SARAH Mchele ni mama wa watoto wawili mwenye maisha yasiyo ya kawaida kwa siku 69 mpaka kufikia jana, ambaye bila msaada wa Serikali ataendelea kulazimika kunyeshewa mvua nyakati nyingine baada ya kupigwa na baridi.
Akizungumza na Nipashe kwenye kata ya Hamgembe, Manispaa ya Bukoba jana, Sarah alisema amekuwa akiishi kwenye hema ambalo alipewa msaada siku tatu baada ya tetemeko la ardhi la Septemba 10, ambalo lilisababisha vifo vya watu 17.
Mbali na vifo hivyo, tetemeko hilo ambalo lilielezwa kuwa na ukubwa wa 5.9 katika vipimo ya majanga hayo kimataifa, na kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa earthquaketrack.com, liliacha majeruhi 170 waliohitaji kulazwa katika hospitali mbalimbali huku 83 wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa.
Aidha, tetemeko hilo ambalo ndilo kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini katika miaka ya 2010, lilisababisha nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,254 kupasuka kuta.
Mchele anasema alipokea msaada wa hema moja na blanketi kwa ajili yake na wanae wawili wenye umri wa miaka minne na mwaka mmoja Septemba 13, na tangu hapo hajapatiwa msaada mwingine.
Mchele alisema uongozi wa kata hiyo, kupitia kwa Afisa Mtendaji, ulipita kuwaeleza kuwa wavumilivu wakati wakisubiri Serikali iwasaidie kurejesha makazi yao.
Alisema hunyeshewa na mvua yeye na wanawe wakati hema linapoezuliwa na upepo. Aidha, katika baadhi ya siku hukesha wakiwa wamesimama kwa sababu maji huingia mpaka kwenye eneo analolala na watoto.
Mvua inapokuwa kubwa? Mchele huenda kujificha kwenye nyumba za majirani zilizopata mipasuko, kitu ambacho anadai ni hatari kwa maisha ya familia hiyo.
"Naenda kwa jirani, naomba angalau wanangu wajikinge lakini unaambiwa nyumba imejaa au hakuna nafasi," alisema Mchele.
"Unakuwa hauna jinsi, naamua kujimbanza kwenye nyumba iliyopasuka ili wanangu wasilowane... wataniugulia wakati sina hata hela.
"Sehemu niliyokuwa nafanya kazi (tajiri) alifunga kwa vile nyuma ile ilianguka.
"Yaani serikali wangetusaidia kiasi chochote cha pesa tupate kuokoa hawa watoto; hasa nyumba hata za muda tu jamani.
"Wanajenga shule kabla ya makazi yetu. Shule hizo watasoma kina nani kama watoto wenyewe wanaotegemewa kusajiliwa kwenye hizo shule ndio hawa wanaohangaika na maradhi ya nimonia kila wakati (kwa) sababu ya kupingwa na baridi la kila siku?
"Miezi miwili sasa na siku, ni baridi tu. Hizo elimu (shule) zenyewe watahudhuria vizuri kweli?"
Naye Jackson Charles, mkazi wa mtaa wa Kashabo, kata Hamgembe alisema aliwahi kupata msaada kutoka shirika la Msalaba Mwekundu baada ya kulala nje kwa wiki mbili tangu Septemba 10.
Alisema nyumba aliyokuwa akiishi na familia yake ya watoto watano ilianguka chumba kimoja na vingine kubaki na mipasuko mikubwa.
"Yaani kwa kipindi chote hicho serikali wamekaa kimya tu, angalau watupe vianzio vya kujenga nyumba zetu. Hali zetu (kiuchumi ni) ngumu (kwani) imegusa hadi maeneo ya kazi zetu," alisema Cherles.
"Hatuna chochote ndani (Serikali) itusaidie."
MATUMIZI YA FEDHA
Kasi ndogo ya utoaji wa misaada kwa waathirika wa tetemeko ilichukua sura mpya katikati ya wiki iliyopita baada ya wabunge wa mkoa wa Kagera, bila kujali vyama wanakotoka, kuamua kukutana kwa dharura kutoa kauli moja kwa Serikali.
Wabunge wakiwa na mkakati huo, Ofisi ya Waziri Mkuu yenye jukumu la kuratibu misaada wakati wa maafa nayo ilitoa ufafanuzi wa kile ilichokiita upotoshaji wa matumizi ya fedha zilizotolewa kusaidia waathirika.
Aidha, Mwenyekiti wa kamati ya maafa ya mkoa huo, ambae ni Mkuu wa Mkoa, Meja Jeneral mstaafu Salim Kijuu aliainisha mchanganuo Novemba 15 wakati wa uzinduzi wa ugawaji misaada kwa makundi maalumi katika kata ya Kashai, Manispaa ya Bukoba.
Alisema kaya 200 zitapata vifaa vya ujenzi kwa awamu ya kwanza, ikifuatiwa na kaya 170 zitakazokuwa zimebaki kwa awamu ya pili.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Rwegasira Mukasa (CCM), aliiambia Nipashe kwa simu kuwa wabunge wa mkoa wa Kagera wameamua kukutana kwa dharura ndani ya wiki kulijadili suala hilo.
"Ndani ya siku tatu, nne wabunge wote wa mkoa wa Kagera tutakutana na kutoka na kauli moja," alisema Mukasa.
“Pale msaada unapotolewa kwa waathiriwa, wapo wanaoguswa na mwathiriwa moja kwa moja, aliyemuona analala nje, na si kupeleka msaada katika kituo cha afya ya elimu.
“Tunajiandaa na kikao ambacho ni cha dharura, wabunge wote wa Kagera tutajadili suala hili maana suala hili lilitokea wakati tukiwa bungeni na hatukupata muda wa kulijadili kwa sababu kulikuwa na misiba."
Naye Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare, akizungumzia suala hilo wiki iliyopita, alisema serikali kuelekeza fedha za msaada za waathiriwa wa tetemeko kwenye miradi ya maendeleo kunaonyesha namna inavyoshindwa kuandaa bajeti ya kitengo cha maafa kusaidia wanaokumbwa na maafa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari wiki iliyopita na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Uledi Mussa, ilisema serikali kwa kushirikiana na wadau imesaidia waathirika kwa kutoa matibabu bure kwa majeruhi wote 560 na kuandaa na kugharimia mazishi ya watu 17 waliofariki dunia, na kutoa mkono wa pole wa Sh. milioni 1.8 kwa familia zilizopatwa na msiba.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa tathmini za wataalamu na makadirio ya awali yanabainisha takribani Sh. bilioni 104.9 zinahitajika kurejesha hali ya mkoa wa Kagera kufuatia maafa hayo.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ SIKU 70 AKIISHA MAISHA DUNI BAADA YA NYUMBA KUBOMOKA KATIKA TETEMEKO LA ARDHI BUKOBA
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment