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka ili kujua kama akaunti hiyo ya twitter inamilikiwa na chama hicho.
“Siwezi kusema ndiyo au siyo kwa sasa, hiyo twitter sijaiona, nipo nje ya ofisi… Mimi siingii kwenye hayo mambo, wanaingia vijana,” alisema Sendeka.
Hata hivyo, kuna taarifa kuwa akaunti hiyo inamilikiwa na mmoja wa watoto wa kigogo wa chama hicho.
MTANZANIA Jumapili, juzi liliripoti juu ya kuwako kwa taarifa ambazo hazijathibitishwa, zilizodai kuwa imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya wasaidizi wa Kikwete kusafiri nje ya nchi bila kuwa na viza, na kwamba tukio la safari ya Jumamosi kukwama lisingetokea kwa bahati mbaya kama ilivyoonekana.
Msaidizi mmoja wa Kikwete aliyezungumza na gazeti hili Jumamosi, alikiri kuwapo kwa tukio hilo la kushindwa kusafiri na alisema lilitokea wakati mizigo ikiwa tayari imepandishwa ndani ya ndege ya Emirates.
Kwa mujibu wa msaidizi huyo, walilazimika kushusha mizigo hiyo ili kukamilisha kwanza taratibu walizotakiwa kuzikamilisha.
Msaidizi huyo wa Kikwete alikiri kiongozi huyo mstaafu na ujumbe wake walikuwa wanaelekea Abu Dhabi na ilikuwa wapande ndege hiyo ya Emirates hadi Dubai na kisha kuendelea na usafiri mwingine.
Ofisa mmoja wa juu serikalini ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu maalumu, akizungumza na na gazeti hili jana alisema: “Ni kweli Kikwete na ujumbe wake walishindwa kusafiri siku ya Jumamosi kwa Shirika la Ndege la Emirates baada ya baadhi ya wasaidizi wake kuonekana kuwa na shida kwenye viza.”
Kwa mujibu wa ofisa huyo ambaye alisema hata yeye amefuatilia kwa undani suala hilo, pamoja na shida hiyo kutokea, rais huyo mstaafu aliruhusiwa kusafiri kwa ndege hiyo, ila washauri wakasema ni vyema aliweke sawa jambo hilo ili aweze kuondoka.
“Sio kama alizuiwa, hapana, viza za wasaidizi wake zilikuwa hazijasoma kwenye system (mfumo), baadaye aliruhusiwa ila washauri walisema ni vyema ali-clear (aliweke sawa) kwanza jambo hilo ndipo aondoke.
“Halafu jambo jingine, kama imetokea shida, kwa mtu kama Kikwete kwa hadhi yake anaambiwa akiwa nyumbani, mambo kama yapo sawa sawa ndio anakwenda airport (uwanja wa ndege),” alisema ofisa huyo.
Juzi MTANZANIA Jumapili lilidokezwa na chanzo chake kutoka JNIA kuwa rais huyo mstaafu na ujumbe aliokuwa ameongozana nao alikwama kusafiri kuelekea nchini Dubai.
Chanzo hicho kilisema: “Kikwete kama Kikwete yeye hakuwa na shida kwa sababu ana Diplomatic Passport, watu wengine ndio hawakuwa na viza.
“Kwa kawaida International flight (ndege za kimataifa) kaunta zinafungwa saa moja kabla ya ndege kuruka, na ndege waliyokuwa waondoke nayo ilikuwa inaondoka saa 10:30 jioni, viza za hao watu zilikuja saa 10:00 wakati kaunta zikiwa zimefungwa.”
Chanzo kilisema kwa kiongozi kama Kikwete, linapotokea tatizo kama hilo, wakati mwingine unaweza kupiga simu kwa watu wa Uhamiaji huko anakoelekea, lakini hilo halikuwezekana kwa sababu tayari ndege ilikuwa imeondoka.
Juzi, MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Msemaji wa JNIA, Nuru Nyoni, azungumzie sababu za Kikwete na ujumbe wake kukwama, alisema suala hilo lipo chini ya Uhamiaji.
Baada ya juzi Ofisa Uhusiano wa Idara ya Uhamiaji, Abasi Ilovia kutoa ahadi ya kujibu maswali yote kuhusi kilichotokea hadi rais huyo mstaafu kushindwa kusafiri kwa ndege ya Emirates, jana alipopigiwa simu kwa mara nyingine alionekana kukwepa maswali ya mwandishi.
Ilovia alipoulizwa juu ya kile alichoahidi kuzungumza na gazeti hili alisema: “Nyinyi waandishi wa habari msiwe watu wa kukurupuka, hili suala ni nyeti sana, kwanini msiende hapo uwanja wa ndege, hebu nendeni hata kwa miguu basi.”
Mwandishi wa habari hizi alipomjibu kuwa waliwasiliana na JNIA kupitia kwa msemaji wake, Nuru Nyoni ambaye alisema suala hilo lipo Uhamiaji, Ilovia alisema: “Ngoja nimtafute huyo Nuru.”
Alipoulizwa ni kwanini tangu Jumamosi ameshindwa kumtafuta Nuru na kwanini ameshindwa kutekeleza ahadi yake ya kujibu maswali ya MTANZANIA, ofisa huyo alijibu kwa kifupi: “Naona wewe ni mgeni kwenye uandishi wa habari.”
Mwandishi wa habari hizi alipomweleza kuwa ana miaka karibu kumi chumba cha habari alijibu tena: “Basi njoo kesho asubuhi.”
Juhudi za gazeti hili kumtafuta msemaji huyo wa Uhamiaji zinaendelea.
Jumamosi saa 1:00 usiku Ilovia, alipopigiwa simu yake ya kiganjani, aliomba apigiwe baada ya dakika kumi ili aweze kuwasiliana na watu waliopo JNIA kwa taarifa zaidi.
Alipopigiwa tena baada ya muda huo, alisema anasubiri majibu kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji cha Uwanja wa Ndege.
Hata hivyo, alipopigiwa tena kwa mara ya tatu, hakupokea simu hadi gazeti linakwenda mtamboni.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment