BAADA ya gharama za matibabu ya ugonjwa wa homa ya ini (Hepatitis B) kuwa janga linalofanya Watanzania wengi kupoteza maisha yao kutokana na kushindwa gharama zake, serikali sasa imepata ufadhili wa tiba ya ugonjwa huo kwa kipindi cha miaka mitano.
Tiba hiyo itaanza kutolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ambako inatarajia kuanza kufanya uchunguzi wa virusi hivyo na kutoa tiba ya bure kwa kutumia dawa ya Tenofovir kuanzia Desemba Mosi, mwaka huu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, daktari bingwa wa magonjwa ya ini na matumbo, John Rwegasha alisema utaratibu wa kutoa huduma hiyo utafanyika kwa ushirikiano na ufadhili wa wadau wa maendeleo kutoka Kitengo cha Udhibiti wa Magonjwa nchini Marekani.
“Tiba hii hasa ni katika kupima wingi na kinga ya virusi hivi mwilini pamoja na tiba za ugonjwa huu kwa kutumia dawa hiyo kwa kipindi chote cha miaka mitano ya mpango huo,” alisema Dk Rwegasha na kuongeza: “Mpango huu una lengo pia la kujenga uwezo wa ndani wa nchi ili kufanya tiba kuwa endelevu katika miongozo inayotolewa juu ya tiba ya ugonjwa huu na Shirika la Afya Duniani (WHO) hususan katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.”
Alisema asilimia tano ya wagonjwa wa homa ya ini hawaponi, hivyo kuendelea kuleta maambukizi sugu mwilini na hasa kwenye ini na figo na hivyo baada ya miaka 10 na kuendelea, ini husinyaa na kupata magonjwa nyemelezi, tumbo kujaa maji na figo kushindwa kufanya kazi huku asilimia 95 ya wagonjwa miili yao hujitengenezea kinga za kupambana na virusi ndani ya miezi sita na kupona kabisa.
“Mgonjwa mwenye ugonjwa huu inabidi kutumia dawa hizo kwa muda mrefu usiopungua miaka mitano kumwezesha mgonjwa kujitengenezea kinga inayojiwezesha kupambana na ugonjwa huo,” alieleza Dk Rwegasha.
Alisema ugonjwa huo unashabihiana na ugonjwa wa Ukimwi hasa katika njia za maambukizi kama kufanya ngono zisizo salama, kuchangia sindano na vitu vyenye ncha kali, kupewa damu yenye maambukizi na pia kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Aidha, alisema inakadiriwa kuwa watu wanane kati ya 100 wana maambukizi ya ugonjwa huo na kwamba asilimia 60 ya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili waliokutwa na saratani ya ini, inatokana na maambukizi ya virusi hivyo.
“Utafiti unaonesha kuwa uwezekano wa kupata ugonjwa huu ni mara kumi zaidi ya maambukizi ya Ukimwi ingawa changamoto kubwa ni uelewa kwa jamii ukilinganisha na ugonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na magonjwa mengine ya kuambukiza,” alifafanua na kutoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili wafanyiwe uchunguzi zaidi na kupata tiba baada ya kupata ufadhili huo ambao ulikuwa ukimhitaji mgonjwa kutumia fedha nyingi.
Alisema hata hivyo utaratibu utabaki ule ule wa mgonjwa kufika hospitali kwa gharama za kufungua faili, kumuona daktari na kupima vipimo vya awali kisha kuingia katika huduma ya kupima wingi wa virusi na pia kinga ya mwili na kupatiwa dawa kama itahitajika.
Alisema kwa kawaida dalili za ugonjwa huo zinapojitokeza, huwa katika hatua za mwisho za ugonjwa ambapo ini huwa limeshaharibiwa kiasi kikubwa na hivyo tiba za magonjwa nyemelezi hutolewa kusaidia kuyapunguza makali, na wakati mwingine ini huwa limeshambuliwa na saratani na hivyo nafasi ya mgonjwa kuishi hupungua na kuwa chini ya kipindi cha mwaka mmoja.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment