BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUYU NDIYE SAMUEL SITTA

 
Samuel John Sitta alizaliwa Desemba 18, 1942 huko wilayani Urambo Mkoa wa Tabora. 

Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo kati ya mwaka 1950 – 1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 - 1957 na kuendelea na masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge Middle School”. 

Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo ya sekondari Shule ya Wavulana Tabora yaani “Tabora Boys” kidato cha I – IV na cha V – VI.

Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, Sitta alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Sheria (L LB) mwaka 1964 na kuhitimu mwaka 1971.

Sitta amesoma shahada yake kwa miaka 7 kwa sababu mwaka 1966, wakati yuko mwaka wa pili na akiwa kiongozi wa wanafunzi UDSM, wanafunzi waligoma na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa mishahara yao baada ya JKT. 


Hoja ya wanafunzi ilikuwa na mantiki kubwa, kwamba mbona vigogo wa serikali na wanasiasa wanalipwa mishahara minono na marupurupu makubwa?

Baada ya shinikizo hilo la wanafunzi Mwalimu Julius Nyerere alikubali kupunguza mshahara wake wa Sh4,000 bila kodi akaagiza pia mishahara ya mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili. 


Miezi miwili baadaye akatangaza Azimio la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi hao.

Watukutu wawili – Sitta na Wilfred Mwabulambo (Wote sasa marehemu) na wengine kadhaa – waliojitia wazimu na kutetea kile walichokiita haki zao, (haki za wakulima na wafanyakazi), walimshutumu Mwalimu Nyerere kwa maneno makali wakidai “…ni heri wakati wa ukoloni kuliko utawala wa Mwalimu”.

Mwalimu Nyerere alikasirika na kuwafukuza chuo wanafunzi wote 400 kwa kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao”. 


Miezi kumi baadaye, baada ya Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia akaamua kuwarudisha chuoni wanafunzi 392. Viongozi wa mgomo; Sitta na wenzake 7 walitiliwa ngumu, hawakurejeshwa chuoni.

Busara za viongozi wa chuo zilifanya Mwalimu aliliwe zaidi na kuandikiwa barua mbili maalumu na chuo zenye Kumb. Na. C3/Sa.13 ya 2/3/1967 na C3/Ss.13 ya 9/07/1967. 


Mwalimu alikubali kilio hicho na kuwaruhusu vijana hao wanane warudi kwa sharti kwamba wale watukutu wawili (Sitta na Mwabulambo) watandikwe viboko na “Mwalimu Nyerere” mwenyewe. 

Hii ndiyo ilikuwa pona ya Sitta ambaye alirejea UDSM na kuendelea na masomo kwa miaka kadhaa hadi alipohitimu mwaka 1971.

Wakati Sitta anarudi chuoni tayari alikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya “CALTEX OIL” kama Meneja wa Tawi (1967 – 1969) na mwaka 1969 – 1975 aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kama Katibu na Mkurugenzi wa Utawala.

Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua kujiendeleza kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo Kikuu cha IMEDE ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huohuo 1976.

Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta alikuwa kiongozi wa juu wa CCM na serikali akiwa mbunge, mkuu wa mkoa na Waziri katika nyakati tofauti na ameendelea kuwa mbunge na waziri katika mfumo wa vyama vingi.

Sitta alimuoa Margareth Simwanza Sitta
Mbio za ubunge
Enzi za chama kimoja 1975 - 1995 Sitta alikuwa mbunge wa Jimbo la Urambo (kabla halijagawanywa na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alifanikiwa kuwa waziri kwa nyakati tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa Waziri za Katiba na Sheria.

Mwaka 1995 Sitta aliingia kwenye mapambano mapya ya siasa za vyama vingi na kwa bahati mbaya akawa mmoja wa vigogo walioangushwa na wabunge wa NCCR. 


Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob Abraham. Msina alishinda kwa kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta.

Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la siasa mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu na aliwashinda wapinzani wake wakuu Lumatiliza Yotamu Lubungila wa NCCR na Wilson George Ntakamulenga wa CUF. 


Sitta alipata kura 28,660 (72.3%) na kurejesha heshima yake jimboni Urambo Mashariki. Kurudi kwa nguvu kulimpa nafasi ya kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge la Tanzania na akaliongoza Bunge la Tisa aliloliita bunge la Viwango Na Kasi "Speed and Standards" kwa mafanikio na changamoto nyingi.

Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa (CHADEMA) na Zombwe Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 (70.47%). 


Baada ya ushindi huo, Sitta alijaribu tena kuwania uspika bila mafanikio; utendaji wake wa kuiuma serikali na wakati mwingine kuipuliza kwenye Bunge la Tisa ulimfanya achukiwe na serikali.

Ilipoonekana ana nguvu akatengenezewa “chui wa karatasi” (mshindani), Andrew Chenge. Chenge naye akachukua fomu ya uspika ghafla, likatengenezwa ‘zengwe’ kuwa wagombea wote wana nguvu, hapo CCM ikapata mwanya wa kutamka kuwa haiwataki wote ili kuondoa mvutano. 


Sitta akapoteza ndoto za uspika na ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda.

Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza la Mawaziri mwaka 2010 alimpa Sitta Wizara ya Afrika Mashariki kama Waziri,vilevile alihamishiwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.

Mbio za urais

Samuel John Sitta alianza mbio za urais “kimyakimya” tangu alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010). 


Kuna nyakati alikuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti huku akionyesha kuwa nchi ina viongozi thabiti na hawajapewa uongozi mkuu wa nchi, akiwemo yeye.

Hata alipoliongoza Bunge la Katiba mwaka 2014, mara nyingi Sitta alionekana kama mtu mwenye shauku kubwa na urais na alipohojiwa, mara kwa mara, juu ya urais alionyesha ana ndoto hizo. Mara kadhaa, alilalamika kuwa wala rushwa wakubwa wanampiga vita kwa sababu ni msafi.

Katika Uchaguzi wa 2015, Sitta alitangaza nia ya kuwania Urais na alichukua fomu ya kugombea urais kupita chama cha Mapinduzi ambapo baada ya uchaguzi wa ndani chama, John Magufuli ndo jina lililofanikiwa kupenya na kuteuliwa na chama kugombea Urais wa Tanzania.

Mungu Ailaze Roho Ya Marehemu Mahali Pema Peponi Amen.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: